< 1 Samweli 31 >

1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika Mlima Gilboa.
Basi Wafilisti wakapigana dhidi ya Waisraeli. Waisraeli wakakimbia mbele ya Wafilisti na wakaanguka chini wakafa katika mlima wa Gilboa.
2 Wafilisti wakawafuatia kwa bidii Sauli na wanawe, wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-Shua.
Wafilisti wakamwandama Sauli na wanawe kwa karibu. Wakawaua wanawe Yonathani, Abinadabu, and Malkishua.
3 Mapigano yakawa makali sana kumzunguka Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya.
Vita vikamwelemea Sauli, na wapiga upinde wakampata. Akapata maumivu makali kwa sababu yao.
4 Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja wanichome na kunidhalilisha.” Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia.
Kisha Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Chomoa upanga wako unichome nao. Vinginevyo, hawa wasiotahiriwa watakuja na kuninyanyasa.” Lakini mbeba silaha wake hakukubali, kwa kuwa aliogopa sana. Hivyo Sauli alichukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia.
5 Mchukua silaha wake alipoona Sauli amekufa, naye pia akaangukia upanga wake akafa pamoja naye.
Yule mbeba silaha akaona kwamba Sauli amekufa, yeye naye vivyo hivyo akauangukia upanga wake akafa pamoja naye.
6 Basi Sauli, wanawe watatu, mbeba silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile.
Kwa hiyo Sauli alikufa, wanawe watatu, na mbeba silaha wake - watu hawa wote walikufa pamoja siku iyo hiyo.
7 Waisraeli waliokuwa kandokando ya bonde na wale waliokuwa ngʼambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaja na kukaa humo.
Watu wa Israeli waliokuwa upande mwingine wa bonde, na hao waliokuwa ng'ambo ya Yordani, walipoona kwamba Waisraeli wamekimbia, na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, waliiacha miji yao na kukimbia, nao Wafilisti wakaja na kukaa humo.
8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka katika Mlima Gilboa.
IKawa katika siku iliyofuata, Wafilisti wakafika kuchukua nyara za waliokufa, ndipo wakamuona Sauli na wanawe watatu wameanguka juu ya mlima wa Gilboa.
9 Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao.
Nao wakakata kichwa chake na kuondoa silaha zake, na wakawatuma wajumbe kwenda pande zote katika nchi ya Wafilisti kutangaza habari hizo katika mahekalu yao ya sanamu na kwa watu.
10 Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani.
Wakaziweka silaha zake katika hekalu la Ashtorethi, nao wakakitundika kiwiliwili chake kwenye ukuta wa mji wa Bethi Shani.
11 Watu wa Yabeshi-Gileadi waliposikia yale Wafilisti walichomfanyia Sauli,
Na wenyeji wa Yabeshi Gileadi waliposikia kile Wafilisti walichomfanyia Sauli,
12 mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka kwenye ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, mahali ambapo waliiteketeza kwa moto.
wapiganaji wote wakainuka na kwenda usiku wote na wakauondoa mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Bethi Shani. Nao wakaenda Yabeshi na wakaichoma moto hiyo miili huko.
13 Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.
Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, na wakafunga siku saba.

< 1 Samweli 31 >