< 1 Samweli 17 >

1 Wakati huu Wafilisti wakakusanya majeshi yao kwa ajili ya vita, nao wakakusanyika huko Soko katika Yuda. Wakapiga kambi huko Efes-Damimu, kati ya Soko na Azeka.
Basi Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa ajili ya vita. Walikusanyika huko Soko, iliyoko Yuda. Nao wakapiga kambi kati ya Soko na Aseka katika Efesdamimu.
2 Sauli na Waisraeli wakakusanyika na kupiga kambi katika Bonde la Ela na kupanga jeshi ili kupigana vita na Wafilisti.
Sauli na watu wa Israeli alijikusanya na kuweka kambi katika bonde la Ela, na wakapanga vita kukutana na Wafilisti.
3 Wafilisti wakawa katika kilima kimoja na Waisraeli katika kilima kingine, hilo bonde likiwa kati yao.
Wafilisti walisimama juu ya mlima upande mmoja, na Iraeli nao walisimama juu ya mlima upande mwingine wakitenganishwa na bonde kati yao.
4 Shujaa aliyeitwa Goliathi, aliyetoka Gathi, akajitokeza kutoka kambi ya Wafilisti. Alikuwa na urefu dhiraa sita na shibiri moja.
Mtu mmoja mwenye nguvu akatoka katika kambi ya Wafilisti, mtu huyo aliitwa Goliathi wa Gathi, kimo chake mikono sita na shubiri moja.
5 Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya shaba kifuani mwake yenye uzito wa shekeli elfu tano.
Alikuwa na chepeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya chuma. Hiyo dirii ilikuwa na uzito wa shekeli elfu hamsini za shaba.
6 Miguuni mwake alivaa mabamba ya shaba, na alikuwa na mkuki wa shaba mgongoni mwake.
Alikuwa na mabampa ya shaba kwenye miguu yake na mkuki wa shaba katikati ya mabega yake.
7 Mpini wa huo mkuki ulikuwa kama mti wa mfumaji, na ncha ya chuma yake ilikuwa na uzito wa shekeli mia sita. Mbeba ngao wake alitangulia mbele yake.
Ule mpini wa mkuki wake ulikuwa mkubwa, wenye kamba iliyo na kitanzi kwa ajili ya kuutupia kama kamba ya sindano ya mfumaji. Kichwa cha mkuki wake kilikuwa na uzito wa shekeli mia sita za chuma. Aliyembebea ngao alitembea mbele yake.
8 Goliathi alisimama na kuwapigia kelele majeshi ya Israeli, akisema, “Kwa nini mmetoka kupanga vita? Je, mimi si Mfilisti, na ninyi ni watumishi wa Sauli? Chagueni mtu na anishukie mimi.
Alisimama akayapigia kelele majeshi ya Israeli, “Kwa nini mmekuja na mmejipanga kwa ajili ya vita? Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Chagueni mtu kutoka kwenu ateremke na kuja kwangu.
9 Kama anaweza kupigana nami na kuniua, tutakuwa chini yenu; lakini kama nikimshinda na kumuua, ninyi mtakuwa chini yetu na mtatutumikia.”
Kama anaweza kupigana nami na kuniua, hapo ndipo tutakuwa watumwa wenu. Lakini kama nitamshinda na kumuua, basi mtakuwa watumwa wetu na kututumikia.”
10 Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.”
Mfilisti huyo akasema tena, “Leo ninayapa changamoto majeshi ya Israeli. Mnipe mtu ili tuweze kupigana naye.”
11 Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa.
Sauli na Israeli wote waliposikia alichosema Mfilisti huyo, walikata tamaa na kuogopa sana.
12 Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefrathi jina lake Yese aliyekuwa ametoka Bethlehemu ya Yuda. Yese alikuwa na wana wanane, naye wakati wa Sauli alikuwa mzee tena wa umri mkubwa.
Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefraimu wa Bethtelehemu ya Yuda, aliyeitwa Yese. Naye alikuwa na watoto wanane wa kiume. Yese alikuwa mtu mzee katika siku za Sauli, mwenye umri mkubwa kati ya watu.
13 Wana wakubwa watatu wa Yese walikuwa wamefuatana na Sauli vitani: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Eliabu, wa pili Abinadabu, na wa tatu Shama.
Watoto watatu wakubwa wa Yese walimfuata Sauli vitani. Majina ya watoto wake watatu waliokwenda vitani yalikwa ni Eliabu mzaliwa wa kwanza, aliyemfuata Abinadabu, na watatu aliitwa Shama.
14 Daudi ndiye alikuwa mdogo wa wote. Hao wakubwa watatu wakamfuata Sauli,
Daudi ndiye aliyekuwa mdogo kabisa. Hao wakubwa watatu walimfuata Sauli.
15 lakini Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili kuchunga kondoo wa baba yake huko Bethlehemu.
Basi Daudi alikwenda na kurudi akipita kati ya majeshi ya Sauli akiwa na kondoo za baba yake huko Bethtelehemu, ili kuwachunga.
16 Kwa siku arobaini huyo Mfilisti alikuwa akija mbele kila siku asubuhi na jioni na kujionyesha.
Kwa muda wa siku arobaini yule Mfilisti mwenye nguvu alikuwa akijitokeza asubuhi na jioni kwa ajili ya vita.
17 Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao.
Kisha Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Wapelekee kaka zako efa ya bisi na hii mikate kumi, na uzipeleke upesi kule kambini kwa ajili ya kaka zako.
18 Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao.
Pia peleka hizi jibini kumi kwa jemedari wa kikosi chao cha elfu. Ukawaangalie wako na hali gani kisha uniletee habari kuhusu wanavyoendelea vizuri.
19 Wao wako pamoja na Sauli na watu wote wa Israeli huko kwenye Bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.”
Kaka zako wako pamoja na Sauli na watu wote wa Israeli katika bonde la Ela, wanapigana na Wafilisti.”
20 Asubuhi na mapema Daudi akaondoka, akaliacha kundi la kondoo pamoja na mchungaji, akapakia vitu vile na kuondoka, kama vile Yese alivyokuwa amemwagiza. Akafika kambini wakati jeshi lilikuwa likitoka kwenda kwenye sehemu yake ya kupigania, huku wakipiga kelele za vita.
Daudi aliamka asubuhi na mapema na kuliacha kundi chini ya uangalizi wa mchungaji. Akachukua vile vitu na kuondoka, kama Yese alivyomwamuru. Akafika kambini wakati jeshi linaondoka kwenda uwanja wa vita wakipiga kelele za vita.
21 Israeli na Wafilisti walikuwa wakipanga safu zao wakitazamana.
Nao Israeli na Wafilisti walijipanga kivita, jeshi dhidi ya jeshi.
22 Daudi akaacha vile vitu vyake kwa mtunza vifaa, akakimbilia katika safu za vita na kuwasalimu ndugu zake.
Daudi aliviacha vitu vyake kwa mtunza mahitaji, akalikimbilia jeshi, na kuwasalimia kaka zake.
23 Alipokuwa akisema nao, Goliathi, yule Mfilisti shujaa kutoka Gathi, akajitokeza mbele ya safu zake na kupiga ile kelele yake ya kawaida ya matukano, naye Daudi akayasikia.
Alipoongea nao, yule mtu mwenye nguvu, Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akajitokeza kutoka majeshi ya Wafilisti, naye akasema maneno yaleyale kama hapo mwanzo. Naye Daudi akayasikia.
24 Waisraeli walipomwona yule mtu, wote wakamkimbia kwa woga mkuu.
Watu wote wa Israeli walipomwona Goliathi, walimkimbia na waliogopa sana.
25 Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.”
Watu wa Israeli walisema, “Umemuona mtu huyu aliyejitokeza? Amekuja kuipa changamoto Israeli. Basi mfalme atampa mali nyingi mtu atakayemua, atamuozesha binti yake, na familia ya baba yake haitalipa kodi katika Israeli.”
26 Daudi akauliza watu waliokuwa wamesimama karibu naye, “Je, atafanyiwa nini mtu atakayemuua huyu Mfilisti na kuondoa aibu hii katika Israeli? Ni nani huyu Mfilisti asiyetahiriwa hata atukane majeshi ya Mungu aliye hai?”
Daudi akawauliza watu waliosimama karibu naye, “Atafanyiwa nini mtu ambaye atamuua Mfilisti huyu na kuiondolea Israeli fedheha? Ni nani Mfilisti huyu asiyetahiriwa ayatukanaye majeshi ya Mungu aliye hai?”
27 Wakarudia yale yaliyokuwa yamesemwa na kumwambia kuwa, “Hili ndilo atakalotendewa mtu yule atakayemuua.”
Ndipo watu wakarudia kile walichokuwa wamesema na kumwambia, “Ndivyo iitakavyofanyika kwa mtu atakayemuua.”
28 Eliabu nduguye mkubwa Daudi alipomsikia akizungumza na watu hasira ikawaka juu yake akamuuliza, “Kwa nini umeteremka kuja hapa? Nao wale kondoo wachache kule nyikani umewaacha na nani? Ninajua jinsi ulivyo na kiburi na jinsi moyo wako ulivyo mwovu; umekuja hapa kutazama vita tu.”
Kaka yake mkubwa Eliabu, alisikia wakati akisema na watu. Hasira ya Eliabu ikawaka moto dhidi ya Daudi, naye akamuuliza, “Kwa nini umekuja hapa? Wale kondoo wachache umewaacha na nani huko nyikani? Nakijua kiburi chako, na utundu wa moyo wako; maana umekuja hapa ili uweze kuona mapigano.”
29 Daudi akasema, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi hata kuongea.”
Naye Daudi akamjibu, “Nimefanya nini sasa? Mimi si nuliuliza swali tu?
30 Daudi akamgeukia mtu mwingine na kumuuliza jambo lilo hilo, nao watu wakamjibu vilevile kama mwanzo.
Akamgeukia mtu mwingine na kumwacha huyo, na kusema vivyo hivyo. Nao watu wakajibu vilevile kama mwanzo.
31 Lile Daudi alilosema likasikiwa na kuelezwa kwa Sauli, naye Sauli akatuma aitwe.
Maneno aliyosema Daudi yaliposikika, askari waliyasema tena kwa Sauli, naye akawatuma kwa Daudi.
32 Daudi akamwambia Sauli, “Mtu yeyote asife moyo kwa habari ya huyu Mfilisti; mtumishi wako atakwenda kupigana naye.”
Kisha Daudi akamwambia Sauli, “Pasiwepo moyo wa mtu atakayezimia kwa sababu ya Mfilisti huyo; Mtumishi wako atakwenda kupigana na Mfilisti huyu.”
33 Sauli akamjibu Daudi, “Wewe hutaweza kwenda kupigana dhidi ya huyu Mfilisti; wewe ni kijana tu, naye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.”
Sauli akamwambia Daudi, “Huwezi kumpinga Mfilisti ama kupigana naye; wewe ni kijana tu, na yeye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.”
34 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako amekuwa akichunga kondoo wa baba yake. Wakati simba au dubu alikuja na kuchukua kondoo kutoka kundi,
Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake. Mara simba au dubu alikuja akamchukua mwana kondoo kutoka kundini,
35 nilifuatia, nikampiga na nikampokonya kondoo kwenye kinywa chake. Aliponigeukia, nilimkamata nywele zake, nikampiga na kumuua.
Nilimfukuza na kumshambulia na kumpokonya kutoka kinywani mwake. Na aliponirukia, nilimshika ndevu zake, nilimpiga, na kumuua.
36 Mtumishi wako ameshaua simba na dubu pia; huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa hao, kwa sababu ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
Mtumishi wako amekwisha kmuua simba na dubu. N huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa wanyama hao, kwa kuwa ameyadharau majeshi ya Mungu aliye hai.”
37 Bwana ambaye aliniokoa toka katika makucha ya simba na makucha ya dubu ataniokoa kutoka mikono ya huyu Mfilisti.” Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, naye Bwana na awe pamoja nawe.”
Daudi akasema, “BWANA aliyeniokoa kutoka makucha ya simba na makucha ya dubu. Ataniokoa kutoka mkono wa Mfilisti huyu.” Kisha Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, BWANA awe pamoja nawe.”
38 Ndipo Sauli akamvika Daudi silaha zake mwenyewe za vita. Akamvika dirii na chapeo ya shaba kichwani mwake.
Sauli akamvika Daudi vazi lake la vita. Akamvika chepeo ya shaba kichwani pake, na akamvika koti la chuma.
39 Daudi akajifunga upanga juu ya hayo mavazi na kujaribu kutembea kwa sababu alikuwa hana uzoefu navyo. Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda nikiwa nimevaa hivi, kwa sababu sina uzoefu navyo.” Hivyo akavivua.
Daudi akaufunga upanga wake juu ya vazi la Sauli. Lakini hakuweza kutembea, kwa sababu hakupata mafunzo kwa mavazi hayo. Ndipo Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda kupigana nikiwa na haya, maana sikupata mafunzo kwa haya.” Kwa hiyo Daudi akayavua.
40 Kisha akachukua fimbo yake mkononi, akachagua mawe laini matano kutoka kwenye kijito, akayaweka kwenye kifuko ndani ya mfuko wake wa kichungaji, akiwa na kombeo yake mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
Akachukua fimbo mkononi mwake na akachagua mawe matano laini kutoka katika kijito; akayaweka kwenye mfuko wake wa kichungaji. Kombeo lake lilikuwa mkononi akawa anamsogelea yule Mfilisti.
41 Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi.
Yule Mfilisti akaja na kumsogelea Daudi, mbeba ngao yake akiwa mbele yake.
42 Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau.
Mfilisti alipotazama kila upande na kumuona Daudi, akamdharau, maana alikuwa kijana tu, mwekundu, na umbo la kupendeza.
43 Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
Ndipo Mfilisti akamuuliza Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata ukanijia na fimbo? Naye Mfilisti kwa miungu yake akamlaani Daudi.
44 Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.”
Huyo Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu, na nyama yako nitawatupia ndege wa angani na wanyama wa mwituni.”
45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana.
Daudi akamjibu Mfilisti, “Unaniijia kwa upanga, kwa mkuki na mkuki mdogo. Bali mimi nakuijia kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa Majeshi ya Israeli, uliyemdharau.
46 Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli.
Leo BWANA atanipa ushindi dhidi yako, na nitakuua na kukiondoa kichwa chako kwenye kiwiliwili. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni walioko duniani mizoga ya jeshi la Wafilisti, ili dunia yote ijue kwamba yupo Mungu katika Israeli,
47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”
na kusanyiko hili lote lijue kwamba BWANA hatoi ushindi kwa upanga wala kwa mkuki. Kwa kuwa vita ni ya BWANA, na atawaweka katika mkono wetu.”
48 Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye.
Mfilisti aliponyanyuka na kukaribia akutane na Daudi, ndipo Daudi akakimbia kwa haraka kuelekea jeshi la adui ili akutane naye.
49 Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka chini kifudifudi.
Daudi aliweka mkono wake mfukoni, akachukua jiwe kutoka humo, akalitupa kwa kombeo, na likampiga Mfilisti kwenye paji la uso, akaanguka chini kifudifudi.
50 Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mikononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumuua.
Daudi alimshinda Mfilisti kwa kombeo na kwa jiwe moja. Alimpiga huyo Mfilisti na kumuua. Mkononi mwa Daudi hakukuwa na upanga.
51 Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumuua, akakata kichwa chake kwa ule upanga. Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia.
Ndipo Daudi akakimbia akasimama juu ya Mfilisti na kutwaa upanga wake, akauchomoa kutoka alani, akamuua, na kukata kichwa chake kwa upanga huo.
52 Ndipo watu wa Israeli na Yuda wakainuka kwenda mbele wakipiga kelele na kufuatia Wafilisti mpaka kwenye ingilio la Gathi kwenye malango ya Ekroni. Maiti zao zilitawanyika kando ya barabara ya Shaaraimu hadi Gathi na Ekroni.
Ndipo watu wa Israeli na wale wa Yuda wakaamka kwa kelele, na kuwafukuza Wafilisti kuvuka bonde na malango ya Ekroni. Na maiti za Wafilisti walilala katika njia iendayo Shaaraimu, na njia yote kuelekea Gathi na Ekroni.
53 Waisraeli waliporudi kutoka kuwafukuza Wafilisti, waliteka nyara kutoka kambi yao.
Watu wa Israeli wakarejea kutoka kuwafukuza Wafilisti, na wakateka nyara kambi yao.
54 Daudi akachukua kichwa cha yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu, naye akaweka silaha za huyo Mfilisti katika hema lake mwenyewe.
Daudi akachukua kichwa cha Mfilisti na kukipeleka Yerusalemu, lakini akaliweka vazi la vita katika hema lake.
55 Sauli alipomwona Daudi anakwenda kukabiliana na huyo Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, “Abneri, yule kijana ni mwana wa nani?” Abneri akajibu, “Hakika kama uishivyo, ee mfalme, mimi sifahamu.”
Sauli alipomuona Daudi akienda kukabiliana na yule Mfilisti, akamwambia Abneri, jemedari wa jeshi, “Abneri, kijana huyu ni mtoto wa nani? Abneri akasema, “Kama uishivyo, mfalme, mimi sijui.”
56 Mfalme akasema, “Uliza huyu kijana ni mwana wa nani.”
Naye mfalme akasema, “Waulize wanaoweza kufahamu, mvulana huyu ni kijana wa nani.”
57 Mara Daudi aliporudi kutoka kumuua huyo Mfilisti, Abneri akamchukua na kumleta mbele ya Sauli. Daudi alikuwa bado anakishikilia kichwa cha yule Mfilisti.
Daudi aliporudi kutoka kumuua yule Mfilisti, Abneri alimchukuwa, na kumleta mbele ya Sauli akiwa na kichwa cha Mfilisti mkononi mwake.
58 Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” Daudi akasema, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese wa Bethlehemu.”
Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mtoto wa nani? Na Daudi akamjibu, “Mimi ni mtoto wa mtumishi wako Yese Mbethlehemu.”

< 1 Samweli 17 >