< 1 Wafalme 10 >
1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la Bwana, akaja kumjaribu kwa maswali magumu.
2 Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake.
3 Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea.
4 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,
5 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika hekalu la Bwana, alipatwa na mshangao.
6 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.
7 Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia.
8 Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako!
9 Ahimidiwe Bwana Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake Bwana wa milele ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”
10 Naye akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni.
11 (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani.
12 Mfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo ya Hekalu la Bwana na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa au kuonekana humo tangu siku ile.)
13 Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
14 Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666,
15 mbali na mapato kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Kiarabu na watawala wa nchi.
16 Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600
17 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
18 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.
19 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na egemeo la nyuma lilikuwa la mviringo kwa juu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
20 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote.
21 Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo siku za Solomoni.
22 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.
23 Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
24 Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake.
25 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.
26 Solomoni akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000, ambayo aliyaweka katika miji ya magari na mengine akawa nayo huko Yerusalemu.
27 Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani.
28 Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue.
29 Waliagiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha na farasi kwa shekeli 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.