< 1 Nyakati 16 >
1 Wakaleta Sanduku la Mungu na kuliweka ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, na wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu.
2 Baada ya Daudi kumaliza kutoa hizo sadaka za kuteketezwa na hizo sadaka za amani, akawabariki watu katika jina la Bwana.
3 Kisha akamgawia kila Mwisraeli mwanaume na mwanamke mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu.
4 Akawaweka pia baadhi ya Walawi ili wahudumu mbele ya Sanduku la Bwana kufanya maombi, kumshukuru na kumsifu Bwana, Mungu wa Israeli:
5 Asafu ndiye alikuwa mkuu wao, akisaidiwa na Zekaria, Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Matithia, Eliabu, Benaya, Obed-Edomu na Yeieli. Hawa ndio wangepiga zeze na vinubi, Asafu angepiga matoazi,
6 nao Benaya na Yahazieli makuhani, ndio wangepiga tarumbeta mara kwa mara mbele ya Sanduku la Agano la Mungu.
7 Siku ile, kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa Bwana:
8 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake; wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
9 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa; waambieni matendo yake yote ya ajabu.
10 Lishangilieni jina lake takatifu; mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.
11 Mtafuteni Bwana na nguvu zake; utafuteni uso wake siku zote.
12 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka,
13 enyi wazao wa Israeli mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
14 Yeye ndiye Bwana Mungu wetu; hukumu zake zimo duniani pote.
15 Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
16 agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki.
17 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele:
18 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.”
19 Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake,
20 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
21 Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
22 “Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.”
23 Mwimbieni Bwana dunia yote; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
24 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
25 Kwa kuwa Bwana ni mkuu, mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
26 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Bwana aliziumba mbingu.
27 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
28 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa, mpeni Bwana utukufu na nguvu,
29 mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake. Leteni sadaka na mje katika nyua zake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.
30 Dunia yote na itetemeke mbele zake! Ulimwengu ameuweka imara; hauwezi kusogezwa.
31 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; semeni katikati ya mataifa, “Bwana anatawala!”
32 Bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake; mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo ndani yake.
33 Kisha miti ya msituni itaimba, itaimba kwa furaha mbele za Bwana, kwa maana anakuja kuihukumu dunia.
34 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele.
35 Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe. Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.”
36 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni Bwana.”
37 Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la Bwana ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku.
38 Pia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango.
39 Daudi akamwacha kuhani Sadoki pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema ya ibada ya Bwana katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni
40 ili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Bwana kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika sheria ya Bwana ambayo alikuwa amempa Israeli.
41 Waliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa Bwana shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.”
42 Hemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni.
43 Kisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani kwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.