< 1 Samweli 29 >
1 Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.
Basi Wafilisti walikusanya pamoja majeshi yao yote huko Afeki; Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.
2 Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi.
Nao wakuu wa Wafilisti wakapitwa na mamia kwa maelfu; Daudi na watu wake wakapita wakiwa wa mwisho pamoja na Akishi.
3 Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?” Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lolote kwake.”
Kisha wakuu wa Wafilisti wakasema, “Hawa Waebrania wanafanya nini hapa?” Akishi akawaambia wakuu wengine wa Wafilisti, “Huyu si Daudi, mtumishi wa Sauli, mfalme wa Israeli, ambaye amekaa nami kwa siku hizi, au kwa miaka hii, nami nimeona hana kosa tangu aje kwangu hadi leo?”
4 Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe?
Lakini wale wakuu wa Wafilisti walimkasirikia Akishi; wakamwabia, Mfukuze mtu huyo, aende kwake kule ulikompatia; usimruhusu aende nasi vitani, ili asiwe adui yetu katika vita. Kwa jinsi gani mtu huyu angeweza kufanya amani na bwana wake? Siyo kwa gharama ya vichwa vya watu wetu?
5 Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema: “‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?”
Je, huyu siye Daudi ambaye walimuimba kwa kupokezana na kucheza, wakisema: 'Sauli ameua maelfu yake, Na Daudi makumi elfu yake?”'
6 Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Kama vile Bwana aishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lolote kwako, lakini hao watawala hawakukubali.
Ndipo Akishi alimwita Daudi na kumwambia, “Kama BWANA aishivyo, umekuwa mwema, na kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema kama nionavyo mimi; maana sijaona kosa kwako tangu siku unakuja kwangu hadi siku hii ya leo. Hata hivyo, wakuu hawakupendi.
7 Rudi na uende kwa amani; usifanye chochote cha kuwakasirisha watawala wa Kifilisti.”
Basi sasa rudi na uende kwa amani, ili usiwakwaze wakuu wa Wafilisti.”
8 Daudi akamuuliza Akishi, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”
Daudi akamwambia Akishi, “Lakini nimefanya nini? Kitu gani umekiona kwa mtumishi wako kwa muda ambao nimekuwa mbele yako hadi leo, kiasi kwamba nisiende kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”
9 Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’
Akishi akajibu na kumwambia Daudi, “Najua kwamba hauna lawama mbele zangu kama alivyo malaika wa Mungu; hata hivyo, wale wakuu wa Wafilisti wamesema, Kamwe hatapanda pamoja nasi hadi vitani.'
10 Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.”
Basi sasa amka asubuhi na mapema na watumishi wa bwana wako waliokuja pamoja nawe; mara tu muamkapo asubuhi na mapema na kupata mwanga, ondokeni.”
11 Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli.
Hivyo Daudi aliamka mapema, yeye pamoja na watu wake, waondoke asubuhi, warudi kule katika nchi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walipanda kwenda Yezreeli.