< 1 Samweli 16 >
1 Bwana akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli mpaka lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.”
BWANA akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli kwa muda gani, ikiwa nimemkataa asiwe mfalme juu ya Israeli? Ijaze pembe yako mafuta na uende. Nitakutuma kwa Yese akaaye Bethlehemu, maana nimejichagulia mfalme katika wanawe.
2 Lakini Samweli akasema, “Nitakwendaje? Sauli atasikia juu ya jambo hili na ataniua.” Bwana akamwambia, “Chukua mtamba wa ngʼombe na useme, ‘Nimekuja kumtolea Bwana dhabihu.’
Samweli akasema, “Jinsi gani nitaenda? Kama Sauli akisikia jambo hili, ataniua.” BWANA akasema, “chukua mtamba na useme, 'Nimekuja kutoa dhabihu kwa BWANA.'
3 Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakalofanya. Utamtia mafuta kwa ajili yangu yule nitakayekuonyesha.”
Umwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha kile utakachofanya. Utamtia mafuta kwa ajili yangu yule nitakaye kuambia.”
4 Samweli akafanya kile Bwana alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?”
Samweli akafanya kama BWANA alivyosema na akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji walikuwa wakitetemeka walipokuja kuonana naye na wakasema, “Je, umekuja kwa amani?”
5 Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu.
Naye akasema, “kwa amani; Nimekuja kutoa dhabihu kwa BWANA. Jitoeni wenyewe kwa BWANA kwa ajili ya dhabihu na muandamane nami,” Na akamweka wakfu Yese na watoto wake kwa BWANA, na baadaye aliwaita wote kwenye dhabihu.
6 Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa Bwana anasimama hapa mbele za Bwana.”
Walipofika, akamwangalia Eliabu na akajisemea mwenyewe kwamba mtiwa mafuta wa BWANA hakika amesimama mbele yake.
7 Lakini Bwana akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Bwana hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Bwana hutazama moyoni.”
Lakini BWANA akamwambia Samweli, “Usimwangalie sura yake ya nje, au kimo cha umbo lake; kwa sababu nimemkataa. Maana BWANA haangalii kama mtu aangaliavyo; mtu hutazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.”
8 Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu Bwana hakumchagua.”
Kisha Yese akamwita Abinadabu akamwambia apite mbele ya Samweli. Na Samweli akasema, “Hata huyu BWANA hakumchagua.”
9 Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu Bwana hakumchagua.”
Kisha Yese akmwambia Shama apite karibu. Na Samweli akasema, “Hata huyu BWANA hakumchagua.”
10 Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “Bwana hajawachagua hawa.”
Yese akawaleta watoto wake saba wakapita mbele ya Samweli. Na Samweli akamwambia Yese, “Hakuna hata mmoja aliyechaguliwa na BWANA kati ya hawa.”
11 Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?” Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.” Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi mpaka afike.”
Kisha Samweli akamuulia Yese, “Je, watoto wako wote wako hapa?” Naye akajibu, “Yupo mdogo kabisa lakini anachunga kondoo.” Samweli akamwambia Yese, “Tuma watu wakamwite; maana hatutakaa chini hadi atakapofika hapa.”
12 Basi akatuma aitwe naye akaletwa. Alikuwa mwekundu, mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza. Ndipo Bwana akasema, “Inuka na umtie mafuta, huyu ndiye.”
Yese akawatuma watu wakamleta. Naye kijana huyu alikuwa mwekundu na mwenye macho mazuri na mwenye muonekano mzuri. BWANA akasema, “Amka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.”
13 Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumtia mafuta mbele ya ndugu zake, kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Bwana akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.
Ndipo Samweli akachukua pembe yenye mafuta na kumtia mafuta katikati ya kaka zake. Roho wa BWANA akamwijia Daudi kwa nguvu tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samweli akanyanyuka na kwenda Rama.
14 Basi Roho wa Bwana alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Bwana ili imtese.
Basi Roho wa BWANA akamwacha Sauli, badala yake roho ya ubaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua.
15 Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Angalia, roho mbaya imeachiwa nafasi na Bwana nayo inakutesa.
Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho ya ubaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walioko hapa kutafuta mtu ambaye anaweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.”
Haya bwana wetu hebu sasa amuru watumishi wako walio mbele yako wamtafute mtu mwenye ujuzi wa kupiga kinubi. Basi ikwa roho wa ubaya kutoka kwa Mungu yuko juu yako, atakipiga kinubi nawe utajisikia vizuri.”
17 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.”
Sauli akawaambia watumishi wake, “Mnitafutie mtu anayeweza kupiga vizuri na mmlete kwangu.”
18 Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa wa vita. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. Bwana yu pamoja naye.”
Ndipo kijana mmoja kati yao akajibu, na kusema, “Nimemuona mtoto wa Yese Mbethtelehemu, aliye mjuzi katika kupiga, ni mwenye nguvu, mtu jasiri, mtu wa vita, mwenye busara aongeapo, mtu mzuri kwa uso; na BWANA yuko pamoja naye.”
19 Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.”
Hivyo Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mtoto wako Daudi, anayewatunza kondoo.” 1 Samweli! 6: 20-21
20 Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe.
Yese akamchukua punda aliyebeba mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, na akamtuma kwa Sauli pamoja na vitu hivyo.
21 Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake.
Ndipo Daudi akafika kwa Sauli na kuanza kazi yake. Sauli alimpenda sana Daudi, na akawa mbeba silaha wake.
22 Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.”
Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi awe mbele yangu, maana amepata kibali machoni pangu.”
23 Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.
Wakati wowote roho ya usumbufu kutoka kwa Mungu ikiwapo juu ya Sauli, Daudi alichukuwa kinubi na kukipiga. Hivyo Sauli angeburudishwa na kupona, na huyo roho wa usumbufu angemtoka.