< 2 Nyakati 24 >
1 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba.
2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ya Yehoyada kuhani.
3 Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.
4 Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Bwana.
5 Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.
6 Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Mose mtumishi wa Bwana pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema ya Ushuhuda?”
7 Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Bwana kwa mabaali.
8 Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Bwana.
9 Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu kwamba inapasa wamletee Bwana kodi ile ambayo Mose, mtumishi wa Bwana alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani.
10 Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha mpaka likajaa.
11 Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana.
12 Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Bwana. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Bwana, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Bwana.
13 Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Bwana likarudi katika hali yake ya awali na kuliimarisha.
14 Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Bwana: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada alipokuwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Bwana.
15 Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku wakati alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka 130.
16 Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.
17 Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walikuja kumpa mfalme heshima, naye akawasikiliza.
18 Wakaacha Hekalu la Bwana, Mungu wa baba zao, wakaabudu nguzo za maashera na sanamu. Kwa sababu ya hatia yao, hasira ya Mungu ikawajia Yuda na Yerusalemu.
19 Ingawa Bwana aliwatuma manabii wawarudishe watu kwake na ingawa waliwaonya, hawakuwasikiliza.
20 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Bwana? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.’”
21 Lakini wakafanya shauri baya juu yake na kwa amri ya mfalme wakampiga kwa mawe mpaka akafa katika ukumbi wa Hekalu la Bwana.
22 Mfalme Yoashi hakukumbuka wema aliotendewa na Yehoyada baba yake Zekaria ila alimuua mwanawe, ambaye alisema wakati akiwa amelala akingojea kufa, “Bwana na alione hili na alipize kisasi.”
23 Mwishoni mwa ule mwaka, jeshi la Waaramu likaja dhidi ya Yoashi, likavamia Yuda na Yerusalemu na kuwaua viongozi wote wa watu. Wakapeleka nyara zao zote kwa mfalme wao huko Dameski.
24 Ingawa jeshi la Waaramu lilikuwa limekuja na watu wachache tu, Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa kuliko lao. Kwa sababu Yuda walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, hukumu ilitekelezwa juu ya Yoashi.
25 Waaramu walipoondoka, walimwacha Yoashi akiwa mgonjwa sana. Maafisa wake wakafanya hila dhidi yake kwa sababu alikuwa amemuua mwana wa Kuhani Yehoyada, nao wakamuulia kitandani mwake. Hivyo akafa na wakamzika katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
26 Wale waliofanya hila mbaya dhidi yake walikuwa Zabadi, mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, Yehozabadi, mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabu.
27 Kwa habari za wanawe, unabii mwingi kumhusu na kumbukumbu za kutengenezwa upya kwa Hekalu la Mungu, zimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme. Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.