< 1 Samweli 14 >

1 Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake.
Siku moja, Yonathani mwana wa Sauli alimwambia mbeba silaha wake aliye mdogo, “Njoo, hebu twende hadi upande mwingine kwenye ngome ya Wafilisti.” Lakini hakumjulisha baba yake.
2 Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu kama 600,
Sauli alikuwa akikaa nje ya mji wa Gibea chini ya mti wa mkomamanga ulio katika Migroni. Takribani watu mia sita walikwa pamoja naye,
3 miongoni mwao alikuwepo Ahiya, ambaye alikuwa amevaa kisibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Bwana huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka.
akiwemo Ahiya mwana wa Ahitubu (nduguye Ikabodi) mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Watu hao hawakujua kwamba Yonathani ameondoka.
4 Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwepo na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene.
Katikati ya vichochoro, ambavyo Yonathani alinuia kuvipita hadi ngome ya Wafilisti, kulikuwa na mwamba wenye mteremko mkali upande mmoja, na mteremko mkali upande mwingine. Jabali moja liliitwa Bosesi, na jingine liliitwa Sene.
5 Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba.
Lile jabali lenye mteremko mkali zaidi liliinuka upande wa kaskazini mbele ya Mikmashi, na jingine upande wa kusini mbele ya Geba.
6 Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda Bwana atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia Bwana kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”
Yonathani akamwambia kijana mbeba silaha, “Njoo, na tuvuke hadi ngome ya hawa wasiotahiriwa. Pengine BWANA atatenda kwa niaba yetu, kwa maana hakuna kitu kiwezacho kumzuia BWANA asiokoe kwa wengi au kwa watu wachache.”
7 Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.”
Mbeba silaha wake akajibu, “Fanya kila kitu kilicho ndani ya moyo wako. Songa mbele, tazama, niko pamoja nawe, nitatii maagizo yako yote.”
8 Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone.
Ndipo Yonathani akasema, “Tutavuka twende kwa watu hao, na tutajionesha wenyewe kwao.
9 Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao.
Kama watatuambia, 'Subirini hapo hadi tutakapokuja kwenu' - basi tutabaki katika sehemu yetu na hatutavuka kwenda kwao.
10 Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba Bwana amewatia mikononi mwetu.”
Lakini kama watajibu, 'Njoni kwetu,' ndipo tutavuka; kwa sababu BWANA amewaweka mkononi mwetu. Hii ndiyo itakuwa ishara yetu.”
11 Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.”
Kwa hiyo wote wawili wakajifunua mbele ya ngome ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Angalia, Webrania wanakuja kutokea kwenye mashimo walimojificha.”
12 Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu nasi tutawakomesha.” Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; Bwana amewatia mikononi mwa Israeli.”
Ndipo watu wa ile ngome wakamwita Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njoni huku kwetu, tutawaonesha jambo fulani.” Na Yonathani akamwambia mbeba silaha wake; “Nifuate nyuma yangu, kwa sababu BWANA amewaweka katika mkono wa Israeli.”
13 Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake.
Yonathani alipanda juu kwa mikono na miguu yake, na mbeba silaha akimfuata nyuma yake. Wafilisti waliuwawa mbele ya Yonathani, na mbeba silaha wake akiwaua baadhi nyuma yake.
14 Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka.
Hilo shambulio la kwanza walilofanya Yonathani na mbeba silaha wake, waliua watu wapatao ishirini katika urefu wa nusu handaki kwenye eka moja ya ardhi.
15 Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.
Kukawa na hofu kubwa katika kambi, uwandani, na katika watu. Hata ngome ya jeshi na watekaji nyara nao wakawa na hofu kubwa
16 Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote.
Ndipo walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona kundi la askari wa Wafilisti likitawanyika, wakienda kule na huku.
17 Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka katikati yetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo.
Kisha Sauli akawaambia watu aliokuwa nao, “Mjihesabu ili muone nani hayupo hapa.”Walipokuwa wamehesabu, wakagundua kuwa Yonathani na mbebaji wa silaha zake hawapo.
18 Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.)
Sauli akamwambia Ahiya, “Lete hapa naivera ya Mungu”- kwa maana siku hiyo Ahiya alivaa naivera akiwa pamoja na askari wa Israeli.
19 Wakati Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.”
Wakati Sauli akiongea na kuhani, kelele na ghasia kubwa iliendelea na kuongezeka katika kambi ya Wafilisti. dipo sauli akamwambia kuhani, “Acha kazi unayofanya.”
20 Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake.
Sauli na watu wote aliokuwa nao wakajipanga na kwenda kwenye mapigano. Upanga wa kila Mfilisti ulikwa juu ya Mfilisti mwenzake, na kulikuwa na ghasia kubwa.
21 Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
Basi Waebrania ambao mwanzoni walijiunga na Wafilisti, na kwenda kwenye kambi yao, wao pia waliungana na Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
22 Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii.
Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika milima karibu na Efraimu waliposikia kwamba Wafilisti wamekimbia, nao pia wakawafuata Wafilisti nakuwafukuza kwenye hiyo vita.
23 Hivyo Bwana akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.
Hivyo siku hiyo BWANA aliwaokoa Israeli, na mapigano yalivuka kupitiliza Beth aveni.
24 Basi watu wa Israeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote ambaye atakula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula.
Siku hiyo watu wa Israeli walifadhaika kwa sababu Sauli aliwaweka watu chini ya kiapo akasema, “Na alaaniwe mtu atakaye kula chakula kabla ya jioni na kabla sijalipiza kisasi kwa maadui zangu.” Hivyo hakuna hata mmoja kati ya watu wote aliyeonja chakula.
25 Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwepo na asali ardhini.
Ndipo watu wote wakaingia msituni na kuona asali ikiwa juu ya ardhi.
26 Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo.
Watu walipoingia humo msituni, asali ilitiririka, lakini hakuna aliyeweka mkono wake kinywani kwa maana watu waliogopa kiapo.
27 Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakawa maangavu.
Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kwamba baba yake amewaagiza watu kwa kiapo. Akanyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya kwenye sega la asali. Kisha akanyoosha mkono wake hadi kinywani mwake, na macho yake yakaangaziwa.
28 Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.”
Ndipo mmoja wa watu hao, akamwambia, “Baba yako aliwaagiza watu kwa mkazo na kwa kiapo, kwa kusema, 'Alaaniwe mtu atakaye kula chakula kwa siku ya leo,' ingawa watu wamedhoofika kwa ajili ya njaa.”
29 Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi nilivyopata nguvu mpya nilipoonja asali hii kidogo.
Baadaye Yonathani alisema, “Baba yangu amefanya matatizo katika nchi. Angalia jinsi macho yangu alivyotiwa nuru kwa sababu nilionja asali hii kidogo.
30 Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangalikula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?”
Je, siyo vivuri sana kama leo watu wangekula bila kizuizi nyara walizopata kutoka kwa maadui zao? Kwa sababu sasa mauaji hayakuwa makubwa katikati ya Wafilisti.”
31 Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi mpaka Aiyaloni, walikuwa wamechoka.
Siku hiyo waliwashambulia Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni. Na watu walikuwa wamechoka sana.
32 Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ngʼombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu.
Hivyo watu wakazivamia nyara na kuchukua kondoo, ng'ombe na ndama na kuwachinja hapo chini. Watu walikula nyama zao pamoja na damu.
33 Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya Bwana kwa kula nyama yenye damu.” Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.”
KIsha wakamwambia Sauli, “Tazama, watu wanamtenda BWANA dhambi kwa kula pamoja na damu.” Sauli akasema, “Mmetenda isivyo haki. Sasa, viringisheni jiwe kubwa kwangu.” Sauli akasema,
34 Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ngʼombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya Bwana kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’” Hivyo kila mmoja akaleta ngʼombe wake jioni ile na kumchinja hapo.
“Nendeni kati watu, na muwaambie, 'Kila mtu alete ng'ombe na kondoo wake, wawachinje hapa, na kuwala. Msimtende BWANA dhambi kwa kula na damu.”' Kwa hiyo watu wote wakaleta kila mtu na ng'ombe wake usiku huo na kuwachinja mahali hapo.
35 Ndipo Sauli akamjengea Bwana madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu.
Sauli akamjengea BWANA madhabahu, ambayo ilikuwa ya kwanza kwake kumjengea BWANA.
36 Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara mpaka mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.” Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.” Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.”
Ndipo Sauli akasema, “Haya tuwafukuze Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi asubuhi; tusimwache hata mtu mmoja akiwa hai.” Nao wakamjibu, “Fanya unaloona linakupendeza.” Lakini kuhani akasema, “Hebu na tumkaribie Mungu mahali hapa.”
37 Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile.
Sauli alitaka kumuuliza Mungu maswali zaidi, “Je, inanipasa kuwafukuza Wafilisti? Je, utawaweka katika mkono wa Israeli?” Lakini siku hiyo BWANA hakumjibu kitu.
38 Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo.
Ndipo Sauli akasema, “Njoni hapa, viongozi wote wa watu; mjue na kuona jinsi dhambi hii ilivyotokea leo.
39 Kwa hakika kama Bwana aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa juu ya mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno.
Kwa maana, kama BWANA aishivyo, aliyewaokoa Israeli, hata kama angekuwa mwanangu Yonathani, atapaswa kufa.” Lakini hakuna hata mtu mmoja miongoni mwa watu aliye mjibu neno.
40 Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.” Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.”
Basi akawaambia Waisraeli wote, “Simameni upande mmoja, na mimi na Yonathani tutasimama upande mwingine.” Kisha watu wakamwambia Sauli, “Fanya lile unaloona jema kwako.”
41 Kisha Sauli akamwomba Bwana, Mungu wa Israeli, akisema, “Nipe jibu lililo sawa.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama.
Kwa hiyo, Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, “Tuoneshe Thumimu.” Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu walinusurika kuchaguliwa.
42 Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani.
Basi Sauli akasema, “Tupa mawe ya bahati nasibu tuone kati yangu na mwanangu Yonathani.” Ndipo Yonathani akatwaliwa.
43 Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.” Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?”
Kisha Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie umefanya nini.” Yonathani akamwambia baba yake, “Nilionja asali kidogo kwa kutumia ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwangu. Niko hapa; Nitakufa.”
44 Sauli akasema, “Mungu na anishughulikie kwa ukali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.”
Sauli akasema, “Mungu afanye hivyo na kuzidi hata kwangu, kama Yonathani hautakufa.”
45 Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta wokovu huu mkubwa Israeli? Hasha! Hakika kama Bwana aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa.
Basi watu wakamuuliza Sauli, “Je, inampasa Sauli afe, ni nani aliyetekeleza ushindi huu mkubwa kwa ajili ya Israeli? Mbali na hayo! Kama BWANA aishivyo, hata unywele mmoja wa kichwa chake hautaanguka chini, kwa maana leo amefanya kazi pamoja na Mungu.” Hivyo hao watu walimuokoa Yonathani ili asife.
46 Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao.
Basi Sauli akasita kuwafuatia Wafilisti, nao wakarudi katika makao yao.
47 Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda.
Sauli alipoanza kutawala juu ya Israeli, alipigana na adui zake wote kila upande. Alipigana dhidi ya Moabu, dhidi ya watu wa Amoni, Edomu, wafalme wa Zoba, na Wafilisti. Popote alipogeukia aliwapiga kwa adhabu adui zake.
48 Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara.
Alitenda kwa ushujaa mkubwa na kuwashinda Waamaleki. Aliwaokoa Israeli kutoka mikono ya watu ambao waliwateka nyara.
49 Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali.
Basi wana wa Sauli walikuwa ni hawa Yonathani, Ishvi, na Malkishua. Na majina ya binti zake wawili yalikuwa ni haya, Merabu mzaliwa wa kwanza, na mdogo aliitwa Mikali.
50 Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti wa Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli.
Jina la mke wa Sauli aliitwa Ahinoamu; naye alikuwa binti Ahimaasi. Na jina la Jemedari wa jeshi lake aliitwa Abneri mwana wa Neri, baba mdogo wa Sauli.
51 Babaye Sauli yaani, Kishi na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli.
Kishi alikuwa baba yake Sauli; na Neri alikuwa baba yake na Abneri, wote walikuwa wana wa Abieli.
52 Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.
Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya Wafilisti katika siku zote za Sauli. Naye alipomwona mtu yeyote mwenye nguvu, au mtu yeyote jasiri, alimuunganisha kwake.

< 1 Samweli 14 >