< 1 Samweli 22 >
1 Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
2 Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao 400 walikuwa pamoja naye.
3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa huko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe mpaka nijue nini Mungu atakachonifanyia.”
4 Hivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni.
5 Ndipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi.
6 Basi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka.
7 Sauli akawaambia, “Sikilizeni enyi watu wa Benyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia?
8 Je, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.”
9 Lakini Doegi Mwedomu, ambaye alikuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu.
10 Ahimeleki akamuuliza Bwana kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.”
11 Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme.
12 Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.” Akajibu, “Naam, bwana wangu.”
13 Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga shauri baya dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena hukumuuliza Mungu kwa ajili yake, na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?”
14 Ahimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako?
15 Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.”
16 Lakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”
17 Ndipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa Bwana, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.” Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa Bwana.
18 Kisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano wavaao visibau vya kitani.
19 Pia akaupiga Nobu kwa upanga, mji wa makuhani, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto wadogo na wale wanyonyao, ngʼombe wake, punda na kondoo.
20 Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi.
21 Akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Bwana.
22 Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile, wakati Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli. Mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa ya baba yako yote.
23 Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”