< 1 Wafalme 22 >
1 Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli.
Miaka mitatu ilipita bila kuwepo na vita kati ya Washami na Wisraeli.
2 Lakini katika mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme wa Yuda akashuka kwenda kumwona mfalme wa Israeli.
Ikawa katika mwaka wa tatu, Yehoshafati mfalme wa Israeli akashuka kwa mfalme wa Isreli.
3 Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?”
Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia watumishi wake, “Je, mnajua kuwa Ramothi Gileadi ni yetu, ila hatufanyi chochote kuitwaa kutoka kwenye mkono wa mfalme wa Shamu?”
4 Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
Kwa hiyo akamwambia Yehoshafati, “Je, utakwenda na mimi katika vita huko Ramothi Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, na farasi wangu ni kama farasi wako.”
5 Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri la Bwana.”
Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, “Tafadhali tafuta mwongozo kutoka neno la BWANA juu ya kile unachopaswa kufanya kwanza.”
6 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?” Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”
Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii pamoja, walikuwa wanaume elfu nne, akawaambia, “Je, niende Ramothi Gileadi kupigana, au nisiende?” Nao wakamwambia, “Ivamie, kwa kuwa Bwana ataitoa katika mkono wa mfalme.”
7 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Bwana hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”
Lakini Yehoshafati akasema, “Je, hapa hayupo nabii mwingine wa BWANA ambaye tunaweza kupata ushauri?”
8 Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri la Bwana, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.” Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”
Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Bado kuna mtu mmoja ambaye tunaweza kupata ushauri toka kwa BWANA ili kusaidia, Makaya mwana wa Imla, lakini namchukia kwa sababu huwa hanitabirii mazuri yanayonihusu, ila hunitabiria matatizo tu.” Lakini Yehoshafat akasema, “mfalme na asiseme hivyo,”
9 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”
Kisha mfalme wa Israeli akmwita akida na akamwamuru, “Kamlete Makaya mwana wa Imla, sasa hivi.”
10 Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao.
Wakati huo Ahabu mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi kila mmoja kwenye kiti cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika eneo la wazi kwenye lango la kuingilia Samaria, na manabii walikuwa wakiwatabiria.
11 Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’”
Sedekia mwana wa Kenaana akajitengenezea pembe za chuma akasema, “BWANA asema hivi: 'Kwa hili utawasukuma Washami mpaka watakapoisha.'”
12 Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Bwana ataitia mkononi mwa mfalme.”
Na manabii wengine wote wakasema hivyo, wakisema, “Ishambulie Ramothi Gileadi na ushinde, kwa kuwa BWANA ameiweka kwenye mkono wa mfalme.”
13 Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”
Yule mjumbe aliyeenda kumwita Makaya akamwambia, akisema, “Tazama sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja wanatabiri mambo mema kwa mfalme. Tafadhali maneno yako yawe kama yao ukaseme mambo mazuri.”
14 Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo, nitamwambia kile tu Bwana atakachoniambia.”
Makaya akajibu, “Kama BWANA aishivyo, kile BWANA atakachosema kwangu ndicho nitakachosema.'”
15 Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa Bwana atawatia mkononi mwa mfalme.”
Naye alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, “Makaya, je twende Ramothi Gileadi kupigana, au tusiende?” Makaya akamjibu, “Ivamie na ushinde. BWANA ataitoa kwenye mkono wa mfalme.”
16 Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Bwana?”
Kisha mfalme akamwambia. “Je, nikutake mara ngapi ili kuniapia ukweli kwa jna la BWANA?”
17 Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’”
Makaya akasema, “Ninaiona Israeli yote imesambaa kwenye milima, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, na BWANA amesema, 'Hawa hawana mchungaji. Kila mtu na arudi nyumbani kwake kwa amani.'”
18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, bali mabaya tu?”
Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Je sikukwambia kuwa huwa hanitabirii mambo mema yanayonihusu, ila majanga tu?”
19 Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Bwana: Nilimwona Bwana ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto.
Kisha Makaya akasema, “Kwa hiyo sikiliza neno la BWANA: Nimemwona BWANA akiwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi, na majeshi yote ya mbinguni yalikuwa yamesimama karibu yake upande wake wa kulia na upande wake wa kushoto.
20 Naye Bwana akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’ “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
BWANA akasema, 'Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili kwamba apande akafie Ramothi Gileadi? Na mtu mmoja akajibu kwa njia hii, na mwingine akajbu kwa njia ile.
21 Mwishoni, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Bwana na kusema, ‘Nitamshawishi.’
Ndipo pepo moja akajitokeza, akasimama mbele ya BWANA, akasema, 'Mimi nitamdanganya.' BWANA akmwuliza, 'Kwa jinsi gani?'
22 “Bwana akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “Bwana akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’
Yule pepo akamjibu, 'Nitakwenda na kuwa roho idanganyayo katika vinywa vya manabii wake,' BWANA akamjibu, 'utaweza kumdanganya, na utafanikiwa. Nenda sasa ukafanye hivyo.'
23 “Kwa hiyo sasa Bwana ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Bwana ameamuru maafa kwa ajili yako.”
Tazama sasa, BWANA ameweka roho idangayo kwenye vinywa vya hawa manabii wako, na BWANA ametangaza janga kwako.”
24 Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Bwana alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”
Kisha Sedekia mwana wa Kenaana, akaja, akamzabua Makaya shavuni, akasema, “Je, yule roho wa Bwana alitokaje kwangu ili asema na wewe?”
25 Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”
Makaya akasema, “Tazama, “utatambua hilo katika siku hiyo, utakapokimbilia katika chumba cha ndani kujificha.”
26 Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme.
Mfalme wa Israeli akamwambia mtumishi wake, “Mkamate Makaya umpeleke kwa Amoni, liwali wa mji, na kwa mwanangu, Yoashi.
27 Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’”
Mwambie, 'mfalme anasema mweke huyo gerezani na awe anampa mkate kidogo na maji kidogo, mpaka nitakaporudi salama.'”
28 Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Bwana hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”
Naye Makaya akasema, “Kama utarudi salama basi BWANA hajasema kupitia kinywa changu.” Na akaongeza, “Sikilizeni hili, ninyi watu.”
29 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi.
Ahabu, mfalme wa Israeli, na Yehoshafati mfalme wa Yuda, wamepanda Ramothi Gileadi.
30 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.
Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitajibadilisha mwenyewe niende vitani, lakini wewe uvae vazi lako la kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na akaenda vitani.
31 Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.”
Naye mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru majemedari thelathini na mbili wa magari yake, akisema, “Msimwamgamize askari wa muhimu au ambaye si wa muhimu, badala yake mshambulieni mfalme wa Israeli tu.”
32 Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele,
Ikawa wakati majemedari wa magari walipomwona Yehoshafati wakasema, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Wakageuka ili kumshambulia, kwahiyo Yehoshafati akapiga kelele.
33 wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, nao wakaacha kumfuatilia.
Ikawa majemedari wa magari walipoona kuwa yeye hakuwa mfalme wa Israeli, wakamwacha.
34 Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.”
Lakini mtu mmoja akavuta upinde wake kwa kubahatisha na akampiga mfalme wa Israeli katikati ya mwunganiko wa mavazi yake ya chuma. Ahabu akamawambia dereva wa gari lake, “geuza unirudishe kutoka vitani, kwa kuwa nimeumizwa sana.”
35 Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa.
Vita ikawa mbaya sana siku hiyo na mfalme akalazwazwa garini mwake akiwakabili Washami. Akafa jioni hiyo. Damu ilimwagika kutoka kwenye jeraha lake ndani ya gari.
36 Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!”
Ikawa wakati wa kuzama jua, kilio kikatawala kwa jeshi lote, wakisema, “Kila mtu arudi kwenye mji wake; na kila mtu arudi kwenye mkoa wake!”
37 Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko.
Kwa hiyo mfalme Ahabu akafa na akaletwa Samaria, wakamzika huko Samaria.
38 Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limesema.
Wakaliosha lile gari kwenye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake (hapa ni mahali ambapo makahaba waliogea), kama vile neno la BWANA lilivyokuwa limesema.
39 Kwa matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea maboma, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Kwa mambo mengine yanayohusisana na Ahabu, yote ambayo alifanya, ile nyumba ya pembe aliyojenga, na miji yote aliyojenga, je, hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio cha wafalme wa Israeli?
40 Ahabu akalala pamoja na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.
Kwa hiyo Ahabu akalala pamoja na mababu zake, na Ahaziya mwanae akawa mfalme mahali pake.
41 Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.
Kisha Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.
42 Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na mitano. Jina la mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi.
Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano alipoanza kutawala, na akatawala Yerusalemu kwa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba, binti wa Shilhi.
43 Katika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakwenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
Akatembea katika njia za Asa, baba yake, hakuziacha; akafanya yaliyokuwa mema mbele ya macho ya BWANA. Lakini bado mahali pa juu palikuwa hapajabomolewa. Watu walikuwa bado wanaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba mahali pa juu.
44 Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli.
Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli.
45 Kwa habari ya matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, mafanikio aliyokuwa nayo na uhodari wake katika vita, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
Kwa mambo mengine kuhusiana na Yehoshafati, na nguvu zake alizoonyesha, na jinsi alivyopigana vita, je, hayajaandikwa katika kitabu cha matukio cha wafalme wa Israeli?
46 Aliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa kuabudia miungu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa.
Aliwaondoa kutoka katka nchi wale makahaba wa kipagani waliokuwa wamebaki katika siku za baba yake Asa.
47 Tangu hapo hapakuwepo na mfalme katika Edomu, naibu ndiye alitawala.
Hapakuwepo mfalme katika Edomu isipokuwa kaimu mtawala.
48 Wakati huu Yehoshafati akaunda merikebu nyingi za biashara ili kwenda Ofiri kuchukua dhahabu, lakini kamwe hazikusafiri, kwa maana zilivunjika huko Esion-Geberi.
Yehoshafati alijenga merikebu: ziende Tarshishi na Ofri kuleta dhahabu, lakini hazikusafiri kwa sababu zile merikebu zilivunjika kule Esioni Geberi. Kisha
49 Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa.
Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Naomba watumishi wangu waende pamoja na watumishi wako merikebuni. “Lakini Yehoshafati hakuruhusu hilo.
50 Kisha Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Mwanawe Yehoramu akawa mfalme baada yake.
Yehoshafati akalala na mababu zake na akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi, babu yake; Yoramu mwanawe akawa mfalme mahali pake.
51 Ahazia mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye alitawala katika Israeli kwa miaka miwili.
Ahazia mwana Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli ya Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa mfalme Yehoshafati mfalme wa Yuda, na akatawala kwa mika miwili juu ya Israeli.
52 Akafanya maovu machoni mwa Bwana kwa sababu alienenda katika njia za baba yake na mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli itende dhambi.
Naye akafanya yaliyo maovu mbele ya macho ya BWANA akatembea katika njia za baba yake, katika njia za mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwazo aliifanya Israeli kufanya dhambi.
53 Alimtumikia na kumwabudu Baali na kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
Alimtumikia Baali na kumwabudu na kwa hiyo akamghadhabisha BWANA, Mungu wa Israeli, katika hasira, kama vile baba yake alivyofanya.