< 1 Timotheo 1 >

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na ya Kristo Yesu tumaini letu.
Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu,
2 Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani: Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo
Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao.
4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani.
Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani.
5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli.
Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli.
6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa,
Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana.
7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.
Wanapenda kuwa walimu wa Sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza.
8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa.
Twajua kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo.
9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji,
Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale;
10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli,
sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya kweli.
11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.
Mafundisho hayo hupatikana katika Habari Njema ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri, Habari Njema ya Mungu mtukufu na mwenye heri.
12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake.
Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie,
13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu.
ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya.
14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.
Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu.
15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote.
Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote,
16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. (aiōnios g166)
lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aonyeshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uzima wa milele. (aiōnios g166)
17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen. (aiōn g165)
Kwake yeye aliye Mfalme wa milele na asiyekufa, yeye aliye Mungu pekee—kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. (aiōn g165)
18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vita vizuri,
Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri,
19 ukiishikilia imani na dhamiri njema, ambazo wengine wamevikataa, na hivyo wakaangamia kwa habari ya imani yao.
na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao.
20 Miongoni mwao wako Himenayo na Aleksanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.
Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

< 1 Timotheo 1 >