< 1 Wafalme 13 >

1 Kwa neno la Bwana, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka.
Mtu wa Mungu alikuja tokea Yuda kwa neno la BWANA kule Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa amesimama karibu na madhabahu ili kufukiza uvumba.
2 Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Bwana: “Ee madhabahu, madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu wale ambao wanatoa sadaka hapa sasa, nayo mifupa ya wanadamu itachomwa juu yako.’”
Akalia kinyume na zile madhabahu kwa neno la BWANA: “Ee madhabahu, madhabahu” hivi ndivyo asemavyo BWANA, 'Tazama, mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika familia ya Daudi, na juu yenu atawachinja makuhani ambao sasa wanafukiza uvumba mahali hapa pa juu kwa ajili yako. Juu yako watachoma mifupa ya watu.'”
3 Siku iyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Bwana aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”
Kisha mtu wa Mungu akatoa ishara siku hiyohiyo, akisema, “Hii ndiyo isharaya kwamba BWANA amesema: 'Tazama, madhabahu zitavuunjika, na majivu yaliyo juu yatamwagika.”
4 Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamate!” Lakini mkono aliokuwa ameunyoosha kumwelekea yule mtu ukasinyaa na kubaki hapo hapo, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha.
Naye mfalme aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, kwamba amelia kinyume cha zile madhabahu kule Betheli, Yeroboamu akanyosha mkono wake kutoka madhabahuni, akisema, “mkamateni.” Ndipo ule mkono aliokuwa ameunyosha dhidi ya mtu wa Mungu ukakauka, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha mwenyewe.
5 Pia, madhabahu yalipasuka na majivu yakamwagika sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.
Na ile madhabahu ikavunjika vipande vipande, na yale majivu yakamwagika kutoka madhabahuni, kama ilivyokuwa imefafanuliwa kuwa ndiyo ishara ya kwamba mtu wa Mungu alikuwa amepewa kwa neno la BWANA.
6 Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Bwana Mungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Bwana, nao mkono wa mfalme ukapona na kuwa kama ulivyokuwa hapo kwanza.
Mfalme Yeroboamu akajibu akimwambia mtu wa Mungu, “Msihi BWANA, Mungu wako akupe neema ili uniombee, ili kwamba mkono wangu urejee kwangu tena.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwomba BWANA, na mkono wa mfalme ukarejea katika hali yake tena, na ukawa kama ulivyokuwa mwanzoni.
7 Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”
Yule mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”
8 Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali zako, nisingekwenda pamoja na wewe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa.
Yule mtu wa Mungu akamwambia mfalme, “Hata kama utanipa nusu ya miliki yako. staende na wewe, wala sitakula au kunywa maji mahali hapa,
9 Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’”
kwa sababu BWANA ameniamuru kwa neno lake, 'hutakula mkate wala kunywa maji, wala kurudi kwa njia ulioijia.'”
10 Kwa hiyo akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia ile ambayo alikuwa ameijia Betheli.
Kwa hiyo mtu wa Mungu akaondoka na hakurudi nyumbani kwa njia aliyokuja nayo huko Betheli.
11 Basi kulikuwepo na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme.
Sasa kulikuwa na nabii mwingine mzee aliyekuwa akiishi Betheli, na mmoja wa wana wake akaja kumwambia mambo yote ambayo mtu wa Mungu amefanya siku hiyo kule Betheli. Wana wake wakamwambia pia maneno ambayo Yule mtu wa Mungu alimwambia mfalme.
12 Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonyesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita.
Baba yao akawaambia, “Alienda kwa njia gani?” Wale wanawe walikuwa wamemwona yule mtu wa Mungu kutoka Yuda njia aliyotumia kurudi.
13 Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda
Kwa hiyo akawaambia wanawe, “Nitandikeni punda.” Kwa hiyo wakamtandikia punda naye akampanda.
14 na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?” Akamjibu, “Mimi ndiye.”
Yule nabii mzee akamfuata yule mtu wa Mungu na akamkuta amekaa chini ya mti wa mwaloni; akamwambia, “Je, wewe ndiye mtu wa Mungu aliyetoka Yuda?” Naye akamjibu, “Mimi ndiye.”
15 Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi ule.”
Kisha yule nabii mzee akamwambia, “twende nyumbani kwangu ukale chakula.”
16 Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa.
Yule mtu wa Mungu akamjibu, “Siwezi kurudi na wewe wala kuingia ndani na wewe, tena sitakula chakula wala kunywa maji pamoja na wewe mahali hapa,
17 Nimeambiwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’”
kwa sababu niliamuriwa hivyo kwa neno la BWANA, 'Hautakula chakula wala kunywa maji kule, wala kurudi kwa njia utakayokuja nayo.'”
18 Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Bwana: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.)
Kwa hiyo yule nabii mzee akamwambia, “Mimi pia ni nabii kama ulivyo, na malaika amesema na mimi neno la BWANA, akisema, 'Mrudishe aje na wewe katika nyumba yako, ili aweze kula chakula na kunywa maji.'” Lakini alikuwa anamdanganya mtu wa Mungu.
19 Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.
Kwa hiyo yule mtu wa Mungu akarudi pamoja na yule nabii mzee na akala chakula nyumbani kwake na akanywa maji.
20 Wakati walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu.
Walipokuwa wamekaa mezani, neno la BWANA likamjia yule nabii aliyemrudisha,
21 Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Umeasi neno la Bwana na hukushika amri uliyopewa na Bwana Mungu wako,
naye akalia kwa mtu wa Mungu aliyetoka Yuda, akisema “BWANA anasema, 'Kwa kuwa umeshindwa kutii nenola BWANA na umeshindwa kuishika amri ya BWANA ambayo Mungu wako alikupa,
22 bali ulirudi na ukala mkate na kunywa maji mahali ambapo alikuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’”
bali umerudi na umekula chakula na kunywa maji mahali ambapo BWANA alikwambia usile chakula wala kunywa maji, basi mwili wako hautazikwa kwenye makaburi ya baba zako.'”
23 Wakati huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake.
Baada ya kula chakula na kunywa maji, Yule nabii akatandika punda wa mtu wa Mungu, yule mtu aliyerudi naye.
24 Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, yule punda wake na simba wakiwa wamesimama karibu yake.
Baada ya mtu wa Mungu kuondoka, akakutana na simba njiani na kumwua barabarani, na mwili wake uliachwa barabarani. Na yule punda akasimama pembeni yake, na yule simba naye akasimama pembeni ya ule mwili.
25 Baadhi ya watu waliopita pale waliona maiti imebwagwa pale chini, simba akiwa amesimama kando ya maiti, wakaenda na kutoa habari katika mji ambao nabii mzee aliishi.
Watu walipopita na kuuona ule mwili umeachwa barabarani, na yule simba akisimama karibu na ule mwili, walikuja wakaeleza habari hiyo mjini kule ambako yule nabii mzee aliishi.
26 Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu ambaye aliasi neno la Bwana. Bwana amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limemwonya.”
Yule nabii aliyemrudisha toka njiani aliposikia, akasema, “Yeye mtu wa Muugu ndiye aliyeshindwa kutii neno la BWANA. Kwa hiyo BWANA alimtoa kwa simba, ambaye amemrarua katika vipande vipande na kumwua, kama vile neno la BWANA lilivyokuwa limemwonya.”
27 Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo.
Kwa hiyo yule nabii mzee akawaamnbia wanawe, akisema, “Tandikeni punda wangu,” nao wakamtandikia.
28 Kisha akatoka akaenda akakuta maiti imebwagwa chini barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda.
Akaenda akaukuta mwili umeachwa barabarani, punda na simba wamesimama pembeni ya ule mwili. Yule simba hakuula ule mwili, wala hakumshambulia yule punda.
29 Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika.
Yule nabii akauchukua ule mwili wa mtu wa Mungu, akaulaza juu ya punda, na akaurudisha. Akaja kwenye mji wake kuomboleza na kuuzika.
30 Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”
Akaulaza mwili kwenye kaburi lake, nao wakamwombolezea, wakisema, “Aa! ndugu yangu!”
31 Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Wakati nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
Kisha baada ya kumzika, yule nabii mzee akawaambia wanawe, akasema, “Nitakapokufa, mtanizika kwenye kaburi ambalo tumemzika mtu wa Mungu. Mtalaza mifupa yangu pembeni mwa mifupa yake.
32 Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Bwana dhidi ya madhabahu huko Betheli na dhidi ya madhabahu yote katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Samaria, hakika yatatokea kweli.”
Kwa kuwa ule ujumbe uliosemwa na BWANA, dhidi ya madhabahu kule Betheli na dhidi ya nyumba zote za mahali pa juu katika mji wa Samaria, hakika yatatokea.
33 Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu.
Baada ya haya Yeroboamu hakuuacha uovu wake, aliendelea kuchagua makuhani wa kawaida kwa ajili ya mahali pa juu kutoka kwa watu wa kila aina. Yeyote ambaye angeweza kutumika alimtakasa kuwa kuhani.
34 Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.
Jambo hili likawa dhambi kwenye familia ya Yeroboamu na kusababisha familia yake kuangamizwa na kuondolewa kabisa katika uso wa dunia.

< 1 Wafalme 13 >