< 1 Wakorintho 12 >

1 Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu.
Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya:
2 Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au ingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena.
Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu.
3 Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu.
Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: “Yesu alaaniwe!” Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: “Yesu ni Bwana,” asipoongozwa na Roho Mtakatifu.
4 Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule.
Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja.
5 Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule.
Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja.
6 Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.
Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote.
7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote.
Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote.
8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo.
Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu apendavyo Roho huyohuyo.
9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja.
Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya;
10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha.
humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua.
11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.
Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe.
12 Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo.
Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote—ingawaje ni vingi—hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo.
13 Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.
14 Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi.
Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi.
15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili.
Kama mguu ungejisemea: “Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili”, je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha!
16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili.
Kama sikio lingejisemea: “Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili”, je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La!
17 Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi?
Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa?
18 Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda.
Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda.
19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
20 Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.
Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja.
21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!”
Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: “Sikuhitaji wewe”, wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: “Siwahitaji ninyi.”
22 Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana.
Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi.
23 Navyo vile viungo tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee;
Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi,
24 wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa,
ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima,
25 ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake.
ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote vishughulikiane.
26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.
Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho.
27 Sasa ninyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja wenu ni sehemu ya huo mwili.
Basi, ninyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo.
28 Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, aina mbalimbali za lugha.
Mungu ameweka katika kanisa: kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya, kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni.
29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza?
Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza?
30 Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri?
Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha?
31 Basi tamanini sana karama zilizo kuu. Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.
Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonyesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote.

< 1 Wakorintho 12 >