< 2 Wakorintho 7 >

1 Wapenzi, kwa kuwa tunazo ahadi hizi, basi na tujitakase nafsi zetu kutokana na kila kitu kitiacho mwili na roho unajisi, tukitimiza utakatifu kwa kumcha Mungu.
Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa, na tuishi kwa kumcha Mungu.
2 Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote.
Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote.
3 Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo, kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja.
Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, ninyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja.
4 Mara nyingi najivuna kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.
Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno.
5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na raha. Tulisumbuliwa kila upande, kwa nje kulikuwa na mapigano na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu.
Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: nje ugomvi; ndani hofu.
6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito.
Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito.
7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.
Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa ninyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana.
8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu,
Maana, hata kama kwa barua ile yangu nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda.
9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.
Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru ninyi kwa vyovyote.
10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti.
Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu, husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo.
11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo.
Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: ninyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Ninyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili.
12 Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu.
Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu.
13 Kwa ajili ya haya tumefarijika. Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.
Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo.
14 Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kila kitu tulichowaambia ninyi, kilikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia.
Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia ninyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli mtupu.
15 Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, na kumpokea kwa hofu na kutetemeka.
Hivyo upendo wake wa moyo kwenu unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi ninyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka.
16 Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.
Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea ninyi kabisa katika kila jambo.

< 2 Wakorintho 7 >