< 1 Petro 4 >
1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi.
Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi.
2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu.
Tangu sasa, basi, maisha yaliowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, si na tamaa za kibinadamu.
3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu.
Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu.
4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi.
Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni.
5 Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.
Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu wazima na wafu!
6 Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.
Kwa sababu hiyo, hao waliokufa ambao walikuwa wamehukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama anavyohukumiwa kila mmoja, walihubiriwa Habari Njema kusudi katika maisha yao ya kiroho waishi kama aishivyo Mungu.
7 Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na akili tulivu na kiasi, mkikesha katika kuomba.
Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na nidhamu, ili mweze kusali.
8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.
Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi.
9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko.
Muwe na ukarimu ninyi kwa ninyi bila kunung'unika.
10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile uwakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu.
11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen. (aiōn )
Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumika anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina. (aiōn )
12 Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata.
Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida.
13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili mweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.
14 Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu.
Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu.
15 Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine.
Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni muuaji, mwizi, mhalifu au mwovu.
16 Lakini kama ukiteseka kwa kuwa Mkristo, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo.
Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo.
17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?
Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu?
18 Basi, “Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka, itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?”
Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?”
19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.
Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.