< 1 Wafalme 12 >
1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wamekwenda huko kumfanya yeye kuwa mfalme.
Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Israeli yote walikuwa wameenda Shekemu kumfanya awe mfalme.
2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Solomoni), akarudi kutoka Misri.
Ikatokea kuwa Yeroboamu mwana wa Nebati akayasikia haya (Kwa kuwa alikuwa bado yuko Misri, ambako alikuwa amekimbilia kumkwepa mfalme Sulemani), Kwani Yeroboamu alikuwa anaishi Misri.
3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu, yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia,
Kwa hiyo wakatuma watu kumwita, na Yeroboamu pamoja na mkutano wote wa Israeli wakaja wakamwambia Rehoboamu,
4 “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”
Baba yako aliifanya nira yetu kuwa nzito. Sasa ifanye kazi ngumu ya baba yako kuwa nyepesi kuliko nira ngumu ambayo baba yako alituwekea, nasi tutakutumikia.”
5 Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.
Naye Rehobiamu akawaambia, “Ondokeni kwa siku tatu, kisha nirudieni.” Kwa hiyo watu wakaondoka.
6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee ambao walimtumikia Solomoni baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri nini katika kuwajibu watu hawa?”
Mfalme Rehoboamu akatafuta ushauri kwa wazee waliokuwa wamesimama mbele ya Sulemani baba yake wakati wa uhai wake, naye akasema, “mnanishauri niwajibuje hawa watu?”
7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”
Nao wakamwambia, “Kama wewe utakuwa mtumishi wa hawa watu na akawatumikia, na akawapa majibu ya maneno mema, ndipo watakapokuwa watumishi wako daima.”
8 Lakini Rehoboamu akakataa shauri alilopewa na wazee na akataka ushauri kwa vijana wanaume rika lake waliokuwa wakimtumikia.
Lakini Rehoboamu akapuuzia ushauri aliopewa na wazee na akaenda kuomba ushauri kwa vijana ambao alikua pamoja nao wakasimama mbele yake.
9 Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu?’”
Akawaambia, “Mnanipa ushauri gani ili niweze kuwajibu hawa watu waliosema nami kwamba, 'ifanye nyepesi nira ambayo baba yako alituwekea'”
10 Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Waambie watu hawa waliokuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ kuwa, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
Wale vijana waliokua pamoja na Rehoboamu wakamjibu, wakisema, “Waambie hawa watu kuwa baba yako Sulemani aliifanya nira yenu kuwa nzito lakini ninyi wenyewe mnaweza kuifanya rahisi. Uwaambie hivi, 'Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
11 Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.’”
Kwa hiyo sasa, ingawa baba yangu aliwatwika kongwa zito, Mimi nitaiongeza kongwa lenu. Baba yangu aliwaadhibu kwa mijeredi, Lakini mimi nitawaadhibu kwa nge.'”
12 Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.”
Kwa hiyo siku ya tatu Yeroboamu na watu wote wakaja kwa Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amewaelekeza aliposema, “mrudi kwangu siku ya tatu.”
13 Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Akikataa shauri alilopewa na wazee,
Naye mfalme akawaambia wale watu kwa ukali na akapuuzia ushauri wa wale wazee ule waliokuwa wamempatia.
14 akafuata shauri la vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.”
Akawaambia akifuata ushauri wa wale vijana; akasema, “Baba yangu aliwatwika kongwa zito, lakini mimi nitaongeze kongwa lenu. Baba yangu aliwaadhibu kwa mijeredi, mimi nitawaadhibu kwa nge.”
15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili kutimiza neno ambalo Bwana alikuwa amenena kwa Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia Ahiya Mshiloni.
Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza wale watu, kwa kuwa ilikuwa zamu ya tukio lililoletwa na BWANA, ili kwamba aweze kulitimiza neno lake ambalo alikuwa amelisema kupitia Ahiya.
16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme: “Tuna fungu gani kwa Daudi? Sisi hatuna urithi kwa mwana wa Yese. Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli! Angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!” Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao.
Israeli yote ilipoona kuwa mfalme hakuwasikiliza, watu wakamjibu wakimwambia, “Je, tuna sehemu gani kwa Daudi? Hatuna urithi kwa mwana wa Yese! Nenda kwenye hema zako, ewe Israeli. Sasa tazama kwenye nyumba yako, Daudi.” Kwa hiyo Israeli akarudi kwenye hema zake.
17 Lakini kwa habari ya Waisraeli waliokuwa wakiishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.
Lakini kwa watu wa Israeli waliokuwa wakiishi kwenye miji ya Yuda, Rehoboamu akawa mfalme juu yao.
18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake na kutorokea Yerusalemu.
Kisha mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, lakini Waisraeli wote wakampiga kwa mawe wakamwua kwa mawe. Mflme Rehoboamu akakimbia haraka kwa gari lake kwenda Yerusalemu.
19 Hivyo Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.
Kwa hiyo Israeli wakawa wapinzani dhidi ya nyumba ya Daudi mpaka leo.
20 Waisraeli wote waliposikia kwamba Yeroboamu amerudi, wakatuma watu na kumwita kwenye kusanyiko na kumfanya mfalme juu ya Israeli yote. Ni kabila la Yuda peke yake lililobaki kuwa tiifu kwa nyumba ya Daudi.
Ndipo Israeli yote waliposikia kuwa Yeroboamu alikuwa amerudi, walimwita kwenye kusanyiko lao wakamweka kuwa mfalme wa Israeli. Hapakuwepo na mtu aliyeifuata familia ya Daudi, isipokuwa tu kabila la Yuda.
21 Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda na kabila la Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.
Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akawakusanya wote wa nyumba ya Yuda na kabila la Benjamini; walichaguliwa wanaume wanajeshi 180, 000 ili wapigane na nyumba ya Israeli, kwa lengo la kurudisha ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.
22 Lakini neno hili la Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu:
Lakini neno la Mungu likamjia Shemaya, mtu wa Mungu; likisema,
23 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, na nyumba yote ya Yuda na Benyamini, na watu wengine wote,
“Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na kwa nuymba yote ya Yuda na Benjamini, na kwa watu wote; uwaambie,
24 ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu, Waisraeli. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na kurudi nyumbani, kama Bwana alivyokuwa ameagiza.
“BWANA asema hivi, Usipigane wala kuwavamia ndugu zako watu wa Israeli. Kila mtu lazima arudi nyumbani kwake, kwa kuwa jambo hili nimelisababisha mimi.” Kwa hiyo wakalisikiliza neno la BWANA na wakrudi nyumbani kwa njia zao na wakalitii neno lake.
25 Kisha Yeroboamu akajenga Shekemu akaizungushia ngome katika nchi ya vilima ya Efraimu na akaishi huko. Akatoka huko, akaenda akajenga Penueli.
Kisha Yeroboamu akaijenga Shekemu katika nchi ya milima ya Efraimu, na akaishi huko. Akatoka huko na kuijenga Penueli.
26 Yeroboamu akawaza moyoni mwake, “Sasa inawezekana ufalme ukarudi katika nyumba ya Daudi.
Yeroboamu akafikiri moyoni mwake, “Sasa ufalme utarudi kwenye nyumba ya Daudi.
27 Kama watu hawa watapanda kwenda kutoa dhabihu katika Hekalu la Bwana huko Yerusalemu, mioyo yao itamrudia bwana wao, Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua mimi na kurudi kwa Mfalme Rehoboamu.”
Kama hawa watu wataenda kutoa sadaka kwenye hekalu la BWANA kule Yerusalemu, basi mioyo ya hawa watu itarudi tena kwa bwana wao, kwa Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua na kurudi kwa Rehoboamu mfalme wa Yuda.”
28 Baada ya kutafuta shauri, mfalme akatengeneza ndama wawili wa dhahabu. Akawaambia watu, “Ni gharama kubwa kwenu kukwea kwenda Yerusalemu. Hii hapa miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
Kwa hiyo mfalme Yeroboamu akatafuta ushauri na akafanya ndama wawili wa dhahabu; akawaambia watu, “Ni vigumu sana kwenu kwenda Yerusalemu. Tazameni, hawa ndiyo miungu yenu, Ee Israeli, iliyowatoa toka nchi ya Misri.”
29 Ndama mmoja akamweka Betheli na mwingine Dani.
Akamweka mmoja Betheli na mwingine Dani.
30 Nalo jambo hili likawa dhambi, watu wakawa wanaenda hadi Dani kumwabudu huyo aliyewekwa huko.
Kwa hiyo jambo hili likawa dhambi. Watu wakaenda kwa huyo na wengine kwa hawa, mpaka huko Dani.
31 Yeroboamu akajenga madhabahu mahali pa juu pa kuabudia miungu na kuwateua makuhani kutoka watu wa aina zote, ijapokuwa hawakuwa Walawi.
Yeroboamu akajenga nyumba mahali pa juu na kufanya makuhani kutoka kwa watu wote, ambao hawakuwa wana wa Lawi.
32 Pia Yeroboamu akaweka sikukuu katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, kama sikukuu iliyokuwa ikifanyika huko Yuda, na akatoa dhabihu juu ya madhabahu. Akafanya hivyo huko Betheli akitoa dhabihu kwa ndama alizotengeneza. Huko Betheli akawaweka makuhani, na pia katika sehemu za juu za kuabudia miungu alizozitengeneza.
Yeroboamu akafanya sikukuu katika mwezi wa nane, katika siku ya kumi na tano ya mwezi, kama sikukuu ambayo iko Yuda, na akaenda juu kwenye madhabahu. Akafanya hivyo kule Betheli, akawatolea sadaka wale ndama aliokuwa amewatengeneza, na akaweka kuhani huko Betheli mahali pa juu alipokuwa amepatengeneza.
33 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouchagua mwenyewe, alitoa dhabihu juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga huko Betheli. Kwa hiyo akaweka sikukuu kwa ajili ya Waisraeli na akapanda madhabahuni kutoa sadaka.
Yeroboamu akapanda kwenda kwenye madhabahu ambayo aliitengeneza kule Betheli katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, ndio mwezi aliokuwa amefikiri katika akili yake; akafanya sikukuu kwa watu wa Israeli n a akaenda madhabahuni kufukiza uvumba.