< 1 Wakorintho 3 >
1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo.
Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo.
2 Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari.
Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari.
3 Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida?
Maana bado mu watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na magombano kati yenu? Mambo hayo yanaonyesha wazi kwamba ninyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia.
4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?
Mmoja wenu anaposema, “Mimi ni wa Paulo”, na mwingine, “Mimi ni wa Apolo”, je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu?
5 Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kupitia wao mliamini, kama vile Bwana alivyompa kila mtu huduma yake.
Apolo ni nani? na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu ambao tuliwaleteeni ninyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na Bwana.
6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliikuza.
Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini aliyeiotesha mbegu ni Mungu.
7 Hivyo mwenye kupanda na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ambaye huifanya ikue.
Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota.
8 Apandaye mbegu ana lengo sawa na yule atiaye maji na kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake.
Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa, ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe.
9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.
Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na ninyi ni shamba lake; ninyi ni jengo lake.
10 Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga.
Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga. Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake.
11 Kwa maana hakuna mtu yeyote awezaye kuweka msingi mwingine wowote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo.
Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo.
12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi,
Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi.
13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu.
Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana wakati Siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, Siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonyesha ubora wake.
14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake.
Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo;
15 Kama kazi kitateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.
lakini kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni.
16 Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
17 Kama mtu yeyote akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ndiyo hilo hekalu.
Basi, mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni takatifu, na hekalu hilo ni ninyi wenyewe.
18 Msijidanganye. Kama mtu yeyote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima. (aiōn )
Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli. (aiōn )
19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,”
Maana, hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao.”
20 tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.”
Na tena: “Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai.”
21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Vitu vyote ni vyenu,
Basi, mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu.
22 ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefa au dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu
Paulo, Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni yenu.
23 na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.
Lakini ninyi ni wa Kristo naye Kristo ni wa Mungu.