< 1 Timotheo 5 >
1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako;
2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.
3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli.
4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu.
5 Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie.
6 Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi.
7 Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo yeyote wa kulaumiwa.
8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.
9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja,
10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.
11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena.
12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza.
13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema.
14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu.
15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.
16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.
17 Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha.
18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”
19 Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu.
20 Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa.
21 Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo.
22 Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.
23 Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.
24 Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni; na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao.
25 Vivyo hivyo, matendo mema yako dhahiri, na hata yale ambayo si mema hayawezi kufichika.