< 1 Samweli 26 >
1 Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?”
Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi akujificha katika vilima vya Hakila, ambavyo viko mbele ya jangwa?”
2 Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na watu wake 3,000 wa Israeli waliochaguliwa, kumsaka Daudi huko.
Kisha Sauli akaamka na kwenda chini ya jangwa la Zifu, akiwa na watu elfu tatu waliochaguliwa katika Israeli, wamtafute Daudi katika jangwa la Zifu.
3 Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko,
Sauli akaweka kambi kwenye kilima cha Hakila, kilicho mbele ya jangwa, kando ya barabara. Lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, na akaona kwamba Sauli alikuwa anamfuatia huko jangwani.
4 Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili.
Hivyo Daudi akawatuma wapelelezi na akafahamu kwamba hakika Sauli alikuwa amekuja.
5 Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka.
Daudi akaamka na kwenda hadi mahali ambapo Sauli alipiga kambi; akaona mahali alipolala Sauli, na Abneri mwana wa Neri, mkuu wa jeshi lake; Sauli alilala katikati ya kambi, na watu walipiga kambi kumzunguka, na wote wamesinzia.
6 Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” Abishai akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe.”
Ndipo Daudi akamwambia Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, “Ni nani atakwenda nami kambini kwa Sauli? Abishai akasema, “Mimi nitashuka pamoja nawe.”
7 Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.
Hivyo Daudi na Abishai wakaliendea jeshi usiku. Na Sauli alikuwapo akisinzia ndani ya kambi, mkuki wake umechomekwa chini pembeni mwa kichwa chake. Abneri na Askari wake wamelala kwa kumzunguka.
8 Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome mpaka ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”
Kisha Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemweka adui yako mkononi mwako. Basi tafadhali acha nimchome mkuki nimtoboe hadi chini kwa pigo moja. Sitampiga mara mbili.”
9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Bwana na asiwe na hatia?”
Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; kwa maana nani awezaye kunyoosha mkono wake dhidi ya mtiwa mafuta wa BWANA na asiwe na hatia?”
10 Daudi akasema, “Hakika kama vile Bwana aishivyo, Bwana mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au atakwenda vitani na kuangamia.
Daudi akasema, “Kama BWANA aishivyo, BWANA atamuua, au siku ya kufa kwake itakuja, au atakwenda katika vita na ataangamia.
11 Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa Bwana. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.”
BWANA apishe mbali nisinyooshe mkono wangu dhidi ya mtiwa mafuta wake; lakini sasa, nakusihi chukua mkuki uliokichwani pake na jagi la maji, tuondoke.”
12 Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu Bwana alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.
Hivyo Daudi akachukua mkuki na jagi la maji kutoka kichwani pa Daudi, wakatoweka. Hakuna mtu aliyewaona au kufahamu habari hii, wala hakuna aliyetoka usingizini, maana wote walisinzia, kwa sababu usingizi mzito kutoka kwa BWANA uliwaangukia.
13 Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao.
Kisha Daudi akaenda upande mwingine na akasimama juu ya mlima mbali sana; ukiwepo umbali mkubwa katikati yao.
14 Daudi akalipigia kelele jeshi na Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?” Abneri akajibu, “Nani wewe umwitaye mfalme?”
Daudi akawapigia kelele watu hao na Abneri mwana Neri; akisema, “Hujibu neno, Abneri?” Ndipo Abneri akajibu na kusema, “Wewe ni nani unayempigia mfalme kelele?”
15 Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako.
Daudi akamwambia Abneri, “Wewe siye mtu jasiri? Ni nani yuko kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukukaa macho kumlinda bwana wako mfalme? Kwa maana mtu fulani aliingia kumuua mfalme, bwana wako.
16 Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama aishivyo Bwana, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa Bwana. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?”
Jambo hili ulilolifanya siyo zuri. Kama BWANA aishivyo, unapaswa kufa kwa sababu hukumlinda bwana wako, mtiwa mafuta wa BWANA. Na sasa tazama ulipo mkuki wa mfalme, na jagi la maji lililokuwa kichwani pake.”
17 Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.”
Sauli aliitambua sauti ya Daudi akasema, “Hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akasema, “Ni sauti yangu, mfalme, bwana wangu.”
18 Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia?
Daudi akasema, “Kwa nini bwana wangu anamwandama mtumishi wake? Nimefanya nini? Mkononi mwangu kuna uovu gani?
19 Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama Bwana amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini hata hivyo, kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za Bwana! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa Bwana wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’
Kwa hiyo sasa, nakusihi, bwana wangu mfalme asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama ni BWANA ndiye amekuchochea dhidi yangu, na aikubali sadaka; lakini kama ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA, maana leo wamenifukuza, nisishikamane na urithi wa BWANA; wameniambia, 'Nenda ukaabudu miungu mingine.'
20 Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa Bwana. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.”
Kwa hiyo, sasa, usiiachilie damu yangu ianguke ardhini mbali na uwepo wa BWANA; kwa kuwa mfalme wa Israeli ametoka nje kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware milimani.”
21 Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”
Kisha Sauli akasema, “Nimefanya dhambi. Rudi, Mwanangu, Daudi; maana sitakudhuru tena, kwa sababu leo maisha yangu yalikuwa yenye thamani machoni pako. Tazama, nimetenda upumbavu na nimekosa sana.”
22 Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua.
Daudi akajibu na akasema, “Tazama, mkuki wako uko hapa, mfalme! Mruhusu kijana mmojawapo aje auchukue na aulete kwako.
23 Bwana humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. Bwana alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa Bwana.
Na BWANA amlipe kila mtu kwa ajili ya uadilifu wake na kwa uaminifu wake; kwa sababu leo BWANA alikuweka mkononi mwangu, lakini nisinge mpiga mtiwa mafuta wake.
24 Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa Bwana na kuniokoa kutoka taabu zote.”
Na tazama, kama maisha yako leo yalivyokuwa ya thamani machoni pangu, vivyo hivyo maisha yangu yathaminiwe sana machoni pa BWANA, na aweze kuniokoa katika shida zote.”
25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.” Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani.
Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Na ubarikiwe, mwanangu Daudi, ili uweze kutenda mambo makuu, na hakika uweze kufanikiwa.” Ndipo Daudi akaenda zake, na Sauli akarudi kwake.