< 1 Samweli 25 >

1 Basi Samweli akafa, nao Israeli wote wakakusanyika na kumwombolezea; wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akateremka kwenye Jangwa la Maoni.
Basi Samweli akafariki. Waisraeli wote wakakusanyika pamoja na kumwomboleza, na wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akainuka na akashuka hadi jangwa la Parani.
2 Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli.
Kulikuwa na mtu mmoja huko Maoni, na mali zake zilikuwa huko Karmali. Mtu huyo alikuwa tajiri sana. Alikuwa na kondoo elfu tatu na mbuzi elfu moja. Naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake huko Karmeli.
3 Jina la mtu huyo lilikuwa Nabali, naye mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe, ambaye alikuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake.
Na mtu huyo aliitwa Nabali, na jina la mke wake aliitwa Abigaili. Mwanamke huyo alikuwa mwenye busara na mzuri kwa sura. Lakini mwanaume alikwa mkaidi na mwovu katika mambo yake. Alikuwa wa uzao wa nyumba ya Kalebu.
4 Daudi alipokuwa huko jangwani, akasikia kuwa Nabali alikuwa anakata kondoo manyoya.
Daudi akasikia akiwa jangwani kwamba Nabali alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake.
5 Basi akatuma vijana kumi na kuwaambia, “Pandeni kwa Nabali huko Karmeli, mkamsalimie kwa jina langu.
Hivyo Daudi aliwatuma kwake vijana kumi. Akawaambia wale vijana, “Pandeni kwanda Karmeli, mwendeeni Nabali, na mkamsalimie kwa jina langu.
6 Mwambieni: ‘Amani iwe kwako! Amani iwe kwako pamoja na wa nyumbani mwako! Pia amani iwe pamoja na vyote ulivyo navyo!
Mtamwambia, 'Uishi katika baraka, Uwe na amani na nyumba yako iwe na amani, na wote ulionao wawe na amani.
7 “‘Nasikia kuwa huu ni wakati wa kukata kondoo manyoya. Wachunga mifugo wako walipokuwa pamoja nasi, hatukuwatendea mabaya na wakati wote waliokuwa huko Karmeli hakuna chochote chao kilipotea.
Nasikia kwamba unao wakata manyoya. Wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, na hatukuwafanyia ubaya, na muda wote wakiwa Karmeli hawakupotelewa kitu chochote.
8 Waulize watumishi wako nao watakuambia. Kwa hiyo uwatendee wema vijana wangu, kwani tumekuja wakati wa furaha. Tafadhali wape watumishi wako na mwanao Daudi chochote kitakachokuja mkononi mwako kwa ajili yao.’”
Waulize vijana wako, nao watakuambia. Basi vijana wangu wapate kibali machoni pako, maana tumefika siku ya sherehe. Tafadhali utoe cho chote ulicho nacho mkononi kwa watumishi wako na kwa Daudi mwanao.'”
9 Watu wa Daudi walipofika wakampa Nabali ujumbe huu kwa jina la Daudi. Kisha wakangojea.
Vijana wa Daudi walipofika, walimwambia Nabali yote haya kwa niaba ya Daudi na kisha wakasubiri.
10 Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Huyu Daudi ni nani? Huyu mwana wa Yese ni nani? Watumishi wengi wanakimbia kutoka kwa bwana zao siku hizi.
Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Na ni nani mwana wa Yese? Siku hizi wapo watumishi wengi wanaotoroka bwana zao.
11 Kwa nini nichukue mkate wangu, maji yangu na nyama niliyochinja kwa ajili ya wakata manyoya wangu, na kuwapa watu ambao hakuna anayejua wanakotoka?”
Je, nichukue mkate wangu na maji yangu na nyama yangu ambayo nimewachinjia wakata manyoya wangu, na niwape watu wanaotoka nisikokujua?”
12 Watu wa Daudi wakageuka na kurudi. Walipofika, wakaarifu kila neno.
Hivyo vijana wa Daudi waligeuka na kurudi, nakumwambia kila kitu kilichosemwa.
13 Daudi akawaambia watu wake, “Jifungeni panga zenu!” Basi wakajifunga panga zao, naye Daudi akajifunga upanga wake. Watu kama mia nne hivi wakapanda pamoja na Daudi, na watu mia mbili wakabaki na vifaa.
Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu ajifunge upanga wake.” Kila mtu akajifunga upanga wake. Daudi naye pia akajifunga upanga wake. Yapata kama watu mia nne wakafuatana na Daudi, na wengine mia mbili walibaki kulinda mizigo yao.
14 Mmoja wa watumishi akamwambia Abigaili, mkewe Nabali: “Daudi alituma wajumbe kutoka jangwani kumpa bwana wetu salamu zake, lakini akawavurumishia matukano.
Lakini kijana mmojawapo alimwambia Abigaili, mke wa Nabali akasema, “Daudi aliwatuma wajumbe kutoka jangwani waje wamsalimu bwana wetu, na yeye akawatukana.
15 Hata hivyo watu hawa walikuwa wema sana kwetu. Hawakututendea mabaya, na wakati wote tulipokuwa nje huko mashambani karibu nao, hatukupotewa na kitu chochote.
Bado watu hawa walitutendea mema. Hatukudhurika na hatukupoteza chochote wakati wote tulipotembea nao tulipokuwa mbugani.
16 Usiku na mchana walikuwa ukuta wakituzunguka wakati wote tulipokuwa tukichunga kondoo zetu karibu nao.
Walikuwa ukuta wetu usiku na mchana, wakati wote tulikuwa pamoja nao tukichunga kondoo.
17 Sasa fikiri juu ya jambo hili na uone unaweza kufanya nini, kwa sababu maafa yanakaribia juu ya bwana wetu na nyumba yake yote. Yeye ni mtu mwovu kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kuzungumza naye.”
Kwa hiyo tambua hili na zingatia utafanya nini, maana ubaya unamvizia bwana wetu, na utakuwa juu ya nyumba yake yote. Yeye ni mtu asiyefaa na hakuna awezaye kushauriana naye.”
18 Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda.
Ndipo Abigaili akaharakisha na akachukuwa mikate mia mbili, chupa mbili za divai, kondoo watano waliokwisha andaliwa, vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu, na mikate mia mbili ya tini na akavipakia juu ya punda.
19 Kisha akawaambia watumishi wake, “Tangulieni; mimi nitakuja nyuma yenu.” Lakini hakumwambia Nabali mumewe.
Akamwambia kijana wake, “Tangulia mbele yangu, nami nitakuja nyuma yako.” Lakini hakumwambia mmewe Nabali.
20 Ikawa alipokuwa amepanda punda wake kwenye bonde la mlima, tazama, Daudi na watu wake wakawa wanateremka kumwelekea, naye akakutana nao.
Alipokuwa akienda juu ya punda wake na kutelemka penye kificho cha mlima, Daudi na watu wake walishuka chini wakimwelekea Abigaili, naye akakutana nao.
21 Daudi alikuwa amesema, “Ilikuwa ni kazi bure kuchunga kwangu kote mali za huyu mtu huko jangwani hivi kwamba hakuna chochote chake kilichopotea. Yeye amenilipa baya kwa ajili ya wema.
Basi Daudi alikuwa amesema, “Hakika nimelinda bure vyote alivyonavyo mtu huyu huko nyikani, na vyote alivyonavyo hakuna kilichopotea, pamoja na hayo amenilipa mabaya badala ya mema.
22 Bwana na amshughulikie Daudi, tena kwa ukali, ikiwa kesho asubuhi nitambakizia mwanaume hata mmoja aliye hai miongoni mwa watu wake wote!”
Mungu na anitendee hivyo mimi, Daudi, pia iwe zaidi, iwapo nitamwacha hata mtu mmoja wa kwake akiwa hai ifikapo kesho asubuhi.
23 Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akainama kifudifudi uso wake mpaka nchi mbele ya Daudi.
Abigaili alipomwona Daudi, aliharakisha na kushuka chini ya punda wake, akalala kifudifudi na kujiinamisha hadi chini.
24 Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema.
Akamwangukia miguuni pake na kusema, “Juu yangu tu, bwana wangu, na uwe uovu. Tafadhali acha mjakazi wako aseme nawe, tena uyasikilize maneno ya mjakazi wako.
25 Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu.
Nakusihi bwana wangu usimjali mtu huyu asiyefaa, Nabali, kwa maana kama jina lake lilivyo, ndivyo alivyo. Jina lake ni Nabali, na upumbavu uko pamoja naye. Lakini mimi mjakazi wako sikuwaona vijana wa bwana wangu, uliowatuma.
26 “Basi sasa, kwa kuwa Bwana amekuzuia, wewe bwana wangu, kutokumwaga damu na kutolipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama Bwana aishivyo na kama uishivyo, maadui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali.
Sasa basi, bwana wangu, kama BWANA aishivyo, na kama unavyoishi, kwa kuwa BWANA amekuondoa kutoka kumwaga damu, na kuacha kulipiza kisasi kwa mkono mwenyewe, basi adui zako, na wale ambao wanatafuta kumfanyia uovu bwana wangu, wawe kama Nabali
27 Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe.
Na sasa zawadi hii ambayo mjakazi wako ameileta kwa bwana wangu, na wapewe vijana ambao wanamfuata bwana wangu.
28 Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa Bwana kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya Bwana.
Tafadhali ulisamehe kosa la mjakazi wako, maana BWANA hakika atamfanyia bwana wangu nyumba imara, kwa sababu bwana wangu anapigana vita vya BWANA; na uovu hautaonekana ndani yako maadamu unaishi.
29 Hata ingawa yuko mtu anayekufuatia kuuondoa uhai wako, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na Bwana Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako atavurumishwa kama vile jiwe kutoka kwenye kombeo.
Na ingawa watu wangeinuka na kukuandama ili wakuue, bado uhai wa bwana wangu utafungwa katika furushi la walio hai na BWANA Mungu wako; na atayatupa maisha ya adui zako mbali, kama vile kutoka katika mfuko wa kombeo.
30 Bwana atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu yeye na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli,
Na itakuwa, BWANA atakapokuwa amemtimizia bwana wangu mambo yote mazuri ambayo amekuahidi, na alivyokufanya kiongozi juu ya Israeli,
31 bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. Bwana atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.”
jambo hili halitakuwa huzuni kwako, wala chukizo moyoni kwa bwana wangu, kwa sababu hukumwaga damu bila sababu, na hujajilipizia kisasi. Na BWANA akikuletea mafanikio, umkumbuke mjakazi wako.”
32 Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli aliyekutuma kunilaki leo.
Ndipo Daudi akamwambia Abigaili, “BWANA, Mungu wa Israeli, abarikiwe, aliyekutuma uonane na mimi leo.
33 Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu.
Na hekima yako ibarikiwe, nawe umebarikiwa, kwa sababu leo umenizuia nisiwe na hatia ya kumwaga damu, na kutojilipizia kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.
34 La sivyo, hakika kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna hata mwanaume mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.”
Kwa kweli, kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisikuumize, kama usinge harakisha kuja ukutane nami, kwa hakika kesho asubuhi asinge salia hata mtoto mmoja wa kiume kwa Nabali.”
35 Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani kwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.”
Kwa hiyo Daudi akavipokea kutoka mkononi mwake vile alivyokuwa amemletea; akamwambia, “Nenda kwa amani hadi nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako na nimekubali.”
36 Abigaili alipokwenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote mpaka asubuhi yake.
Abigaili akarudi kwa Nabali; tazama, alikuwa akifanya sherehe katika mji wake, kama sherehe ya mfalme; na moyo wa Nabali ulifurahi ndani yake, kwa sababu alikwa amelewa sana. Kwa hiyo hakumwambia chochote kabisa hadi kulipopambazuka
37 Basi asubuhi, Nabali alipokuwa amelevuka, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe.
Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, basi mkewe akamwambia mambo hayo; moyo wake ukafa ndani yake, na akawa kama jiwe.
38 Baada ya siku kumi, Bwana akampiga Nabali, naye akafa.
Ikawa baada ya siku kumi BWANA alimpiga Nabali naye akafa.
39 Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe Bwana, ambaye amenitetea shauri langu dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na Bwana ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake.
Naye Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “BWANA abarikiwe, aliyenichukulia hatua ya shutuma yangu kutoka mkono wa Nabali, na kumzuia mtumishi wake asifanye maovu. Na amemrudishia Nabali tendo la uovu juu ya kichwa chake mwenyewe.” Ndipo Daudi akawatuma watu wakaongee na Abigaili, ili amchukue awe mke wake.
40 Watumishi wa Daudi wakaenda mpaka Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.”
Watumishi wake Daudi walipofika kwa Abigaili huko Karmeli, wakaongea naye na kusema, “Daudi ametutuma kwako tukuchukue hadi kwake uwe mke wake.”
41 Akainama chini uso wake mpaka ardhini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.”
Abigaili aliinuka, akainamisha uso chini, na akasema, “Tazama, mjakazi wako ni mtumwa aoshaye miguu ya watumishi wa bwana wangu.”
42 Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe.
Akaharakisha na kuamka, akapanda punda akiwa na vijakazi wake watano waliofuatana naye; akawafuata wajumbe wa Daudi, na akawa mke wake.
43 Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake.
Daudi pia alimchukua Ahinoamu wa Yezreeli akamwoa; wote wawili wakawa wake zake.
44 Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu.
Wakati huo Sauli alikuwa amempa Palti, mwana wa Laishi mtu wa Galimu, Mikali, binti yake, aliyekuwa mke wa Daudi.

< 1 Samweli 25 >