< 1 Samweli 7 >
1 Kisha watu wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku la Bwana. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu juu kilimani na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku la Bwana.
2 Sanduku la Bwana lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, yaani jumla ya miaka ishirini, nao watu wa Israeli wakaomboleza na kumtafuta Bwana.
3 Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi na kujitoa wenyewe kwa Bwana na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi na mkono wa Wafilisti.”
4 Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi, nao wakamtumikia Bwana peke yake.
5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.”
6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Bwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa.
7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti.
8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.”
9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Akamlilia Bwana kwa niaba ya Israeli, naye Bwana akamjibu.
10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile Bwana alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli.
11 Watu wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.
12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri, akisema, “Hata sasa Bwana ametusaidia.”
13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena. Katika maisha yote ya Samweli, mkono wa Bwana ulikuwa dhidi ya Wafilisti.
14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ile ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawepo amani kati ya Israeli na Waamori.
15 Samweli akaendelea kama mwamuzi juu ya Israeli siku zote za maisha yake.
16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli mpaka Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote.
17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani kwake, huko pia aliwaamua Israeli. Naye huko alimjengea Bwana madhabahu.