< 1 Samweli 11 >
1 Nahashi yule Mwamoni, akakwea kuuzunguka kwa jeshi mji wa Yabeshi-Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba na sisi, na tutakuwa chini yako.”
2 Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitangʼoa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.”
3 Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote, kama hakuna hata mmoja anayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.”
4 Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa juu ya masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa.
5 Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza jinsi watu wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.
6 Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira.
7 Akachukua jozi ya maksai na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha hofu ya Bwana ikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja.
8 Sauli alipowakusanya huko Bezeki, watu wa Israeli walikuwa 300,000 na watu wa Yuda 30,000.
9 Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni watu wa Yabeshi-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’” Wajumbe walipokwenda na kutoa taarifa hii kwa watu wa Yabeshi, wakafurahi.
10 Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.”
11 Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja mpaka mchana. Wale walionusurika wakasambaa, kiasi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja.
12 Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatawala juu yetu?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.”
13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii Bwana ameokoa Israeli.”
14 Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.”
15 Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele za Bwana. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Bwana, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa.