< 2 Wakorintho 10 >

1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi!
Mimi Paulo, mwenyewe nawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo. Mimi ni mpole wakati nikiwa mbele yenu, Lakini ninaujasiri kwenu wakati nikiwa mbali nanyi.
2 Nawaomba nitakapokuja kwenu nisiwe na ujasiri dhidi ya watu fulani, kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata namna ya ulimwengu huu.
Nawaomba ninyi kwamba, wakati nikiwepo pamoja nanyi, sitahitaji kuwa jasiri na kujiamini kwangu mwenyewe. Lakini nafikiri nitahitaji kuwa jasiri wakati nikiwapinga wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa jinsi ya mwili.
3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo.
Kwa kuwa hata kama tunatembea katika mwili, hatupigani vita kwa jinsi ya mwili.
4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome,
Kwa kuwa silaha tunazotumia kupigana si za kimwili. Badala yake, zina nguvu ya kiungu ya kuharibu ngome. Zinaondosha kabisa mijadara inayopotosha.
5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo,
Pia, tunaharibu kila chenye mamlaka kijiinuacho dhidi ya maarifa ya Mungu. Tunalifanya mateka kila wazo katika utii kwa Kristo.
6 tena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, kutii kwenu kutakapokamilika.
Na tunapata utayari wa kuadhibu kila matendo lisilo na utii, mara tu utii wenu unapokuwa kamili.
7 Angalieni yale yaliyo machoni penu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Kristo, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Kristo, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo.
Tazama kile kilichowazi mbele yenu. Kama yeyote anashawishika kwamba yeye ni wa Kristo, na hebu ajikumbushe yeye mwenyewe kwamba kama tu alivyo ni wa Kristo, hivyo ndiyo na sisi pia tuko hivyo.
8 Basi hata kama nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana alitupa ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya.
Kwa kuwa hata nikijivuna kidogo zaidi kuhusu mamlaka yetu, ambayo Bwana aliyatoa kwa ajili yetu kuwajenga ninyi na siyo kuwaharibu, sitaona haya.
9 Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu.
Sihitaji hili lionekane kwamba nawatisha ninyi kwa nyaraka zangu.
10 Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni dhaifu na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.”
Kwa vile baadhi ya watu husema, “Nyaraka zake ni kali na zina nguvu, lakini kimwili yeye ni dhaifu. Maneno yake hayastahili kusikilizwa.”
11 Watu kama hao wajue ya kuwa, yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi, ndivyo tulivyo na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.
Hebu watu wa jinsi hiyo waelewe kwamba kile tusemacho kwa waraka wakati tukiwa mbali, ni sawasawa na vile tutakavyotenda wakati tukiwa pale.
12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara.
Hatuendi mbali mno kama kujikusanya wenyewe au kujilinganisha wenyewe na wale ambao hujisifia wenyewe. Lakini wanapojipima wenyewe na kila mmoja wao, hawana akili.
13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi.
Sisi, hata hivyo, hatutajivuna kupita mipaka. Badala yake, tutafanya hivyo tu ndani ya mipaka ambayo Mungu ametupimia sisi, mipaka inayofika umbali kama wenu ulivyo.
14 Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama vile ambavyo ingekuwa kama hatukuwa tumekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Kristo.
Kwa kuwa hatukujizidishia wenyewe tulipowafikia ninyi. Tulikuwa wa kwanza kufika kwa umbali kama wenu kwa injili ya Kristo.
15 Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi,
Hatujajivuna kupita mipaka kuhusu kazi za wengine. Badala yake, tunatumaini kama imani yenu ikuwavyo kwamba eneo letu la kazi litapanuliwa sana, na bado ni ndani ya mipaka sahihi.
16 ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine.
Tunatumaini kwa hili, ili kwamba tuweze kuhubiri injili hata kwenye mikoa zaidi yenu. Hatutajivuna kuhusu kazi inayofanywa katika maeneo mengine.
17 Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”
“Lakini yeyote ajivunaye, ajivune katika Bwana.”
18 Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Bwana humsifu.
Kwa maana siyo yule ajithibitishaye mwenyewe anathibitishwa. Isipokuwa, ni yule ambaye Bwana humthibitisha.

< 2 Wakorintho 10 >