< 1 Samweli 21 >
1 Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?”
2 Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi yako wala maagizo yako!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia tukutane mahali fulani.
3 Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.”
4 Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.”
5 Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?”
6 Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwepo mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonyesho iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Bwana na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa.
7 Basi siku hiyo palikuwepo na mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Bwana; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachunga wanyama wa Sauli.
8 Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.”
9 Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungiwa katika kitambaa nyuma ya kisibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.”
10 Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi.
11 Lakini watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema: “‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?”
12 Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi.
13 Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango na kuachia udelele kutiririka kwenye ndevu zake.
14 Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu?
15 Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani kwangu?”