< 2 Nyakati 24 >

1 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba.
Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala kwa mika arobaini katika Yerusalemu. Jina la mama yake aliitwa Sibia wa Beer-sheba.
2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ya Yehoyada kuhani.
Yoashi alifanya yaliyo mema katika macho ya Yahwe siku zote za Yehoyada, yule kuhani.
3 Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.
Yehoyada akajichukulia wake wawili kwa ajili yake, na akawa baba wa wana na mabinti.
4 Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Bwana.
Ikawa baada ya haya, kwamba Yoashi aliamua kuitengeneza nyumba ya Yahwe.
5 Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.
Akawakusanya pamoja makuhani na Walawi, na kusema kwao, “Nendeni nje kila mwaka kwenye miji ya Yuda na kukusanya fedha kutoka Israeli yote kwa ajili ya kuikarabati nyumba ya Mungu wenu. Hakikisheni kwamba mnaanza haraka.” Walawi hawakufanya kitu kwanza.
6 Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Mose mtumishi wa Bwana pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema ya Ushuhuda?”
Kwa hiyo mfalme akamuita Yehoyada, yule kuhani, na kumwambia, “Kwa nini hukuwaagiza Walawi kuleta kutoka Yud na Yerusalemu kodo iliyoagizwa na Musa mtumishi wa Yahwe na kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya amri za hema ya agano?”
7 Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Bwana kwa mabaali.
Kwa maana wana wa Athalia, yule mwanamke muovu, walikuwa wameivunja nyumba ya Mungu na kuwapa Mabaali vitu vyote vitakatifu vya nyumba ya Yahwe.
8 Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Bwana.
Kwa hiyo mfalme aliamuru, na wakatengeneza kasha na kulileta nje kwenye lango kwenye nyumba ya Yahwe.
9 Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu kwamba inapasa wamletee Bwana kodi ile ambayo Mose, mtumishi wa Bwana alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani.
Kisha wakafanya tangazo katika Yuda na Yerusalemu, kwa ajili ya watu kuleta kwa Yahwe kodi aliyoiagiza Musa mtumishi wa Mungu juu ya Israeli jangwani.
10 Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha mpaka likajaa.
Viongozi wote na watu wote wakafurahia na wakaleta fedha na kuiweka kwenye kasha hadi walipomaliza kulijaza.
11 Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana.
Ikatokea kwamba kila lilipoletwa kasha kwa mikono ya Walawi kwa wakuu wa mfalme, na kila walipoona kwamba kulikuwa na fedha nyingi sana ndani yake, waandishi wa mfalme na mkuu wa kuhani mkuu walikuja, kulihamishia fedha kasha, na kulirudisha sehemu yake. Walifanya hivyo siku baada siku, wakikusanya kiasi kikubwa cha fedha.
12 Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Bwana. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Bwana, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Bwana.
Mfalme na Yehoyada akawapa zile fedha wale waliofanya kazi ya kuhudumu katika nyumba ya Yahwe, Watu hawa waliwaajiri waashi na maseremala ili waijenge nyumba ya Yahwe, na pia wale waliofanya kazi katika chuma na shaba.
13 Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Bwana likarudi katika hali yake ya awali na kuliimarisha.
Kwa hiyo wafanya kazi wakafanya kazi, na kazi ya kukarabati ikasonga mbele mikononi mwao; waakaisimamisha nyumba ya Mungu katika hali yake halisi na kuiimarisha.
14 Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Bwana: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada alipokuwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Bwana.
Walipomaliza, wakaleta fedha zilizobaki kwa mfalme na Yehoyada. Fedha hizo zilitumika kutengenezea samani kwa ajili ya nyumba ya Yahwe, vyombo vya huduma na kutolea dhabihu—vijiko na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa bila kukomaa katika nyumba ya Yahwe kwa siku zote za Yehoyada.
15 Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku wakati alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka 130.
Yehoyada akazeeka na alaaikuwa amejaa siku, na kisha akafa; alikuwa na umri wa mika 130 alipokufa.
16 Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.
Wakamzika katika aamji wa Daudi miongoni mwa wafalme, kwa sababu alikuwa amefanya mema katika Israeli, kwa Mungu, na kwa ajili ya nyumba ya Mungu,
17 Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walikuja kumpa mfalme heshima, naye akawasikiliza.
Sasa baada ya kifo cha Yehoyada, kiongozi wa Yuda akaja na kutoa heshima kwa mfalme. Kisha mfalme akawasikiliza.
18 Wakaacha Hekalu la Bwana, Mungu wa baba zao, wakaabudu nguzo za maashera na sanamu. Kwa sababu ya hatia yao, hasira ya Mungu ikawajia Yuda na Yerusalemu.
Wakaiacha nyumba ya Yahwe, Mungu wa babu zao, na kuwaabudu miungu na maashera na sanamu. Ghadhabu ya Mungu ikaja juu ya Yuda na Yerusalemu kwa sababau ya hili kosa lao.
19 Ingawa Bwana aliwatuma manabii wawarudishe watu kwake na ingawa waliwaonya, hawakuwasikiliza.
Bado akatuma manabii kwao ili kuwaleta tena kwake, Yahwe, manabii wakatangaza juu ya watu, lakini walipuuza kusikiliza.
20 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Bwana? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.’”
Roho wa Mungu akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada, yule kuhani; Zekaria akasimama juu ya watu na kusema kwao, “Mungu anasema hivi: Kwa nini mnazivunja amri za Yahwe, ili kwamba msifanikiwe? Kwa kuwa mmemsahau Yahwe, pia amewasahau ninyi.”
21 Lakini wakafanya shauri baya juu yake na kwa amri ya mfalme wakampiga kwa mawe mpaka akafa katika ukumbi wa Hekalu la Bwana.
Lakini wakapanga njama dhidi yake; kwa amri ya mfalme, wakampiga kwa mawe katika uwanja wa nyumba ya Yahwe.
22 Mfalme Yoashi hakukumbuka wema aliotendewa na Yehoyada baba yake Zekaria ila alimuua mwanawe, ambaye alisema wakati akiwa amelala akingojea kufa, “Bwana na alione hili na alipize kisasi.”
Katika namna hii hii, Yoashi, yule mfalme, akapuuza ukarimu ambao Yehoyada, baba yake Zekaria, alikuwa amemfanyia.
23 Mwishoni mwa ule mwaka, jeshi la Waaramu likaja dhidi ya Yoashi, likavamia Yuda na Yerusalemu na kuwaua viongozi wote wa watu. Wakapeleka nyara zao zote kwa mfalme wao huko Dameski.
Ikawa karibu mwisho wa mwaka, kwamba jeshi la Aramu wakaja juu yake Yoashi. Wakaja Yuda na Yerusalemu; wakawaua viongozi wote wa watu na kupeleka nyara zote kutoka kwao kwa mfalme wa Dameski.
24 Ingawa jeshi la Waaramu lilikuwa limekuja na watu wachache tu, Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa kuliko lao. Kwa sababu Yuda walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, hukumu ilitekelezwa juu ya Yoashi.
Jeshsi la Waaramu walikuwa wamekuja na jeshi dogo, lakini Yahwe akawapa ushindi juu ya jeshi kubwa, kwa sababu Yuda alikuwa amemsahau Yahwe, Mungu wa babu zao. Katika namna hii Waaramu wakaleta hukumu juu ya Yoashi.
25 Waaramu walipoondoka, walimwacha Yoashi akiwa mgonjwa sana. Maafisa wake wakafanya hila dhidi yake kwa sababu alikuwa amemuua mwana wa Kuhani Yehoyada, nao wakamuulia kitandani mwake. Hivyo akafa na wakamzika katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
Katika muda ambao Waaramu walikuwa wameondoka, Yoashi alikuwa amejeruhiwa vikali. Watumishi wake wakapanga njama dhidi yake kwa sababu ya mauaji ya wana wa Yehoyada, yule kuhani. Wakamuua katika kitanda chake, na akafa; wakamzika katika mji wa Daudi, lakini siyo katika makaburi ya wafalme.
26 Wale waliofanya hila mbaya dhidi yake walikuwa Zabadi, mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, Yehozabadi, mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabu.
Hawa walikuwa watu waliopanaga njama dhidi yake: Zabadi mwana wa Shimeathi, Mwamoni; na Yehozabadi mwana wa Shimrithi, Mwanamke Mmoabu.
27 Kwa habari za wanawe, unabii mwingi kumhusu na kumbukumbu za kutengenezwa upya kwa Hekalu la Mungu, zimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme. Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
Sasa matukio kuhusu wanaye, unabii muhimu uliokuwa umesemwa kumhusu yeye, na kujengwa tena kwa nyumba ya Mungu, ona, yameandikwa katika Kamusi ya kitabu cha wafalme. Amazia mwanaye, akawa mfalme katika nafasi yake.

< 2 Nyakati 24 >