< 1 Petro 1 >
1 Petro, mtume wa Yesu Kristo: Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia.
Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo nawaandikia ninyi wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia.
2 Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utiifu kwa Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake: Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.
Mungu Baba aliwateua ninyi kufuatana na kusudi lake, na mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu yake. Nawatakieni neema na amani tele.
3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu,
Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Ametujalia tumaini lenye uzima,
4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,
na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza au kuharibika au kufifia.
5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho.
Hizo zitakuwa zenu ninyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati.
6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi.
Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka.
7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa.
Shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu ambayo ni ya thamani zaidi kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima Siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.
8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka.
Ninyi mnampenda ingawaje hamjamwona, na mnamwamini ingawa hamumwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka,
9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.
kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu.
10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa,
Manabii walipeleleza kwa makini na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo ninyi mngepewa.
11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata.
Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata.
12 Walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.
Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo ninyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.
13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa.
Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa kwa nia, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika baraka ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana!
14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga.
Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga.
15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote.
Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu.
16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni.
Mnapomtaja Mungu ninyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu.
18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu,
Maana mnajua kwamba ninyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu, si kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha na dhahabu;
19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa.
bali mlikombolewa kwa damu tukufu ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwana kondoo asiye na dosari wala doa.
20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.
Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.
21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.
Kwa njia yake, ninyi mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu.
22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni.
Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, ninyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote.
23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. (aiōn )
Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, ninyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele. (aiōn )
24 Maana, “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao ni kama maua ya kondeni; majani hunyauka na maua huanguka,
Kama Maandiko yasemavyo: “Kila binadamu ni kama nyasi, na utukufu wake wote ni kama maua ya porini. Nyasi hunyauka na maua huanguka.
25 lakini neno la Bwana ladumu milele.” Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu. (aiōn )
Lakini neno la Bwana hudumu milele.” Neno hilo ni hiyo Habari Njema iliyohubiriwa kwenu. (aiōn )