< 1 Wathesalonike 5 >

1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia,
Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya.
2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku.
Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku.
3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.
Watu watakapokuwa wanasema: “Kila kitu ni shwari na salama” ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.
4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi.
Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.
5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku.
Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.
6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi.
Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.
7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku.
Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.
8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.
Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.
9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye.
ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa.
11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.
Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa.
12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya.
Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo.
13 Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi.
Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu.
14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote.
Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote.
15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.
Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote.
16 Furahini siku zote;
Furahini daima,
17 ombeni bila kukoma;
salini kila wakati
18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
19 Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu;
Msimpinge Roho Mtakatifu;
20 msiyadharau maneno ya unabii.
msidharau unabii.
21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema.
Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema,
22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.
na epukeni kila aina ya uovu.
23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo.
Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu—roho, mioyo na miili yenu—mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.
Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.
25 Ndugu, tuombeeni.
Ndugu, tuombeeni na sisi pia.
26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.
Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo.
27 Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.
Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii.
28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.
Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

< 1 Wathesalonike 5 >