< 1 Yohana 1 >

1 Tunawajulisha lile lililokuwepo tangu mwanzo, lile tulilosikia, ambalo tumeliona kwa macho yetu, ambalo tumelitazama na kuligusa kwa mikono yetu, kuhusu Neno la uzima.
Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe.
2 Uzima huo ulidhihirishwa; nasi tumeuona na kuushuhudia, nasi twawatangazia uzima wa milele, ambao ulikuwa pamoja na Baba, nao ukadhihirishwa kwetu. (aiōnios g166)
Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. (aiōnios g166)
3 Twawatangazia lile tuliloliona na kulisikia, ili nanyi mwe na ushirika nasi. Na ushirika wetu hasa ni pamoja na Baba na Mwanawe, Yesu Kristo.
Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo.
4 Tunaandika mambo haya ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.
Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike.
5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote.
Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake.
6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli.
Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo kwa maneno na matendo.
7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.
8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu.
Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu.
9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote.
Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote.
10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.
Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.

< 1 Yohana 1 >