< 1 Samweli 6 >

1 Sanduku la Bwana lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba,
Basi sanduku la BWANA lilikaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba.
2 Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Bwana? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.”
Ndipo Wafilisti wakawaita makuhani na waganga; wakawaambia, “Tulifanyie nini sanduku la BWANA? Twambieni jinsi ambavyo tunapaswa kulirudisha sanduku katika nchi yake.”
3 Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.”
Makuhani na waganga wakasema, “Kama mtalirudisha sanduku la Mungu wa Israeli, msilipeleke bila zawadi; kwa namna yoyote ile mpelekeeni sadakaa ya hatia. Hapo ndipo mtapona, na mtajua ni kwanini mkono wake hadi sasa haujaondoka juu yenu.”
4 Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?” Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni iyo hiyo imewaua ninyi na watawala wenu.
Ndipo wakawauliza, “Sadaka ya hatia itakuwa nini kwamba tunampelekea?” Wakawajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya watano wa dhahabu, Idadi hiyo ya watano ni sawa na idadi ya viongozi wa Wafilisti. Kwa sababu tauni ya aina moja iliwashambulia ninyi na viongozi wenu.
5 Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mheshimuni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu.
Kwa hiyo, nilazima mtengeneze mifano ya majipu yenu, na mifano ya panya wenu ambayo huiharibu nchi, na mpeni utukufu Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka juu yenu, kutoka juu ya miungu yenu, na kutoka juu ya nchi yenu.
6 Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao?
Kwanini mfanye mioyo yenu kwa migumu, kama vile Wamisri na Farao walifanya mioyo yao kuwa migumu? Hicho ni kipindi ambacho Mungu wa Israeli aliwashughilikia sana; Je, Wamisri hawakuwaachilia watu, na wakaondoka?
7 “Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ngʼombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ngʼombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini.
Basi sasa, andaeni mkokoteni mpya pamoja na ng'ombe wawili wake wanaonyonyesha, ambao hawajawahi kufungwa nira. Wafungeni ng'ombe hao kwenye mkokoteni, lakini warudisheni wale ndama wao nyumbani.
8 Chukueni hilo Sanduku la Bwana na mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekea Bwana kama sadaka ya hatia. Lipelekeni,
Kisha lichukueni sanduku la BWANA na kuliweka ndani ya mkokoteni. Wekeni ndani ya kasha yale maumbo ya dhahabu mnayompelekea ambyo ni sadaka ya hatia kando yake. Ndipo mlipeleke lipate kuondoka.
9 lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litakwenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwamba Bwana ndiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono wa Bwana uliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.”
Kisha muwe makini; kama litapanda kwenda kwa njia hadi nchini mwake hadi Beth Shemeshi, basi mjue kuwa BWANA ndiye aliyetenda pigo hili kubwa. Lakini kama halitakwenda, ndipo tutajua kwamba siyo mkono wake uliotupatia mateso; badala yake tutajua kuwa yaliyotupata ilikuwa ni kwa bahati mbaya tu.
10 Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini.
Watu hao wakafanya kama walivyoambiwa, walichukuwa ng'ombe wawili wanaonyonyesha, wakawafunga kwenye mkokoteni, na kuwabakiza ndama wao nyumbani.
11 Wakaliweka Sanduku la Bwana juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu.
Wakaliweka sanduku la BWANA juu ya mkokoteni, pamoja na lile kasha lililobeba panya wa dhahabu na yale maumbo ya majipu yao.
12 Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
Hao ng'ombe waliondoka moja kwa moja kuelekea Beth Shemeshi. Walikwenda kwa kuifuata nija moja kuu, wakiteremka walipokuwa wakienda, na hwakugeuka upande wa kushoto au kulia. Viongozi wa Wafilisti walifuata kwa nyuma hadi mpaka wa Beth Shemeshi.
13 Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.
Nao watu wa Beth Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao katika bonde. Waliponyanyua macho yao juu na kuliona sanduku, wakafurahi.
14 Lile gari la kukokotwa lilikuja mpaka kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ngʼombe kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
Huo mkokoteni ulifikia ndani ya shamba la Yoshua wa Beth Shemeshi na ukasimama hapo. Kulikuapo jiwe kubwa mahali hapo, wakatayarisha kuni kutokana na mkokoteni huo, na wakawatoa ng'ombe hao kama sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya BWANA.
15 Walawi walilishusha Sanduku la Bwana, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Bwana.
Walawi walilitelemsha sanduku la BWANA chini pamoja na kasha lake lililoyatunza yale maumbo ya dhahabu, wakaweka vitu hivyo juu ya hilo jiwe kubwa. Watu wa Beth Shemeshi walitoa sadaka za kuteketezwa na kutoa dhabihu kwa BWANA siku iyo hiyo.
16 Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi siku ile ile mpaka Ekroni.
Hao viongozi watano wa Wafilisti walipoona hayo, walirejea Ekroni siku iyo hiyo.
17 Haya ndiyo yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwa Bwana, moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.
Haya ndiyo majipu ya dhahabu ambayo Wafilisti walirudisha kama sadaka ya hatia kwa BWANA: moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.
18 Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao iliyozungukwa na maboma, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku la Bwana, ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi.
Idadi ya wale panya wa dhahabu ilikuwa sawa na ile ya idadi ya miji yote ya Wafilisti inayomilikiwa na viongozi watano, kwa miji iliyojengewa maboma na vijiji vya mashambani. Lile jiwe kubwa, ambalo kando yake waliweka sanduku la BWANA, lipo kama ushuhuda hadi leo katika shamba la Yoshua Mbeth- Shemeshi.
19 Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku la Bwana. Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwa Bwana,
BWANA akawashambulia baadhi ya watu wa Bethi Shemeshi kwa sababu walichungulia ndani ya sanduku lake. Aliwaua watu sabini. Watu wakaomboleza, kwa sababu BWANA aliwapa watu pigo kubwa mno.
20 nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele za Bwana, huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?”
Watu wa Bethi Shemeshi wakasema, “Ni nani mwenye uwezo wa kushindana na BWANA, huyu Mungu mtakatifu? Na atampandia nani akitoka kwetu.”” Je, ni nani awezaye kusimama mbele ya BWANA, huyu Mungu mtakatifu? Na ni kwa nani ambako sanduku litaenda likitoka hapa.”
21 Kisha wakatuma wajumbe kwa watu wa Kiriath-Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamerudisha Sanduku la Bwana. Shukeni na mlipandishe huko kwenu.”
Wakawatuma wajumbe kwenda kwa wenyeji wa Kiriath Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamelirudisha sanduku la BWANA; teremkeni na mkalipeleke kwenu.”

< 1 Samweli 6 >