< 1 Samweli 18 >
1 Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe.
Daudi alipokuwa amemaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ilishikana na roho ya Daudi, na Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe.
2 Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake.
Sauli akamweka kazini Daudi siku hiyo, hakumwacha arudi nyumbani kwa baba yake.
3 Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe.
Kisha Yonathani na Daudi wakafanya makubaliano ya urafiki kwa sababu Yonathani alimenda kama roho yake mwenyewe.
4 Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.
Yonathani akavua kanzu aliyokuwa amevaa na kumpa Daudi, akampa na vazi lake la kivita, pamoja na upanga, upinde, na mshipi.
5 Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alitenda kwa hekima, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia.
Daudi alikwenda popote ambapo Sauli alimtuma, naye alifanikiwa. Sauli akamteua Daudi awe mkuu wa wapiganaji. Jambo hili lilipendeza machoni pa watu na katika macho ya watumishi wa Sauli.
6 Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze.
Wakati wanarudi nyumbani kutoka kuwapiga Wafilisti, wanawake walitoka miji yote ya Israeli, wakiimba na kucheza, ili kukutana na mfalme Sauli, wakiwa na matowazi, wenye furaha, na wakiwa na ala za muziki.
7 Walipokuwa wanacheza, wakaimba: “Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake.”
Hao wanawake waliimba kwa kupokezana huku wakicheza; Wakiimba: “Sauli ameua maelfu yake, Na Daudi ameua makumi elfu yake.”
8 Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?”
Sauli alikasirika sana, na wimbo huu haukumpendeza. Naye akasema, “Wamemsifia Daudi juu ya makumi elfu, lakini wamenisifia melfu tu mimi! Atapata kitu gani zaidi isipokuwa ufalme?
9 Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi.
Kuanzia siku hiyo na kuendelea, Sauli alimuangalia Daudi kwa mashaka.
10 Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake;
Kesho yake yule roho ya ubaya kutoka kwa Mungu ikamwingia Sauli kwa nguvu. Naye akawa anafanya kama mwendawazimu nyumbani mwake. Hivyo Daudi akapiga kifaa chake, kama alivyofanya kila siku. Sauli alikuwa na mkuki wake mkononi.
11 akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili.
Sauli akatupa mkuki wake, kwani alifikiri, “Nitampigilia ukutani.” Lakini Daudi mara mbili aliepa uwepo wa Sauli.
12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye.
Sauli alimwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, lakini hakuwa na Sauli tena.
13 Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita.
Hivyo Sauli alimuondoa Daudi mbele yake na akamteua kuwa kamanda wa kikosi cha askari elfu moja. Kwa namna hii David alitoka na kuingia mbele ya watu.
14 Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye.
Daudi alikuwa akistawi kwa mambo yake yote, maana BWANA alikuwa pamoja naye.
15 Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa.
Sauli alipoona kwamba Daudi anastawi, alimwogopa.
16 Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao.
Lakini Israeli yote na Yuda walimpenda Daudi, maana alitoka na kuingia mbele yao.
17 Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya Bwana.” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.”
Kisha Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa ni binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupatia awe mke wako. Ila tu uwe jasiri kwa ajili yangu na upigane vita vya BWANA.” Maana Sauli alifikiri, “Usije mkono wangu ukawa juu yake, ila acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.”
18 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?”
Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, na maisha yangu yana nini, au hata maisha ya familia ya baba yangu katika Israeli, kiasi cha kuwa mkwe wa mfalme?” 1 Samweli 18-19-19
19 Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi.
Lakini wakati ambao Merabu, binti Sauli, ilipasa kuwa ameolewa na Daudi, aliozwa kwa Adrieli Mmeholathi.
20 Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli juu ya jambo hili, likampendeza.
Lakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi. Na watu walimwambia Sauli, na jambo hilo likampendeza.
21 Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili kwamba mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.”
Ndipo Sauli akafikiri, “Nitampatia huyu awe mke wake, ili uwe mtego kwake, na hivyo mkono wa Wafilisti pengine uwe juu yake.” Kwa hiyo Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, “Wewe utakuwa mkwe wangu.”
22 Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’”
Sauli akawaamuru watumishi wake, “Ongeeni na Daudi kwa njia ya siri, na mseme, 'Tazama, mfalme anakufurahia, na watumishi wake wote wanakupenda. Sasa basi, uwe mkwe wa mfalme.'”
23 Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.”
Hivyo watumishi wa Sauli wakayasema maneno haya kwa Daudi. Na Daudi akasema, “Kwenu ninyi mnaona ni jambo dogo kuwa mkwe wa mfalme, mimi ni maskini, na heshima yangu ni ndogo.”
24 Watumishi wa Sauli walipomweleza yale Daudi aliyoyasema,
Watumishi wa Sauli wakarudisha kwake taarifa ya maneno ambayo Daudi aliyasema.
25 Sauli akajibu, “Mwambieni Daudi, ‘Mfalme hataki zawadi nyingine kuwa mahari isipokuwa magovi 100 ya Wafilisti, ili kulipiza kisasi juu ya adui zake.’” Mawazo ya Sauli yalikuwa Daudi akaanguke mikononi mwa Wafilisti.
Na Sauli akasema, “Hivi ndivyo mtakavyo mwambia Daudi, 'Mfalme haitaji mahari yoyote, isipokuwa govi mia moja za Wafilisti, ili ajilipize kisasi kwa adui wa mfalme.”' Basi Sauli alifikiri atamwangusha Daudi kwa mkono wa Wafilisti.
26 Watumishi walipomwambia Daudi mambo haya, ikampendeza kuwa mkwewe mfalme. Basi kabla siku iliyopangwa haijafika,
Watumishi wake walipomwambia maneno haya, yakamvutia Daudi awe mkwe wa mfalme.
27 Daudi na watu wake walitoka na kuwaua Wafilisti mia mbili. Akayaleta magovi yao na kupeleka hesabu kamilifu kwa mfalme, ili kwamba apate kuwa mkwewe mfalme. Ndipo Sauli akamwoza Daudi Mikali binti yake.
Kabla siku hizo hazijapita, Daudi aliondoka na watu wake na kuwaua Wafilisti mia mbili. Daudi akazileta govi zao, na kumkadhi mfalme kulingana na idadi yake, ili aweze kufanyika mkwe wa mfalme. Kwa hiyo Sauli akamwoza Mikali, binti yake, awe mkewe.
28 Sauli alipotambua kuwa Bwana alikuwa pamoja na Daudi na kwamba Mikali binti yake anampenda Daudi,
Basi Sauli aliona na kufahamu kwamba BWANA alikuwa pamoja na Daudi. Mikali, binti Sauli, akampenda Daudi.
29 Sauli akazidi kumwogopa Daudi, naye Sauli akabaki kuwa adui yake siku zote za maisha yake.
Sauli akazidi kumwogopa Daudi. Sauli akawa adui wa Daudi daima.
30 Majemadari wa jeshi la Wafilisti waliendelea kupigana vita na kadiri walivyoendelea kupigana, Daudi akazidi kutenda kwa hekima kuliko maafisa wengine wa Sauli, nalo jina lake likajulikana sana.
Ndipo wakuu wa Wafilisti wakajitokeza kwa ajili ya vita, na mara zote walipojitokeza Daudi alifanikiwa zaidi kuliko watumishi wote wa Sauli, hivyo jina lake likapata heshima kubwa.