< 2 Nyakati 19 >
1 Mfalme Yehoshafati wa Yuda akarudi salama kwenye jumba lake la kifalme huko Yerusalemu.
2 Yehu mwonaji, mwana wa Hanani, akapanda kwenda kuonana naye akamwambia Mfalme Yehoshafati, “Je, utawasaidia waovu na kuwapenda wale wanaomchukia Bwana? Kwa sababu ya jambo hili, ghadhabu ya Bwana iko juu yako.
3 Hata hivyo, kuna mema yaliyoonekana kwako, kwa kuwa umeondoa katika nchi nguzo za Ashera na umeukaza moyo wako katika kumtafuta Mungu.”
4 Yehoshafati aliishi huko Yerusalemu, naye akatoka akaenda tena miongoni mwa watu, kuanzia Beer-Sheba hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kuwageuza wakamrudia Bwana, Mungu wa baba zao.
5 Akawaweka waamuzi katika nchi, kwenye miji yote ya Yuda yenye maboma.
6 Akawaambia, “Angalieni kwa makini yale mtendayo, kwa kuwa hamkuhukumu kwa ajili ya mwanadamu bali kwa ajili ya Bwana ambaye yu pamoja nanyi kila mtoapo hukumu.
7 Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu. Hukumuni kwa uangalifu, kwa kuwa kwa Bwana Mungu wetu hakuna jambo lisilo la haki, upendeleo, wala rushwa.”
8 Pia huko Yerusalemu, Yehoshafati akaweka baadhi ya Walawi, makuhani na viongozi wa jamaa za Waisraeli ili kutoa hukumu kwa ajili ya Bwana na kuamua magomvi. Nao waliishi huko Yerusalemu.
9 Akawapa maagizo haya: “Ni lazima mtumike kwa uaminifu na kwa moyo wote katika kicho cha Bwana.
10 Katika kila shauri lifikalo mbele yenu kutoka kwa ndugu zenu wale waishio katika miji, ikiwa ni la umwagaji wa damu au mambo mengine yahusuyo sheria, amri, hukumu au maagizo, inawapasa ninyi kuwaonya kwamba wasiingie katika hatia dhidi ya Bwana, la sivyo ghadhabu yake itakuja juu yenu na ndugu zenu. Tendeni hivyo, nanyi hamtatenda dhambi.
11 “Amaria kuhani mkuu atakuwa juu yenu katika jambo lolote linalomhusu Bwana naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, kiongozi wa kabila la Yuda, atakuwa juu yenu kwa jambo lolote linalomhusu mfalme, nao Walawi watatumika kama maafisa mbele yenu. Tendeni kwa ujasiri, naye Bwana atakuwa pamoja na wale watendao vyema.”