< 1 Samweli 19 >

1 Sauli akamwambia mwanawe Yonathani na watumishi wake wote wamuue Daudi. Lakini Yonathani mwana wa Sauli alimpenda sana Daudi.
Sauli akamwambia Yonathani mwanawe na watumishi wake wote kwamba wanapaswa kumuua Daudi. Lakini Yonathani, mwana wa Sauli, alitamani sana akae na Daudi.
2 Yonathani akamwonya Daudi, akisema, “Baba yangu Sauli anatafuta nafasi ya kukuua. Ujilinde kesho asubuhi, nenda mahali pa siri na ukae huko.
Hivyo Yonathani akamwambia Daudi, “Baba yangu Sauli anatafuta kukuua. Kwa hiyo uwe macho wakati wa asubuhi na jifiche mahali pa siri.
3 Nitatoka na kukaa na baba yangu shambani mahali uliko. Nitazungumza naye juu yako, nami nitakueleza nitakachogundua.”
Nami nitatoka nje na kusimama kando ya baba yangu huko shambani uliko wewe, na nitazungumza na baba yangu kuhusu wewe. Kama nikijua jambo lolote nitakuambia.”
4 Yonathani akanena mema juu ya Daudi kwa Sauli baba yake na kumwambia, “Mfalme asitende mabaya kwa mtumishi wake Daudi; hajakukosea, aliyoyafanya yamekuwa ya faida sana kwako.
Yonathani alimsifia Daudi mbele ya Sauli baba yake akisema, “Mfalme asije akafanya dhambi dhidi ya mtumishi wake Daudi. Maana yeye hajakutenda dhambi, mambo aliyofanya yamekusaidia sana.
5 Alihatarisha maisha yake alipomuua yule Mfilisti. Bwana akajipatia ushindi mkubwa kwa ajili ya Israeli wote, nawe uliuona na ukafurahi. Kwa nini basi utende mabaya kwa mtu asiye na hatia kama Daudi kwa kumuua bila sababu?”
Maana alijitoa maisha yake na kumuua yule Mfilisti, naye BWANA akawaletea Waisraeli wote wokovu mkuu. Tena uliuona na kufurahi. Kwa nini utende dhambi juu damu isiyo na hatia kwa kumuua Daudi bila sababu?”
6 Sauli akamsikiliza Yonathani na kuapa hivi: “Hakika kama Bwana aishivyo, Daudi hatauawa.”
Sauli alimsikiliza Yonathani. Sauli akaapa, “Kama BWANA aishivyo, Yonathani hatauawa.”
7 Basi Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mazungumzo yote. Akamleta kwa Sauli, naye Daudi akawa pamoja na Sauli kama kwanza.
Ndipo Yonathani akamwita Daudi na kumwambia mambo hayo yote. Na Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye Daudi akawa mbele zake kama zamani.
8 Vita vilitokea tena, naye Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti. Akawapiga kwa nguvu nyingi hata wakakimbia mbele yake.
Baadaye kukawa na vita tena. Daudi akatoka na kupigana na Wafilisti na kuwashinda kwa mauaji makubwa mno. Nao wakakimbia mbele yake.
9 Lakini roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Bwana ikaja juu ya Sauli alipokuwa ameketi katika nyumba yake akiwa na mkuki mkononi mwake. Daudi alipokuwa anampigia kinubi,
Yule roho wa ubaya kutoka kwa BWANA ikamjia Sauli alipokuwa ameketi nyumbani mwake na mkuki mkononi mwake, na Daudi akiwa anapiga chombo chake.
10 Sauli akajaribu kumchomea Daudi ukutani kwa huo mkuki wake, lakini Daudi akauhepa huo mkuki wa Sauli ukakita ukutani. Usiku ule ule Daudi akakimbia na kuokoka.
Sauli alijaribu kumpigilia Daudi ukutani kwa mkuki wake, lakini akaponyoka kutoka machoni pake, na kwamba Sauli akashindilia mkuki ndani ya ukuta. Daudi alikimbia na kutoroka usiku huo.
11 Sauli akatuma watu nyumbani mwa Daudi wailinde hiyo nyumba na kumuua asubuhi. Lakini Mikali, mkewe Daudi, akamwonya akisema, “Kama hukukimbia kuokoa maisha yako usiku huu, kesho yake utauawa.”
Bado Sauli aliwatuma wajumbe nyumbani kwa Daudi wamvizie kusudi aweze kumuua asubuhi. Mkewe Daudi, Mikali, akamwambia, “Usipoyaokoa maisha yako usiku huu, kesho utauwawa.”
12 Basi Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akakimbia na kuokoka.
Hivyo Mikali akamteremsha Daudi kupita dirishani. Naye akaenda, akakimbia na kutoroka.
13 Kisha Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani, akakifunika kwa vazi na kukiwekea singa za mbuzi kichwani.
Mikali alichukua kinyago na kukilaza juu ya kitanda. Kisha akaweka mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na akakifunika na nguo.
14 Sauli alipotuma watu kumkamata Daudi, Mikali akasema, “Yeye ni mgonjwa.”
Sauli alipowatuma wajumbe kumchukua Daudi, mkewe akasema, “Daudi ni mgonjwa.”
15 Kisha Sauli akatuma watu tena kumwona Daudi naye akawaambia, “Mleteni kwangu juu ya kitanda chake ili nipate kumuua.”
Kisha Sauli akawatuma wajumbe kumtazama; akisema, “Mleteni kwangu akiwa kitandani, ili nimuue.”
16 Lakini wale watu walipoingia, kumbe ni kinyago tu kilichokuwa kitandani na kwenye kichwa kulikuwepo na singa za mbuzi.
Wale wajumbe walipoingia ndani, tazama, kile kinyago kilikuwa kitandani pamoja na mto wa singa za mbuzi kichwani.
17 Sauli akamwambia Mikali, “Kwa nini umenidanganya mimi hivi na kumwacha adui yangu aende zake ili apate kuokoka?” Mikali akamwambia, “Yeye aliniambia, ‘Niache niende zangu. Kwa nini nikuue?’”
Sauli akamuuliza Mikali, “Kwa nini umenidanganya na kumwachilia adui yangu aende, na tena ametoroka?” Mikali akamjibu Sauli, “Aliniambia, 'Acha niende. Kwa nini nikuuwe?”'
18 Daudi alipokuwa amekimbia na kuokoka, alimwendea Samweli huko Rama na kumwambia yale yote Sauli alimfanyia. Ndipo Daudi na Samweli wakaenda Nayothi kukaa huko.
Basi Daudi akakimbia na kutoroka, na akaenda kwa Samweli huko Rama na kumweleza yote ambayo Sauli amemtendea. Ndipo yeye na Samweli wakaenda na kukaa Nayothi.
19 Habari zikamfikia Sauli kusema: “Daudi yuko Nayothi huko Rama.”
Naye Sauli akaambiwa kwamba, “Tazama, Daudi yuko huko Nayothi iliyoko Rama.”
20 Basi Sauli akatuma watu kumkamata Daudi, lakini walipoona kundi la manabii wakitoa unabii, wakiwa pamoja na Samweli akiwa amesimama hapo kama kiongozi wao, Roho wa Mungu akaja juu ya watu wa Sauli, nao pia wakatoa unabii.
Kisha Sauli akawatuma wajumbe kumkamata Daudi. Nao walipowaona kundi la manabii wakitabiri, na Samweli akisimama kama kiongozi wao, Roho wa Mungu akawaingia wale wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri.
21 Sauli akaelezwa juu ya hilo, naye akapeleka watu wengine zaidi, nao wakatoa unabii pia. Sauli akatuma watu mara ya tatu, nao pia wakatoa unabii.
Sauli alipoambiwa hivyo, akawatuma wajumbe wengine, nao pia wakatabiri. Basi Sauli aliwatuma tena wajumbe kwa mara ya tatu, na hao pia wakatabiri.
22 Mwishowe, yeye mwenyewe akaondoka kwenda Rama na kwenda hadi kwenye kile kisima kikubwa kilichoko huko Seku. Naye akauliza, “Wako wapi Samweli na Daudi?” Wakasema, “Wako Nayothi huko Rama.”
Kisha naye akaenda Rama na kufika katika kisima kirefu kilichoko huko Seku. Akauliza, “Samweli na Daudi wako wapi?” Mtu mmoja akasema, “Angalia, Wako Nayothi huko Rama.”
23 Hivyo Sauli akaenda Nayothi huko Rama. Lakini Roho wa Mungu akaja juu yake hata yeye, akawa anatembea huku anatoa unabii hadi akafika Nayothi.
Hivyo Sauli akaenda Nayothi huko Rama. Ndipo Roho wa Mungu pia akaja juu yake, naye alipokuwa akienda alitabiri, hadi alipofika Nayothi huko Rama.
24 Akavua majoho yake na pia akatoa unabii mbele ya Samweli. Akalala hali hiyo ule mchana kutwa na usiku kucha. Hii ndiyo sababu watu husema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”
Na yeye pia, alirarua mavazi yake, naye pia akatabiri mbele ya Samweli siku hiyo akilala uchi mchana kutwa na usiku kucha. Kwa sababu ya jambo hili, watu husema, “Je, Sauli pia ni miongoni mwa manabii?”

< 1 Samweli 19 >