< 1 Wafalme 20 >
1 Wakati huu, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira kwa jeshi Samaria na kuishambulia.
Beni Hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote pamoja. Kulikuwa na wafalme thelathini na mbili wasaidizi pamoja naye, na magari na farasi. Akapanda, akaihusuru Samaria na kupigana nayo.
2 Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi:
Akatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, akamwambia, “Beni Hadadi anasema hivi:
3 ‘Fedha yako na dhahabu ni yangu, nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’”
Fedha zako na dhahabu zako ni zangu. Pia wake zako na watoto, wale wazuri, sasa ni wangu.”
4 Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”
Mfalme wa Israeli akajibu akasema, “Na iwe kama unavyosema, bwana wangu, mfalme. Mimi pamoja na vile nilivyo navyo ni mali yako.”
5 Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimetuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako.
Wale wajumbe wakaja tena wakasema, “Beni Hadadi anasema hivi, 'Nilituma neno kwako nikisema kwamba lazima ukabidhi kwangu fedha zako, dhahabu zako, wake zako na watoto wako.
6 Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’”
Lakini kesho nitatuma watumishi wangu kwako wakati kama huu, nao wataichunguza nyumba yako na nyumba za watumishi wako. Nao watatia mikononi mwao na kukichukua kila wakipendacho machoni mwao.'”
7 Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi na akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochokoza! Wakati alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”
Ndipo mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi pamoja akawaambia, ''Hebu angalieni jinsi huyu mtu anavyotafuta matatizo. Amenitumia ujumbe kwamba anataka kuchukua wake zangu, watoto wangu, fedha na dhahabu zangu, nami sijamkatalia.”
8 Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”
Wazee wote na watu wote wakamwambia Ahabu, “Usimsikilize wala kukubaliana na matakwa yake.”
9 Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.
Ahabu akawaambia wajumbe wa Beni Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme kwamba, 'Ninakubaliana na kila kitu ambacho kwanza uliwatuma watumishi wako kufanya kwangu, lakini sikubaliani na matakwa yako haya ya pili.'” Wale watumishi wa Beni Hadadi wakaondoka wakampelekea mrejesho Beni Hadadi.
10 Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema “Miungu iniletee maafa, tena makubwa zaidi, ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wafuatanao nami.”
Naye Beni Hadadi akatuma tena majibu yake kwa Ahabu, akaisema, “basi miungu inifanyie hivyo na zaidi, kama hata mavumbi ya Samaria yatawatosheleza watu watu wote wanaonifuata kuchukua kila mmoja angalau konzi mkononi mwake.”
11 Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’”
Naye mfalme wa Israeli akamjibu akisema, “Mwabieni Beni Hadadi, 'Hakuna abebaye silaha yake, atakayejivuna kama wakati wa kuishusha.”'
12 Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati ambapo yeye na wafalme walikuwa wanakunywa katika mahema yao, na akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kuushambulia mji.
Beni Hadadi aliusikia ujumbe huu wakati alipokuwa akinywa, yeye na wafalme walikuwa pamoja naye waliokuwa kwenye mahema yao. Beni Hadadi akayaamuru majaeshi yake, “Jipangeni katika sehemu zenu kwa ajili ya vita.” Kwa hiyo wakajiandaa kivita ili kuuvamia mji.
13 Wakati ule ule nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe ndipo utajua kwamba mimi ndimi Bwana.’”
Tazama, nabii akaja kwa Ahabu mfalme wa Israeli akasema, “BWANA asema, 'Je umeliona hili jeshi kubwa? Tazama, nitaliweka katika mkono wako leo, nawe utatambua kuwa mimi ni BWANA.'”
14 Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?” Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’” Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?” Nabii akamjibu, “Ni wewe.”
Naye Ahabu akajibu, ''kwa nani? BWANA akamjibu akasema, “kwa kuwatumia viijana wanaotumikia maliwali wa wilaya.” kisha Ahabu akasema, “Ni nani atakayepewa hiyo vita?' BWANA akamwambia, “wewe.”
15 Kwa hiyo Ahabu akawaita maafisa vijana majemadari wa majimbo, wanaume 232. Kisha akawakusanya Waisraeli wote waliobaki, jumla yao 7,000.
Ndipo Ahabu alipowataarifu wale vijna wanaowatumikia maliwali wa wilaya. Idadi yao ilikuwa 232. Baada yao aliwahesabu wanajeshi wote, jeshi lote la Israeli; idadi yao ilikuwa elfu saba.
16 Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa.
Nao wakatoka wakati wa adhuhuri. Naye Beni Hadadi alikuwa akinywa na kulewa hemani mwake, yeye na wale wafalme wadogo thelathini na mbili waliokuwa wakimsaidia.
17 Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza. Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”
Wale maakida vijana waliokuwa wakiwasaidia maliwali wa wilaya walitangulia kwanza. Kisha Beni Hadadi alitaarifiwa na wanaskauti aliokuwa amewatuma kwamaba, “kuna watu wanakuja kutoka Samaria.”
18 Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”
Beni Hadadi akasema, “wawe wamekuja kwa amani au kwa vita, wakamteni wakiwa hai.”
19 Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao,
Kwa hiyo wale vijvana wanaowatumikia maliwali wa wilaya wakaenda mjini na jeshi likawafuata kwa nyuma.
20 kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akatoroka akiwa amepanda farasi wake pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake.
Kila mmoja akaua adui wake na wale washami wakakimbia. Israeli ikawashinda. Beni Hadadi mfalme wa Shamu akatoroka kwa farasi pamoja na wapanda farasi.
21 Mfalme wa Israeli akasonga mbele na kushinda farasi na magari ya vita na kusababisha hasara kubwa kwa Waaramu.
Kisha mfalme wa Israeli akaenda akawashambulia farasi na magari, na kuwaua washami kwa mauaji makubwa.
22 Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja kukushambulia tena.”
Yule nabii akaja kwa mfalme wa Israeli akamwambia, “Nenda, ukajiimarishe mwenyewe, uelewa na kupanga kile unachofanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Shamu atapanda dhidi yako tena.”
23 Wakati ule ule, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini kama tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda.
Wale watumishi wa mfalme wa Shamu wakamwambia, “Mungu wao ni mungu wa milimani. Hiyo ndiyo sababu walikuwa na nguvu kuliko tulivyokuwa. Lakini sasa hebu tupigane nao katika nchi tambarare, na kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.
24 Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote thelathini na wawili kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao.
Na ufanye hivi: waondoe wafalme; mwondoe kila mmoja mahali pake ukaweke majemedari mahali pao.
25 Ni lazima pia uandae jeshi jingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.
Kisha ujihesabie jeshi kama lile jeshi ulilopoteza, farasi kwa farasi na gari kwa gari, nasi tutapigana nao katika nchi tambarare. Kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko walivyo.” Kwa hiyo Beni Hadadi akausikiliza ushauri huo naye akafanya kama alivyoshauriwa.
26 Mwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu mpaka Afeki kupigana dhidi ya Israeli.
Baada ya mwanzo wa mwaka mpya, Beni Hadadi akawahesabu Washami na akapanda Afeki kupigana na Israeli.
27 Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walikwenda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, wakati Waaramu walienea katika nchi yote.
Watu wa Israeli walikuwa wamehesabiwa na walikuwa wamejipanga kupigana nao. Watu wa Israeli wakafanya kambi mbele yao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, lakini Washami wakaujaza upande wa nchi.
28 Mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo: ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiri Bwana ni Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitatia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimi Bwana.’”
Ndipo mtu wa Mungu akaja karibu akaongea mfalme wa Israeli akamwambia, “BWANA anasema: 'Kwa kuwa Washami wamesema kuwa BWANA ni mungu wa milima, na wala si mungu wa mabondeni, nitaliweka hili jeshi kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ni BWANA.'”
29 Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu 100,000 kwa siku moja.
Kwa hiyo majeshi yakaweka kambi yakikabiliana kwa muda wa siku saba. Kisha siku ya saba vita vikaanza. Watu wa Israeli wakawaua Washami 100, 000 wanajeshi wa ardhini kwa siku moja.
30 Waliobaki wakatorokea katika mji wa Afeki, mahali ambapo watu 27,000 waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi akakimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.
Waliobaki wakakimbilia Afeki, mjini, na ule ukuta ukaanguka juu ya watu ishiriinina saba elfu waliobaki. Naye Beni Hadadi akakimbilia mjini. akaingia kwenye chumba cha ndani.
31 Maafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa nguo za gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”
Wale watumishi wa Beni Hadadi wakamwambia, “Tazama sasa, tumesikia kwamba wale wafalme wa nyumba ya Israeli ni wenye rehema. Tafadhali hebu tuvaeni magaunia viunoni mwetu na kamba vichwani mwetu, na twendeni kwa mfalme wa Israeli. Labda atakuokoa roho yako.”
32 Wakiwa wamevaa nguo za gunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, walikwenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’” Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”
Kwa hiyo wakavaa magunia viunoni mwao na kujifunga kamba vichwani mwao na kisha wakaenda kwa mfalme wa Israeli wakamwambia, “Mtumishi wako Beni Hadadi, anasema, 'tafadhali niachie uhai wangu.” Ahabu akawaambia, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”
33 Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!” Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita. Ben-Hadadi akajitolea, akisema,
Sasa wale watu walikuwa wakisikiliza ishara yeyote kutoka kwa Ahabu, kwa hiyo wakamjibu haraka, “Ndiyo ndugu yako Beni Hadadi bado yuko hai.” Ahabu akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ndipo Beni Hadadi alipokuja kwake, na Ahabu akamwacha aje kwenye gari lake.
34 “Nitairudisha ile miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Unaweza kuweka maeneo yako ya soko katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya huko Samaria.” Ahabu akasema, “Katika misingi ya mkataba, nitakuachilia huru.” Kwa hiyo akaweka mkataba naye, akamruhusu aende zake.
Beni Hadadi akamwambia Ahabu, “Nitakurudishia miji yako ambayo baba yangu alichukua toka kwa baba yako, na unaweza kutengeneza masoko kwa ajili yako Dameski, kama baba yangu alivyofanya kule Samaria.” Ahabu akajibu, “Nitakuacha uende kwa agano hili.” Kwa hiyo Ahabu akafanya agano naye kisha akamwacha aende.
35 Kwa neno la Bwana, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.
Mtu mmoja, mmoja wana wa wana wa manabii, akamwambia mmoja wa wale manabii wenzake kwa neno la BWANA, “Tafadhali nipige.” Lakini yule mtu akakataa kumpiga.
36 Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Bwana, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.
Kisha yule nabii akamwambia nabii mwenzake, “Kwa sababu umekataa kutii sauti ya BWANA, mara tu utakaponiacha, simba atakuua.” na mara tu baad ya yule mtu kumwacha, simba akamkuta na kumwua.
37 Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige tafadhali.” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi.
Kisha yule nabii akamkuta mtu mwingine akamwambia, “Tafadhali nipige.”Yule mtu akampiga na kumwumiza.
38 Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho.
Kisha yule nabii akaondoka akaenda kumsubiri yule mfalme barabarani; naye alikuwa amejibadilisha kwa kilemba machoni pake.
39 Mfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alikwenda vitani wakati vita vilipopamba moto, mtu mmoja akanijia na mateka akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Kama akitoroka itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama vipande 3,000 vya fedha.’
Ikawa mfalme alipokuwa akipita, Yule nabii akamwita mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako alienda katikati ya pigano, na askari akasimama akamleta adui kwangu akasema, 'Mwangalie mtu huyu. Na ikiwa kwa vyovyote atatoroka, basi maisha yako yatatolewa kwa ajili ya maisha yake vinginevyo utalipa kilo thelathini za fedha.
40 Wakati mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.” Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”
Lakini kwa kuwa mtumishi wako alikuwa na mambo mengi akienda huku na kule, yule askari adui akatoroka.” Basi mfalme wa Israeli akamwambia, Hivyo ndivyo itakavyokuwa hukukmu yako - umejihukumu mwenyewe.”
41 Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii.
Ndipo yule nabii alipoondoa haraka kile kilemba machoni pake, na mfalme wa Israeli alipotambua kuwa huyo alikuwa mmoja wa manabii.
42 Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo: ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hiyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’”
Yule nabii akamwambia mfalme, “BWANA anasema, 'Kwa sababu umemwachia aende mtu yule niliyekuwa nimemhukumu kifo, maisha yako yatachukua nafasi ya maisha yake.'”
43 Kwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake la kifalme huko Samaria.
Kwa hiyo mfalme wa Israeli akaenda nyumbani kwake akiwa na moyo mzito na mwenye hasira, akafika Samaria.