< 1 Timotheo 1 >

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na ya Kristo Yesu tumaini letu.
Paulo, Mtume wa Kristo Yesu, kulingana na amri ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo aliye ujasiri wetu,
2 Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani: Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
kwa Timotheo mwanangu wa kweli katika imani: Neema, rehema na amani zitokazo kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo
Kama nilivyokusihi nilipoondoka kwenda Makedonia, ubaki Efeso ili kwamba uweze kuwaamru watu fulani wasifundishe mafundisho tofauti.
4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani.
Pia wasisikilize hadithi na orodha za nasaba zisizo na mwisho. Haya husababisha mabishano zaidi kuliko kuwasaidia kuendeleza mpango wa Mungu wa imani.
5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli.
Basi lengo la agizo hili ni upendo utokao katika moyo safi, katika dhamiri nzuri na katika imani ya kweli.
6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa,
Baadhi ya watu wamelikosa lengo wakayaacha mafundisho haya na kugeukia mazungumzo ya kipumbavu.
7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.
Wanataka kuwa waalimu wa sheria, lakini hawafahamu wanachosema au wanachosisitiza.
8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa.
lakini tunajua kwamba sheria ni njema kama mtu ataitumia kwa usahihi.
9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji,
Tunajua kuwa, sheria haikutungwa kwa ajili ya mtu mwenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, watu wasio wataua na wenye dhambi, na ambao hawana Mungu na waovu. Imetungwa kwa ajili ya wauao baba na mama zao, kwa ajili ya wauaji,
10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli,
kwa ajili ya waasherati, kwa ajili ya watu wazinzi, kwa ajili ya wale wanaoteka watu na kuwafanya watumwa, kwa ajili ya waongo, kwa ajili ya mashahidi wa uongo, na yeyote aliye kinyume na maelekezo ya uaminifu.
11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.
Malekezo haya yanatokana na injili yenye utukufu ya Mungu mwenye kubarakiwa ambayo kwayo nimeaminiwa.
12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake.
Ninamshukuru Yesu Kristo Bwana wetu. Alinitia nguvu, kwa kuwa alinihesabu mimi kuwa mwaminifu, na akaniweka katika huduma.
13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu.
Nilikuwa mtu wa kukufuru, mtesaji na mtu wa vurugu. Lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda kwa ujinga kwa kutoamini.
14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.
Lakini neema ya Mungu wetu imejaa imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.
15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote.
Ujumbe huu ni wa kuaminika na unastahili kupokelewa na wote, ya kuwa Kristo Yesu alikuja duniani kuokoa wenye dhambi. Mimi ni mbaya zaidi ya wote.
16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. (aiōnios g166)
Lakini kwa sababu hii mimi nilipewa rehema ili kwamba ndani yangu mimi, awali ya yote, Kristo Yesu adhihirishe uvumilivu wote. Alifanya hivyo kama kielelezo kwa wote watakaomtumaini Yeye kwa ajili ya uzima wa milele. (aiōnios g166)
17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen. (aiōn g165)
Na sasa kwa Mfalme asiye na ukomo, asiyekufa, asiyeonekana, Mungu pekee, iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina. (aiōn g165)
18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vita vizuri,
Ninaliweka agizo hili mbele yako Timotheo, mtoto wangu. Nafanya hivi kulingana na unabii uliotolewa hapo kwanza kukuhusu wewe, ili kwamba uhusike katika vita njema.
19 ukiishikilia imani na dhamiri njema, ambazo wengine wamevikataa, na hivyo wakaangamia kwa habari ya imani yao.
Fanya hivyo ili kwamba uwe na imani na dhamiri njema. Baadhi ya watu wameyakataa haya wakaangamiza imani.
20 Miongoni mwao wako Himenayo na Aleksanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.
Kama vile Himeneyo na Alekizanda ambao nimempa shetani ili wafundishwe wasikufuru.

< 1 Timotheo 1 >