< 2 Wakorintho 11 >

1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo.
Nahisi kwamba mngevumiliana na mimi katika baadhi ya upumbavu. Lakini kwa kweli mnavumiliana na mimi.
2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi.
Kwa kuwa ni mwenye wivu kuhusu ninyi. Nina wivu wa Mungu kwa ajili yenu, tangu nilipowaahidi ninyi kwenye ndoa ya mume mmoja. Niliahidi kuwaleta ninyi kwa Kristo kama bikra safi.
3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.
Lakini ninaogopa kwamba kwa namna fulani, kama nyoka alivyomdanganya Eva kwa hila yake, mawazo yenu yanaweza kupotoshwa mbali kutoka kwenye ibada halisi na safi kwa Kristo.
4 Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.
Kwa kuwa kwa mfano kwamba mtu fulani akaja na kutangaza Yesu mwingine tofauti na yule tuliyewahubiri. Au kwa mfano kwamba mkapokea roho mwingine tofauti na yule mliyempokea. Au kwa mfano kwamba mkapokea injili nyingine tofauti na ile mliyoipokea. Mkavumilia mambo haya vema inatosha!
5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.”
Kwa kuwa nadhani kwamba mimi si miongoni mwa walio duni kwa hao wanaoitwa mitume-bora.
6 Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
Lakini hata kama mimi sijafundishwa katika kutoa hotuba, siko hivyo katika maarifa. Kwa kila namna na katika mambo yote tumelifanya hili kujulikana kwenu.
7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo?
Je, nilifanya dhambi kwa kujinyenyekeza mwenyewe ili ninyi muweze kuinuliwa? Kwa kuwa nilihubiri kwa uhuru injili ya Mungu kwenu.
8 Niliyanyangʼanya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi.
Nilinyang'anya makanisa mengine kwa kupokea msaada kutoka kwao ili kwamba ningeweza kuwahudumia ninyi.
9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia.
Wakati nilipokuwa nanyi na nilikuwa katika uhitaji, sikumlemea yeyote. Kwa kuwa mahitaji yangu yalitoshelezwa na ndugu waliokuja kutoka Makedonia. Katika kila kitu nimejizuia mwenyewe kutokuwa mzigo kwenu, na nitaendelea kufanya hivyo.
10 Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili.
Kama kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, huku kujisifu kwangu, hakutanyamazishwa katika sehemu za Akaya.
11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda!
Kwa nini? Kwa sababu siwapendi? Mungu anajua nawapenda.
12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
Lakini kile ninachokifanya, nitakifanya pia. Nitakifanya ili kwamba niweze kuzuia nafasi ya wale wanaotamani nafasi ya kuwa kama tulivyo katika kile kile wanachojivunia.
13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo.
Kwa kuwa watu wale ni mitume wa uongo na watendakazi wadanganyifu. Wanajigeuza wenyewe kama mitume wa Kristo.
14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru.
Na hii haishangazi, kwa kuwa hata Shetani hujigeuza mwenyewe kama malaika wa nuru.
15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
Hii haina mshangao mkubwa kama watumishi wake pia kujigeuza wenyewe kama watumishi wa haki. Hatma yao itakuwa kama matendo yao yastahilivyo.
16 Nasema tena, mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo.
Nasema tena: Basi na asiwepo mtu yeyote anayefikiri mimi ni mpumbavu. Lakini kama mkifanya, nipokeeni mimi kama mpumbavu ili niweze kujisifu kidogo.
17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga.
Kile ninachosema kuhusu huku kujiamini kwa kujivuna hakuhukumiwi na Bwana, lakini nazungumza kama mpumbavu.
18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu.
Kwa vile watu wengi hujivuna kwa jinsi ya mwili, nitajivuna pia.
19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana!
Kwa kuwa mlichukuliana kwa furaha na wapumbavu, ninyi wenyewe mna busara!
20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyangʼanya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya.
Kwa kuwa mnachukuliana na mtu kama akikutia utumwani, kama husababisha mgawanyiko kati yenu, kama akiwatumia ninyi kwa faida yake, kama akijiweka juu hewani, au kama akiwapiga usoni.
21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo! Lakini chochote ambacho mtu mwingine yeyote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo.
Nitasema kwa aibu yetu kwamba sisi tukuwa dhaifu sana kufanya hivyo. Na bado kama yeyote akijivuna— nazungumza kama mpumbavu— mimi pia nitajivuna.
22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu.
Je, wao ni Wayahudi? Na mimi ni hivyo. Je, wao ni Waisraeli? Na mimi ni hivyo. Je, wao ni uzao wa Abrahamu? Na mimi ni hivyo.
23 Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi.
Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kama nilirukwa na akili zangu. ) Mimi ni zaidi. Nimekuwa hata katika kazi ngumu zaidi, mbali zaidi ya kuwa vifungoni, katika kupigwa kupita vipimo, katika kukabili hatari nyingi za kifo.
24 Mara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja.
Kutoka kwa Wayahudi nimepokea mara tano “mapigo arobaini kutoa moja.”
25 Mara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa,
Mara tatu nilipigwa kwa fimbo. Mara moja nilipigwa mawe. Mara tatu nilinusurika melini. Nimetumia usiku na mchana katika bahari wazi.
26 katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.
Nimekuwa katika safari za mara kwa mara, katika hatari za mito, katika hatari za majambazi, katika hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, katika hatari kutoka kwa watu wa mataifa, katika hatari ya mji, katika hatari ya jangwa, katika hatari ya bahari, katika hatari kutoka kwa ndugu waongo.
27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi.
Nimekuwa katika kazi ngumu na katika maisha magumu, katika usiku mwingi wa kutolala, katika njaa na kiu, mara nyingi katika kufunga, katika baridi na uchi.
28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote.
Mbali na kila kitu kingine, kuna msukumo wa kila siku juu yangu wa wasiwasi wangu kwa ajili ya makanisa.
29 Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?
Nani ni dhaifu, na mimi siyo dhaifu? Nani amesababisha mwingine kuanguka dhambini, na mimi siungui ndani?
30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu.
Kama ni lazima nijivune, nitajivunia kuhusu kile kinachoonyesha udhaifu wangu.
31 Mungu na Baba wa Bwana Yesu, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. (aiōn g165)
Mungu na Baba wa Bwana Yesu, yeye ambaye anatukuzwa milele, anajua kwamba mimi sidanganyi. (aiōn g165)
32 Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata.
Kule Dameski, mkuu wa mkoa chini ya mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Dameski ili kunikamata.
33 Lakini nilishushwa kwa kapu kubwa kupitia katika dirisha ukutani, nikatoroka kutoka mikononi mwake.
Lakini niliwekwa kikapuni, kupitia dirishani katika ukuta, na nikanusurika kutoka mikononi mwake.

< 2 Wakorintho 11 >