< 1 Wakorintho 16 >

1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo.
Sasa kuhusu michango kwa ajili ya waumini, kama nilivyo elekeza makanisa ya Galatia, vivyo hivyo mwapaswa kufanya.
2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.
Katika siku ya kwanza ya wiki, kila mmoja wenu aweke kitu fulani kando na kukihifadhi, kama muwezavyo. Fanyeni hivyo ili kwamba kusiwe na michango wakati nikija.
3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu.
Na nitakapofika, yeyote mtakayemchagua, nitamtuma pamoja na barua kutoa sadaka yenu huko Yerusalem.
4 Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
Na kama ni sahihi kwa mimi kwenda pia, watakwenda pamoja nami.
5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia.
Lakini nitakuja kwenu, wakati ninapitia Makedonia. Kwa kuwa nitapitia Makedonia.
6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo.
Labda naweza kukaa nanyi au hata kumaliza majira ya baridi, ili kwamba muweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendako.
7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda.
Kwa kuwa sitarajii kuwaona sasa kwa muda mfupi. Kwani ninatumaini kukaa nanyi kwa muda fulani, kama Bwana ataniruhusu.
8 Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste,
Lakini nitakaa Efeso mpaka Pentekoste,
9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
kwa kuwa mlango mpana umefunguliwa kwa ajili yangu, na kuna maadui wengi wanipingao.
10 Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo.
Sasa wakati Timotheo akija, muoneni kwamba yuko na ninyi pasipo kuogopa, anafanya kazi ya Bwana, kama ninavyofanya.
11 Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.
Mtu yeyote asimdharau. Mumsaidie katika njia yake kwa amani, ili kwamba aweze kuja kwangu. Kwa kuwa ninamtarajia aje pamoja na ndugu.
12 Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.
Sasa kuhusiana na ndugu yetu Apolo. Nilimtia moyo sana kuwatembelea ninyi pamoja na ndugu. Lakini aliamua kutokuja kwa sasa. Hata hivyo, atakuja wakati ana nafasi.
13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari.
Muwe macho, simameni imara, mtende kama wanaume, muwe na nguvu.
14 Fanyeni kila kitu katika upendo.
Basi yote myafanyayo yafanyike katika upendo.
15 Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi,
Mnaijua kaya ya Stefana. Mnajua kwamba walikuwa waamini wa kwanza huko Akaya, na kwamba walijiweka wenyewe kwenye huduma ya waumini. Na sasa nawasihi, kaka na dada zangu,
16 mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii.
kuweni wanyenyekevu kwa watu kama hao, na kwa kila mtu anayesaidia katika kazi na watenda kazi pamoja nasi.
17 Nilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu.
Na ninafurahi kwa ujio wa Stefana, Fotunato, na Akiko. Wamesimama mahali ambapo ninyi mgepaswa kuwa.
18 Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.
Kwa kuwa wameifurahisha roho yangu na yenu. Kwa hiyo sasa, watambueni watu kama hawa.
19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana.
Makanisa ya Asia wametuma salamu kwenu. Akila na Priska wanawasalimu katika Bwana, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao.
20 Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
Kaka na dada zangu wote wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
21 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.
Mimi, Paulo, naandika hivi kwa mkono wangu.
22 Kama mtu yeyote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo.
Kama yeyote hampendi Bwana, basi laana iwe juu yake. Bwana wetu, njoo!
23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.
Upendo wangu uwe pamoja nanyi katika Kristo Yesu.

< 1 Wakorintho 16 >