< 1 Samweli 12 >

1 Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu.
Samweli aksema na Israeli wote, “Nimesikia kila kitu mlichoniambia, na nimemweka mfalme juu yenu.
2 Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini kwa habari yangu mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu mpaka siku hii ya leo.
Basi, yupo hapa mfalme aliyeko mbele yenu, mimi nimezeeka nakujaa mvi; na watoto wangu wako pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu hadi leo.
3 Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni juu yangu mbele za Bwana na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Ni nani nimepata kumwonea? Ni kutoka kwenye mkono wa nani nimepokea rushwa ili kunifanya nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, mimi nitawarudishia.”
Mimi niko hapa, Nishuhudieni mbele za BWANA na mbele za mtiwa mafuta wake. Nimechukua ng'ombe wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimemdhulumu? Nimemwonea nani? Nimepokea rushwa kutoka mikono ya nani inipofushe macho yangu? Nishuhudieni, nami nitawarudishia
4 Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutuonea. Hujapokea chochote kutoka kwenye mkono wa mtu awaye yote.”
Nao wakasema, Haujatudanganya, kutuonea, au kuiba chochote kutoka mkono wa mtu yeyote.”
5 Samweli akawaambia, “Bwana ni shahidi juu yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.” Wakasema, “Yeye ni shahidi.”
Akawaambia, “BWANA ni shahidi juu yenu, na masihi wake leo ni shahidi, kwamba hamkuona kitu mkononi mwangu.” Na wao wakajibu, “BWANAni shahidi.”
6 Kisha Samweli akawaambia watu, “Bwana ndiye alimchagua Mose na Aroni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri.
Samweli akawaambia watu, “BWANA ndiye aliyemteua Musa na Haruni, na ndiye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri.
7 Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za Bwana wa matendo yote ya haki yaliyofanywa na Bwana kwenu na kwa baba zenu.
Basi sasa, jihudhurisheni, ili niweze kutoa utetezi juu yenu kwa BWANA kuhusu matendo yote ya haki ya BWANA, ambayo aliwafanyia ninyi na baba zenu.
8 “Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia Bwana kwa ajili ya msaada, naye Bwana akawatuma Mose na Aroni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.
Yakobo alipokuwa amefika Misri, na babu zenu walimlilia BWANA. BWANA alimtuma Musa na Haruni, waliowaongoza babu zenu kutoka Misri na wakaja kukaa sehemu hii.
9 “Lakini wakamsahau Bwana Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao.
Lakini walimsahau BWANA Mungu wao; akawauza katika mkono wa Sisera, jemedari wa majeshi ya Hazori, katika mkono wa Wafilisti, na katika mkono wa mfalme wa Moabu; hawa wote walipigana na babu zenu.
10 Wakamlilia Bwana na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha Bwana na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’
Wakamlilia BWANA mkasema, 'Tumefanya dhambi, kwa sababu tumemwacha BWANA na tumewatumikia Mabaali na Mashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya maadui zetu, na tutakutumikia.'
11 Ndipo Bwana akawatuma Yerub-Baali, Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.
Hivyo BWANA akawatuma Yerubu Baali, Bedani, Yefta na Samweli, na akawapa ushindi dhidi ya maadui zenu wote waliowazunguka, na kwamba mliishi kwa amani.
12 “Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa Bwana Mungu wenu alikuwa mfalme wenu.
Mlipoona kwamba Nahashi mfalme wa watu wa Amoni amekuja dhidi yenu, mkaniambia, 'Hapana! Badala yake, mfalme awepo atawale juu yetu'- ingawa BWANA, Mungu wenu, alikuwa mfalme wenu.
13 Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, Bwana amemweka mfalme juu yenu.
Sasa yupo hapa mfalme ambaye mmemchagua, mliyemuomba na ambaye BWANA amemteua awe mfalme juu yenu.
14 Kama mkimcha Bwana na kumtumikia na kumtii nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayetawala juu yenu mkimfuata Bwana, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu!
Ikiwa mnamhofu BWANA, mtumikieni, muitii sauti yake, msikaidi amri ya BWANA, basi wote wawili ninyi na mfalme anayewatawala mtakuwa wafuasi wa BWANA Mungu wenu.
15 Lakini kama hamkumtii Bwana, nanyi kama mkiasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.
Kama hamtaitii sauti ya BWANA, mkaasi amri za BWANA, ndipo mkono wa BWANA utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya babu zenu.
16 “Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Bwana anakwenda kulifanya mbele ya macho yenu!
Hata sasa muwepo kabisa na muone jambo kubwa ambalo BWANA atalifanya mbele ya macho yenu.
17 Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Bwana mlipoomba mfalme.”
Je, leo si mavuno ya ngano? Nitamwomba BWANA, naye ataleta ngurumo na mvua. Ndipo mtajua na kuona kwamba uovu wenu ni mwingi, mlioufanya machoni pa BWANA, kujiombea mfalme wenu ninyi wenyewe.”
18 Kisha Samweli akamwomba Bwana, na siku ile ile Bwana akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Bwana na Samweli.
Hivyo Samweli akamwomba BWANA; na siku iyo hiyo BWANA akatuma ngurumo na mvua. Ndipo watu wote wakamwogopa sana BWANA pamoja na Samweli.
19 Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”
Kisha watu wote wakamwambia Samweli, “Waombee watumishi wako kwa BWANA Mungu wako, ili tusife. Kwa maana tumeongeza uovu huu juu ya dhambi zetu tulipojiombea mfalme sisi wenyewe.”
20 Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa moyo wenu wote.
Samweli akawajibu, “Msiogope. Mmefanya uovu wote huu, lakini msigeukie mbali na BWANA, bali mtumikieni BWANA kwa moyo wenu wote.
21 Msigeukie sanamu zisizofaa. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana.
Wala msigeuke na kufuata mambo matupu yasiyo na faida au kuwaokoa, kwa sababu ni ubatili.
22 Kwa ajili ya jina lake kuu Bwana hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza Bwana kuwafanya kuwa wake mwenyewe.
Kwa ajili ya jina lake kuu, BWANA hatawakataa watu wake, kwa sababu imempendeza BWANA kuwafanya ninyi kuwa watu kwa ajili yake.
23 Kwa habari yangu, iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya Bwana kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na ya kunyooka.
Kwangu mimi, iwe mbali nami kumtenda BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi. Badala yake, nitawafundisha njia iliyo njema na sahihi.
24 Lakini hakikisheni mnamcha Bwana na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu.
Mcheni BWANA tu na mtumikieni yeye katika kweli kwa moyo wenu wote. Tafakarini mambo makuu aliyowatendeeni.
25 Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!”
Lakini kama mtadumu kufanya uovu, ninyi wote na mfalme wenu mtaangamizwa.”

< 1 Samweli 12 >