< 1 Samweli 10 >

1 Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, Bwana hakukutia mafuta uwe kiongozi juu ya watu wake Israeli?
Ndipo Samweli akachukua chupa ya mafuta, akayamimina juu ya kichwa cha Sauli, na akambusu. Akasema, “Je, Mungu hajakutia mafuta uwe mtawala juu ya urithi wake?
2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?”’
Utakapoondoka kwangu leo, utawaona wanaume wawili na kaburi la Raheli, katika nchi ya Benyamini hapo Selsa. Watu hao watakuambia, 'Wale punda mliokuwa mkiwatafuta wamepatikana. Sasa, Baba yako ameacha kuwatunza punda, na ana hofu juu yenu, anasema, “Nitafanya nini kuhusu mwanangu?”
3 “Kisha utakwenda mbele kutoka hapa mpaka uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwa Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai.
Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na utafika katika mwaloni wa Tabori. Utakutana na watu watatu hapo wakienda kwa Mungu huko Betheli, mmoja akibeba wana-mbuzi watatu, mwingine akibeba mikate mitatu, na mwingine akibeba kiriba cha divai.
4 Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao.
Watawasalimu na watawapatia mikate miwili, kutoka mikononi mwao.
5 “Baada ya hayo utakwenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii.
Baada ya hayo, utafika katika mlima wa Mungu, mahali ilipo ngome ya Wafilisti. Utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakiteremka chini kutoka mahali pa juu wakiwa na kinanda, tari, kinubi na filimbi mbele yao; na watakuwa wakitabiri.
6 Roho wa Bwana atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti.
Roho ya BWANA itakujaza, nawe utatabiri pamoja nao, na utabadilishwa na kuwa mtu tofauti.
7 Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.
Basi, ishara hizi zikikufikia, fanya lolote ambalo mikono yako itaona ifanye, kwa sababu Mungu yu pamoja nawe.
8 “Tangulia kushuka mbele yangu mpaka Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.”
Nenda ushuke mbele yangu hadi Gilgali. Kisha nitakufuata huko nitoe dhabihu za kuteketezwa na kutoa dhabihu za amani. Nisubiri kwa muda wa siku saba hadi nije kwako na nikuoneshe unachopaswa kufanya.”
9 Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile.
Sauli alipotega mgongo amuache Samweli, Mungu akampa moyo mwingine. Ndipo ishara zote hizi zikatimia siku hiyo.
10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao.
Walipofika mlimani, kundi la manabii lilikutana naye, na Roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu ili atabiri pamoja nao.
11 Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”
Kila mtu aliyemfahamu kabla hajamwona akitabiri pamoja na manabii, watu waliambizana wao kwa wao:”Kitu gani kimempata mtoto wa Kishi? Hivi Sauli ni mmoja wa manabii siku hizi?”
12 Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”
Mtu mmoja kutoka eneo hilo akajibu, “Na ni nani baba yao?” Kwa sababu ya jambo hili, ukawapo msemo, “Hivi Sauli naye ni mmoja wa manabii?”
13 Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alikwenda mahali pa juu.
Alipomaliza kutabiri, akafika mahali pa juu.
14 Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?” Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulikwenda kwa Samweli.”
Ndipo baba yake mdogo na akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Mlienda wapi?” Naye akamjibu, “Kuwatafuta punnda; tulipoona kwamba hatuwezi kuwapata, tukaenda kwa Samweli.”
15 Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.”
Baba yake mdogo akasema, “Tafadhali niambie kile alichosema kwako Samweli,”
16 Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme.
Sauli akamjibu baba yake mdogo, “Alituambia waziwazi kwamba punda wamepatikana.” Lakini kuhusu swala la ufalme alilosema Samweli hakumwambia.
17 Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa Bwana huko Mispa,
Basi Samweli aliwaita watu pamoja huko Mispa.
18 naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowaonea.’
Akwaambia watu wa Israeli, “Hivi ndivyo BWANA, Mungu wa Israeli asemavyo: 'Niliwatoa Israeli kutoka Misri, na niliwaokoa kutoka nchi ya Wamisri, na kutoka mkono wa falme zote zilizowaonea.'
19 Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za Bwana kwa kabila zenu na kwa koo zenu.”
Lakini leo mmemkataa Mungu wenu, awaokoaye kutoka kwenye majanga na mahangaiko; na mmemwambia, ' Tuwekee mfalme juu yetu; Sasa jihudhurisheni wenyewe mbele za BWANA kwa kabila na jamaa zenu.”
20 Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa.
Kisha Samweli akawaleta kabila zote za Isareli karibu, na kulichagua kabila la Benyamini.
21 Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana.
Akawasogeza karibu kabila la Benyamini kwa kufuata jamaa zao; na jamaa ya Wamatri ikachaguliwa; na Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipokwenda kumtafuta, hakuweza kuonekana.
22 Wakazidi kuuliza kwa Bwana, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?” Naye Bwana akasema, “Ndiyo, amejificha katikati ya mizigo.”
Kisha watu walitaka kumuuliza Mungu maswali zaidi, “Bado yupo mtu mwingine ajaye?” BWANA akajibu, “Yeye mwenyewe kajificha kwenye mizigo.”
23 Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama katikati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote.
Wakaenda mbio na kumleta Sauli kutoka humo. Aliposimama kati yao, alikuwa mrefu kuliko watu wote kuanzia mabega yake kwenda juu.
24 Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye Bwana amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.” Ndipo watu wakapiga kelele, wakasema, “Mfalme na aishi maisha marefu.”
Kisha Samweli akawaambia watu, “Je, mnamuona mtu ambaye BWANA amemchagua? Hakuna mtu kama yeye kati ya watu wote.” Watu wote wakapiga Kelele, “Mfalme na aishi”
25 Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kuweka mbele za Bwana. Kisha Samweli akawaruhusu watu, kila mmoja aende nyumbani kwake.
Ndipo Samweli akawaambia watu desturi na sheria za ufalme, akaziandika katika kitabu, na kuziweke mbele za BWANA. Baadaye Samweli akawaruhusu watu waondoke kila mtu aende nyumbani kwake.
26 Sauli pia akaenda nyumbani kwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao.
Sauli pia alienda nyumbani kwake huko Gibea, akiwa na baadhi ya watu wenye nguvu, wenye mioyo iliyoguswa na Mungu.
27 Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akanyamaza kimya.
Lakini baadhi ya watu wasiofaa walisema, “Huyu mtu atatuokoaje?” Watu hawa walimdharau Sauli na hawakumletea zawadi zozote. Lakini Sauli alinyamaza kimya.

< 1 Samweli 10 >