< 1 Wafalme 18 >
1 Baada ya muda mrefu, katika mwaka wa tatu, neno la Bwana likamjia Eliya kusema, “Nenda ukajionyeshe kwa Ahabu na mimi nitanyesha mvua juu ya nchi.”
Kwa hiyo baada ya siku nyingi neno la BWANA likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu wa ukame, likisema, “Nenda ukajionyeshe mwenyewe kwa Ahabu nami nitainyeshea ardhi mvua.”
2 Kwa hiyo Eliya akaenda kujionyesha kwa Ahabu. Wakati huu njaa ilikuwa kali sana katika Samaria,
Eliya akaenda kujionyesha mwenyewe kwa Ahabu; sasa njaa ilikuwa kali sana kule Samaria.
3 naye Ahabu alikuwa amemwita Obadia ambaye alikuwa msimamizi wa jumba lake la kifalme. (Obadia alimcha Bwana sana.
Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa mkuu wa ikulu. Obadia alimheshimu sana BWANA,
4 Wakati Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Bwana, Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja na akawa akiwapa chakula na maji.)
kwa kuwa wakati Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa BWANA, Obadia alichukua manabii mia akawaficha katika makundi ya hamsini hamsini katika pango na akawalisha kwa mikate na maji.
5 Ahabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu wapate kuishi ili tusilazimike kuwaua hata mmoja wa wanyama wetu.”
Ahabu akamwambia Obadia, “Pita katika nchi yote na katika chemichemi zote za maji na vijito. Yamkini tunaweza kupata maji na nyasi ili tuwaokoa hawa farasi na nyumbu, ili tusiwakose wanyama wote.”
6 Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.
Kwa hiyo wakaigawa nchi kati yao ili wapite kati yake wakitafuta maji. Ahabu akaenda njia yake mwenyewe na Obadia naye akaenda njia yake.
7 Wakati Obadia alipokuwa akitembea njiani, Eliya akakutana naye. Obadia akamtambua, akamsujudia hadi nchi na kusema, “Je, hivi kweli ni wewe, bwana wangu Eliya?”
Wakati Obadia akiwa njiani, akakutana na Eliya pasipo kutegemea. Obadia akamtambua na akalala kifudifudi chini. Akamwambia, “Ndiye wewe, bwana wangu Eliya?”
8 Eliya akamjibu, “Ndiyo, nenda ukamwambie bwana wako Ahabu, ‘Eliya yuko hapa.’”
Naye Eliya akamjibu, Ni mimi. Nenda umwambie bwana wako, 'Tazama, Eliya yuko hapa.'”
9 Obadia akamuuliza, “Ni kosa gani nimefanya, hata ukaamua kumkabidhi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu ili aniue?
Obadia akamjibu. “Nimekoseaje, kwamba umtoe mtumishi wako katika mkono wa Ahabu ili aniue?
10 Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, hakuna taifa hata moja au ufalme ambapo bwana wangu hajamtuma mtu kukutafuta. Kila wakati taifa au ufalme walipodai kwamba haupo huko, aliwafanya waape kwamba hawakuweza kukupata.
Kama BWANA Mungu wako aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambapo bwana wangu hajatuma watu kukutafuta. Kila taifa au ufalme unaposema, “Eliya hayuko hapa,' Ahabu hufanya waape ni kweli hawajakuona.
11 Lakini sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kusema, ‘Eliya yuko hapa.’
Na sasa wewe unasema, 'Nenda, ukamwambie bwana wako kwamba Eliya yuko hapa.'
12 Sijui ni wapi Roho wa Bwana ataamua kukupeleka wakati nitakapokuacha. Kama nikienda kumwambia Ahabu na asikupate, ataniua. Hata hivyo mimi mtumishi wako nimemwabudu Bwana tangu ujana wangu.
Mara tu baada ya kukuacha Roho wa BWANA atakuchukua na kukupeleka mahali ambapo sitapajua. Kisha nikienda na kumwambia Ahabu, na asipokuona, ataniua. Bado, mimi, mtumishi wako, nimekuwa nikimwabudu BWANA kutoka ujana wangu.
13 Je, hukusikia, bwana wangu, nilifanya nini wakati Yezebeli alipokuwa akiua manabii wa Bwana? Niliwaficha manabii wa Bwana mia moja katika mapango mawili, hamsini katika kila moja, nami nikawapatia chakula na maji.
Je, haujaambiwa, bwana wangu, nilichokifanya wakati Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA, jinsi nilivyowaficha wale manabii mia moja wa BWANA katika makundi ya hamsini kwenye pango na kuwalisha kwa mikate na maji?
14 Nawe sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kumwambia, ‘Eliya yuko hapa.’ Yeye ataniua!”
Na sasa unasema, 'Nenda umwambie bwana wako kwamba Eliya yuko hapa,' kwa hiyo ataniua.”
15 Eliya akasema, “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote aishivyo, yeye ninayemtumikia, hakika nitajionyesha kwa Ahabu leo.”
Ndipo Eliya alipomjibu, “Kama vile BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye mimi ninasimama, Kwa hakika nitajionyeshakwa Ahabu leo.”
16 Basi Obadia akaenda kukutana na Ahabu na kumwambia, naye Ahabu akaenda kukutana na Eliya.
Kwa hiyo Obadia akaenda kukutana na Ahabu, nakumwambia kile Eliya alichokuwa amemwambia. Ndipo mfalme alipoenda kukutana na Eliya.
17 Ahabu alipomwona Eliya, akamwambia, “Je, ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”
Ahabu alipomwona Eliya, akamwambia, “Je, ni wewe? Wewe mtabishaji wa Israeli!”
18 Eliya akamjibu, “Mimi sijaitaabisha Israeli. Lakini wewe na jamaa ya baba yako ndio mnaofanya hivyo. Mmeziacha amri za Bwana na mkafuata Mabaali.
Eliya akamwambia, “Mimi sijaitabisha Israeli, Lakiini wewe na familia ya baba yako ndio watabishaji kwa kuziacha amri za BWANA na kufuata sanamu za Baali.
19 Sasa waite watu kutoka Israeli yote tukutane nao juu ya Mlima Karmeli. Nawe uwalete hao manabii wa Baali mia nne na hamsini na hao manabii mia nne wa Ashera, walao chakula mezani mwa Yezebeli.”
Kwa hiyo sasa, Tuma neno na unikusanyie Israeli yote katika mlima Kameli, pamoja na manabii 450 wa Baali na wale manabii 400 wa Ashera wanaokula kwenye meza ya Yezebeli.”
20 Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya mlima Karmeli.
Kwa hiyo Ahabu akatuma neno kwa watu wote wa Israeli na akawakusanya manabii wote kwenye mlima Kameli.
21 Eliya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtasitasita katika mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Bwana ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.” Lakini watu hawakusema kitu.
Eliya akaja karibu na watu wote akasema, “Mtaendelea kubadilisha mawazo yenu mpaka lini? Kama BWANA ni Mungu, mfuateni yeye, Lakini kama Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye,” Lakini watu hawakumjibu neno.
22 Kisha Eliya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Bwana aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini.
Kisha Eliya akawaambia wale watu, “Mimi, pekee yangu, ndiye niliyebaki kuwa nabii wa BWANA, lakini manabii wa Baali wako 450.
23 Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na waweke juu ya kuni lakini wasiiwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni lakini sitawasha moto.
Hebu tutoleeni ng'ombe wawili. Nao wajichagulie ng'ombe mmoja na wamchinje na kumkatakata katika vipnde, na wamweke kwenye kuni, na wasitie moto chini yake. Nami nitamwandaa yule wa pili na kumweke juu ya kuni nami sitatia moto chini yake.
24 Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Bwana Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”
Kisha mtaliita jina la mungu wenu, nami nitaliita jina la BWANA, na Mungu atakayejibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Watu wote wakajibu na kusema, “Hilo ni jambo jema.”
25 Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
Kwa Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni ng'ombe mmoja kwa ajili yenu na mwe wa kwanza kumwamdaa, kwa kuwa ninyi ni wengi, Kisha liiteni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
26 Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa. Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.
Nao wakamchukua yule ng'ombe waliokuwa wamepewa na wakamwandaa, na ndipo walipoliita jina la Baali kuanzia asubuhi hadi adhuhuri, wakisema, “Baali, tusikie.” Lakini hapakuwepo na Sauti, na wala hakuna aliyejibu. Wakachezacheza kuizunguka madhabahu waliyotengeneza.
27 Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.”
Ilipofika adhuhuri Eliya akawakejeli akisema, “Mwiteni kwa nguvu! Huyo ni mungu! labda anawaza kitu, au amepumzika, au yuko safarini, au pengine amelala sharti aamshwe.”
28 Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika.
Kwa hiyo wakamwita kwa nguvu, wakajikatakata kama kawaida yao ilivyokuwa, kwa upanga na nyembe, mpaka damu ikawachuruzika.
29 Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na jibu, hakuna aliyejibu, hakuna aliyeangalia.
Ikawa wakati wa adhuhuri ulipopita, na bado walikuwa wakiendelea kutabiri mpaka wakati wa jioni wa kutoa dhabihu, lakini hapakuwepo na sauti wala mtu wa kuwajibu; wala hapakuwepo na yeyote wa kujibu wala wa kuangalia.
30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya Bwana, ambayo ilikuwa imevunjwa.
Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Nisogeleeni,” na watu wote wakamsogelea. Naye akatengeneza ile madhabahu ya BWANA ambayo ilikuwa imeharibika.
31 Eliya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.”
Eliya akachukua mawe kumi na mawili, kila jiwe moja liliwakilisha kabila moja la wana wa Yakobo - ni kupitia Yakobo kwamba neno la BWANA lilikuja, likisema, “Jina lako litakuwa Israel.”
32 Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Bwana, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu.
Kwa kutumia hayo mawe aliijenga ile madhabahu kwa jina la BWANA na akachimba mfereji kuizunguka ile madhabahu kubwa kiasi cha kubeba lita kumi na tano za maji.
33 Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”
Kisha akaweka kuni kwa ajili ya moto na akamkatakata yule ng'ombe katika vipande vipande na akaweka vile vipande juu ya kuni. Na akasema, “Vijazeni maji hivyo vyombo na yamwageni kwenye hiyo sadaka ya kueketezwa na juu ya hizo kuni.”
34 Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena. Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu.
Akasema tena fanyeni hivyo mara ya pili,” nao wakafanya kwa mara ya pili. kisha akasema, “Fanyeni mara ya tatu,” nao wakafanya kwa mara ya tatu.
35 Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.
Maji yakaizunguka ile madhabahu na kuujaza ule mfereji.
36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
Ikawa wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea na akasema, “BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu wa Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako, na kwamba nimeyafanya mambo haya yote kwa jina lako.
37 Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”
Nisikie, BWANA, nisike, ili hawa watu wajue kuwa wewe, BWANA, ndiye Mungu, na kwamba umeirudisha mioyo yao kwako tena.”
38 Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.
Ndipo moto wa BWANA ukashuka ukairamba ile sadaka, pamoja na zile kuni, mawe na mavumbi, na kuyaramba yale maji yaliyokuwa kwenye ule mfereji.
39 Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana: yeye ndiye Mungu! Bwana: yeye ndiye Mungu!”
watu wote walipoona haya, wakalala kifudifudi chini wakasema, “BWANA, ndiye Mungu! BWANA ndiye Mungu!
40 Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.
Kwa hiyo Eliya akawaambia, “Wakamateni manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja wao atoroke.” Kwa hiyo wakawakamata, na Eliya akawaleta manabii wa Baali chini kwenye kijito cha Kishoni na akawaua huko.
41 Eliya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.”
Eliya akamwambia Ahabu, “Inuka, ule na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.”
42 Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Eliya akapanda kileleni mwa Karmeli, akasujudu na akaweka kichwa chake katikati ya magoti yake.
Kwa hiyo Ahabu akaenda akala na knywa. Kisha Eliya akaenda juu ya mlima Kameli, akasudu chini na akaweka uso wake katikati ya magoti.
43 Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama. Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.” Mara saba Eliya akasema, “Nenda tena.”
Akamwambia mtumishi wake, “Nenda sasa, utazame upande wa bahari.” mtumishi wake akaenda na akasema, “Hakuna kitu,” Eliya akamwambia, “Nenda tena, mpaka mara saba.”
44 Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.” Hivyo Eliya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.’”
Ile mara ya saba mtumishi wake akasema, “Tazama, kuna wingu linapanda kutoka baharini, ni dogo kama mkono wa mtu.” Eliya akamjibu, Nenda ukamwambie Ahabu, 'Andaa gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.'”
45 Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli.
Ikatokea baada ya muda mfupi mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, na kulikuwa na mvua kubwa. Ahabu akapanda gari akaenda zake Yezreeli,
46 Nguvu za Bwana zikamjia Eliya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi maingilio ya Yezreeli.
lakini mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Eliya. Akalikaza vazi lake kwa mshipi wake na akakimbia mbele ya Ahabu kwenye lango la Yezreeli.