< 1 Samweli 21 >

1 Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?”
Kisha Daudi akafika Nobu kumuona Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akaja akutane na Daudi huku akitetemeka na kumwambia, “Kwa nini uko peke yako huna mtu wa kuambatana na wewe?”
2 Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi yako wala maagizo yako!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia tukutane mahali fulani.
Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, “Mfalme amenituma kwa jambo maalum na ameniambia hivi, 'Asiwepo hata mtu mmoja anayejua chochote kuhusu shughuli niliyokutuma, na kile nilichokuagiza.' Nimewaelekeza vijana kwenda sehemu fulani.
3 Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.”
Sasa basi chakula gani kinapatikana hapa? Nipatie mikate mitano, au chochote kilichopo hapa.”
4 Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.”
Huyo Kuhani alimjibu Daudi na kusema, “Hakuna mkate wa kawaida mkononi, lakini ipo mikate takatifu- kama vijana hawajatembea na wanawake.”
5 Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?”
Daudi akamjibu kuhani, “Hakika hatujatembea na wanawake kwa siku hizi tatu. Nilipoanza safari, miili ya vijana iliwekwa wakfu kwa BWANA, ingawa ilikuwa safari ya kawaida. Je, si zaidi sana leo miili yao ikawekwa wakfu kwa BWANA.”
6 Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwepo mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonyesho iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Bwana na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa.
Hivyo kuhani akampa mikate iliyokuwa imewekwa wakfu kwa BWANA. Maana haikuwepo mikate mingine hapo, isipokuwa tu ile ya wonyesho, ambayo iliondolewa kutoka kwa BWANA, ili sehemu yake iwekwe mikate ya moto, inapokuwa imeondolewa.
7 Basi siku hiyo palikuwepo na mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Bwana; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachunga wanyama wa Sauli.
Basi siku hiyo mmoja wa watumishi wa Sauli alikuwapo mahali hapo, ameshilkiliwa mbele za BWANA. Jina la mtu huyo aliitwa Doegi Mwedomu, mkuu wa wachungaji wa Sauli.
8 Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.”
Daudi akamwambia Ahimeleki, “Je, hakuna hata mkuki wowote au upanga? Maana mimi sikubeba upanga wangu wala silaha zangu, maana ile shughuli ya mfalme ilikuwa ya muhimu.”
9 Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungiwa katika kitambaa nyuma ya kisibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.”
Kuhani akasema, “Ule upanga wa Mfilisti Goliathi, uliyemuua katika bonde la Ela, uko hapa umefunikwa katika nguo nyuma ya naivera. kama unataka kuuchukua huo, uchukue, maana hakuna silaha nyingine hapa.” Daudi akasema, “Hakuna silaha nyingine kama hiyo, nipatie hiyo.”
10 Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi.
Daudi aliamka na kukimbia mbali na Sauli na akaenda kwa Akishi, mfalme wa Gathi.
11 Lakini watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema: “‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?”
Mtumishi wa Akishi akamwambia, “huyu siye Daudi mfalme wa nchi hii? Je, wanawake hawakupokezana wakiimba na kucheza, 'Sauli ameua maelfu yake, na Daudi makumi elfu yake?”'
12 Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi.
Daudi akayaweka maneno hayo moyoni mwake na akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi.
13 Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango na kuachia udelele kutiririka kwenye ndevu zake.
Daudi akabadili mwenendo wake mbele yao na akajifanya kuwa mwendawazimu machoni pao; akachora-chora alama kwenye vizingiti vya milango huku akitiririsha mate yake chini ya ndevu zake.
14 Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu?
Ndipo Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni, mnaona mtu huyu ni mwehu.
15 Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani kwangu?”
Kwa nini mmemleta kwangu? Je, mimi nina haja na wehu, kumbe mmemleta mtu huyu ili anifanyie hayo mbele yangu? Hivi kweli huyu ataingia nyumbani mwangu?

< 1 Samweli 21 >