< 1 Wafalme 14 >

1 Wakati ule Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua,
Wakati huo Abiya mwana wa Yeroboamu akawa mgonjwa sana.
2 naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya yuko huko, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme juu ya watu hawa.
Yeroboamu akamwambia mke wake, “amka ujibadilishe, ili wasikutambue kuwa wewe ndiye mke wangu, na uende Shilo, kwa sababu nabii Ahiya yuko huko, yeye ndiye aliyeninea mimi kuwa nitakuwa mfalme juu ya watu hawa.
3 Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.”
Uchukue mikate kumi, na kaki na mtungi wa asali, na uende kwa Ahiya. Naye atakuambia kitakachotokea kwa mtoto.”
4 Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama alivyosema mumewe, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo. Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake.
Mke wa Yeroboamu akafanya hivyo; akaenda Shilo mpaka kwenye nyumba ya Ahiya. Wakati huo Ahiya alikuwa hawezi kuona, kwa kuwa macho yake yalikuwa yameishiwa nguvu kwa sababu ya umri wake.
5 Lakini Bwana alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.”
BWANA akamwambia Ahiya, “Tazama mke wa Ahiya anakuja kutafuta kutaka ushauri toka kwako kuhusiana na mwanae, kwa kuwa ni mgonjwa. Mwambie hivi na hivi, kwa sababu atakapofika atajifanya kuwa ni mwanamke mwingine.”
6 Hivyo Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini kujibadilisha? Nimetumwa kwako nikiwa na habari mbaya.
Naye Ahiya aliposikia sauti za miguu yake alipokuwa akiukaribia mlango, akasema, “karibu, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa mtu mwingine? Nimetumwa kwako nikiwa na habaari mbaya.
7 Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya kiongozi juu ya watu wangu Israeli.
Nenda ukamwambia Yeroboamu kwamba BWANA, Mungu wa Israeli, anasema, 'Nilikuinua kutoka kati ya watu na kukufanya uwe kiongozi wa watu wangu Israeli.
8 Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu.
Niliugawa ufalme kutoka kwa Daudi na kukupa wewe, lakini bado hutaki kuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye alizishika amri zangu na kunifuata kwa moyo wake wote, na kufanya kilichokuwa sawa mbele ya macho yangu.
9 Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunitupa nyuma yako.
Badala yake, umefanya maovu, zaidi ya wote waliokutangulia. Umetengeneza miungu mingine, na umetengeneza sanamu za kuyeyushwa ili kunikasirisha na kunitupa nyuma yako.
10 “‘Kwa sababu ya hili, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu mpaka iteketee yote kama mtu achomaye kinyesi.
Kwa hiyo, tazama, Nitaleta majanga kwenye familia yako; Nitawatupilia mbali watoto wako wote wa kiume katika Israeli, kama ni mtumwa au ni huru, na nitaiondoa familia yako, kama mtu anayechoma mavi mpaka yaishe.
11 Mbwa watawala wale walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji na ndege wa angani watajilisha kwa wale watakaofia mashambani. Bwana amesema!’
Yeyote ambaye ni mwanafamilia yako atakayefia mjini ataliwa na mbwa, na yeyote atakayefia shamabani ataliwa na ndege wa angani, kwa kuwa Mimi BWANA, nimesema;
12 “Kukuhusu wewe, rudi nyumbani. Wakati utakapotia mguu katika mji wako, kijana atakufa.
Kwa hiyo inuka wewe mke wa Yeroboamu, na uende nyumbani kwako; na mguu wako utakapokanyaga mjini, yule mtoto wa Abiya atakufa.
13 Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Kwa sababu ni yeye pekee wa nyumba ya Yeroboamu atakayezikwa, kwa sababu ni yeye peke yake ndani ya nyumba ya Yeroboamu ambaye Bwana, Mungu wa Israeli, ameona kitu chema kwake.
Na Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Ni yeye pekee katika familia ya Abiya atakayepelekwa makaburini, kwa sababu ni yeye pekee yake kutoka kwenye nyumba ya Abiya, ambaye BWANA, Mungu wa Israeli alimwona kuwa ni mwema.
14 “Bwana atajiinulia mwenyewe mfalme juu ya Israeli ambaye ataikatilia mbali jamaa ya Yeroboamu. Siku ndiyo hii! Nini? Naam, hata sasa hivi.
Pia BWANA atainua mfalme katika Israeli ambaye ataifutilia mbali familia ya Yeroboamu katika siku hiyo. Leo ndiyo siku hiyo, sasa hivi.
15 Naye Bwana ataipiga Israeli, hata iwe kama unyasi unaosukwasukwa juu ya maji. Ataingʼoa Israeli kutoka nchi hii nzuri aliyowapa baba zao na kuwatawanya ngʼambo ya Mto Frati, kwa sababu wamemghadhibisha Bwana kwa kutengeneza nguzo za Ashera
Kwa kuwa BWANA ataishambulia Israeli kama vile majani yanavyotikiswa majini, na ataing'oa Israeli katika nchi hii njema ambayo aliwpa mababu. Atawatawanya hata ng'ambo ya Mto Frati, kwa sababu wamefanya nguzo za Ashera kumkasirisha BWANA.
16 Naye atawaacha Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu aliyoyatenda na kusababisha Israeli kuyatenda.”
Ataiacha Israeli kwa sababu ya dhambi ya Yeroboamu, dhambi ambazo ametenda, na kwa hizo ameifanya Israeli kufanya dhambi.
17 Kisha mke wa Yeroboamu akainuka, akaondoka kwenda Tirsa. Mara alipokanyaga kizingiti cha mlango, kijana akafa.
Kwa hiyo mke wa Yeroboamu akainuka na akaondoka na akaenda mpaka Tirza. Naye alipofika kizingitini kwa nyumba yake, yule mtoto akafa.
18 Wakamzika na Israeli yote ikamwombolezea, kama Bwana alivyokuwa amesema kupitia mtumishi wake, nabii Ahiya.
Isareli wote wakamzika na kumwombolezea, kama vile alivyokuwa ameambiwa kwa neno la BWANA ambalo amelisema kupitia mtumishi wake nabii Ahiya.
19 Matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, vita vyake na jinsi alivyotawala, vimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
Na kwa mambo mengine yanayOmhusu Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na jinsi alivyotawala, tazama yameandikwa katika kitabu cha matukio ya wafalme wa Israeli.
20 Yeroboamu akawatawala kwa miaka ishirini na miwili, kisha akalala na baba zake. Naye Nadabu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Yeroboamu alitawala kwa miaka ishirini na mbili naye akalala na babu zake, na Nadabu mwanawe akawa mfalme mahali pake.
21 Rehoboamu mwana wa Solomoni alikuwa mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua kutoka makabila yote ya Israeli ili apate kuliweka humo Jina lake. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni.
Sasa Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mtawala wa Yuda. Rehoboamu alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipokuwa mfalme, na akatawala kwa miaka kumi na saba kule Yerusalemu, mji ambao BWANA alikuwa ameuchagua kati ya makabila yote ya Israeli ili aweke jina lake kule. Jina la mama yake alikuwa Naama Mwamori.
22 Yuda wakatenda maovu machoni pa Bwana. Kwa dhambi walizotenda wakachochea hasira yake yenye wivu zaidi kuliko baba zao walivyofanya.
Yuda ikafanya yaliyo maovu mbele ya macho ya BWANA; wakamtia wivu kwa makosa yao, zaidi ya yote ambayo baba zao walikuwa wamefanya
23 Pia wakajijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu, mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kilichoinuka na kila mti uliotanda.
Kwa kuwa walijijengea wenyewe mahali pa juu, nguzo za mawe, na nguzo za Ashera katika kila mahali pa juu na katika kila mti wenye majani mabichi.
24 Walikuwepo hata wanaume mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu katika nchi; watu wakajiingiza katika kutenda machukizo ya mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
Pia kulikuwepo na ukahaba wa kipagani katika nchi. Walifanya machukizo yaleyale kama wa mataifa yale ambayo BWANA alikuwa amewafukuza kutoka kwa watu wa Israeli.
25 Katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu.
Ilitokea wakati wa mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu wakati Shishaki akiwa mfalme wa Misri, akaja kinyume na Yerusalemu.
26 Akachukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao zote za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza.
Akaichukua hazina iliyokuwa kwenye nyumba ya BWANA, na ile hazina iliyokuwa kwenye nyumba ya Mfalme. Akachukua kila kitu; Pia alizichukua zile ngao za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa ametengeneza.
27 Kwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme.
Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba mahali pake na akazikabidhi kwa wakuu wa walinzi, ambao walilinda malango ya kuingia kwa mfalme.
28 Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu la Bwana, walinzi walizichukua hizo ngao, na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.
Na ikawa kila mfalme alipoingia kwenye nyumba ya BWANA, wale walinzi walizibeba na baadaye walizirudisha katika chumba cha walinzi.
29 Kwa matukio mengine ya utawala wa Rehoboamu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
Lakini katika mambo mengine kuhusiana na Rehoboamu, na yote yale aliyofanya, je, hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Yuda?
30 Kulikuwa na vita vinavyoendelea kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.
Kulikuwa na mapigano yasiyokoma kati ya nyumba ya Rehoboamu na nyumba ya Yeroboamu.
31 Naye Rehoboamu akalala na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama, ambaye alikuwa Mwamoni. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.
Kwa hiyo Rehoboamu akalala na mababu zake naye akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi Jina la mama yake alikuwa Naama Mwamori. Abiya mwanawe akawa mfalme mahali pake

< 1 Wafalme 14 >