< Zekaria 9 >

1 Hili ni tamko la neno la Yahwe kuhusu nchi ya Hadraki na Damesiki. Kwa maana jicho la Yahwe liko juu ya wanadamu wote, na juu ya kabila zote za Israeli pia.
Neno: Neno la Bwana liko kinyume na nchi ya Hadraki na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika, kwa kuwa macho ya watu na ya kabila zote za Israeli yako kwa Bwana,
2 Azimio hili pia linaihusu Hamathi, inayopakana na Damesiki, na linahusu Tiro na Sidoni, japokuwa ni werevu sana.
pia juu ya Hamathi inayopakana nayo, juu ya Tiro na Sidoni, ingawa wana ujuzi mwingi sana.
3 Tiro amejijengea ngome na kurundika fedha kama mavumbi na dhahabu safi kama matope mitaani.
Tiro amejijengea ngome imara, amelundika fedha kama mavumbi na dhahabu kama taka za mitaani.
4 Tazama! Bwana atamnyang'anya na kuharibu nguvu zake juu ya bahari, kwa hiyo atateketezwa kwa moto.
Lakini Bwana atamwondolea mali zake na kuuangamiza uwezo wake wa baharini, naye atateketezwa kwa moto.
5 Ashikeloni ataona na kuogopa! Gaza pia atatemeka sana! Ekroni, tumanini lake litatikiswa! Mfalme ataangamizwa kuanzia Gaza, na Ashikeloni haitakuwa na watu tena!
Ashkeloni ataona hili na kuogopa; Gaza atagaagaa kwa maumivu makali, pia Ekroni, kwa sababu matumaini yake yatanyauka. Gaza atampoteza mfalme wake na Ashkeloni ataachwa pweke.
6 Wageni watafanya makao yao katika Ashidodi, nami nitakiondoa kiburi cha Wafilisiti.
Wageni watakalia mji wa Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
7 Kwani nitaondoa damu yao katika vinywa vyao na machukizo yao kutoka kati ya meno yao. Ndipo watakapokuwa masalia kwa Mungu wetu kama ukoo katika Yuda, na Ekironi atakuwa kama Wayebusi.
Nitaondoa damu vinywani mwao, chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao. Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu, nao watakuwa viongozi katika Yuda, naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi.
8 Nitaweka kambi kuzunguka nchi yangu kinyume cha majeshi ya adui hata hakuna atakayeweza kupita ndani yake tena, kwani hakuna mtesaji atakayeipita tena. Kwa kuwa sasa nitaangalia nchi yangu kwa macho yangu mwenyewe!
Lakini nitailinda nyumba yangu dhidi ya majeshi ya wanyangʼanyi. Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena, kwa maana sasa ninawachunga.
9 Piga kelele kwa furaha, ewe binti Sayuni! Piga kelele kwa shangwe, ewe binti Yerusalem! Tazama! Mfalme wako anakuja kwako pamoja na uadilifu na anakuokoa. Ni mnyenyekevu, amepanda punda, mwanapunda.
Shangilia sana, ee Binti Sayuni! Piga kelele, Binti Yerusalemu! Tazama, Mfalme wako anakuja kwako, ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mpole, naye amepanda punda, mwana-punda, mtoto wa punda.
10 Ndipo nitakapoondoa kibandawazi kutoka Efraimu na farasi kutoka Yerusalemu, na upinde utaondolewa katika vita; kwani atasema amani kwa mataifa, na utawala wake utakuwa kutoka bahari hata bahari, na kutoka katika mto hadi miisho ya dunia!
Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu na farasi wa vita kutoka Yerusalemu, nao upinde wa vita utavunjwa. Atatangaza amani kwa mataifa. Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari, na kutoka Mto Frati hadi mwisho wa dunia.
11 Lakini kwenu, kwa sababu ya damu ya agano langu nanyi, nitawaweka wafungwa wenu huru kutoka shimoni pasipo na maji.
Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya Agano langu nawe, nitawaacha huru wafungwa wako watoke kwenye shimo lisilo na maji.
12 Rudini ngomeni, wafungwa wa matumaini! Hata leo natamka kwamba nitawarudishia mara mbili, kwani nimempinda Yuda kama upinde wangu.
Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata sasa ninatangaza kwamba nitawarejesheeni maradufu.
13 Hata nimelijaza podo langu pamoja na Efraimu. Nimewainua wana wenu, Sayuni, kinyume cha wana wenu, Ugiriki, na amekufanya wewe, Sayuni, kama upanga wa shujaa!
Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu, nitamfanya Efraimu mshale wangu. Nitawainua wana wako, ee Sayuni, dhidi ya wana wako, ee Uyunani, na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.
14 Yahwe atawatokea, na mishale yake itapiga kama radi! Kwa maana Yahwe Bwana wangu atapiga tarumbeta naye ataendelea pamoja na dhoruba kutoka Temani.
Kisha Bwana atawatokea; mshale wake utamulika kama umeme wa radi. Bwana Mwenyezi atapiga tarumbeta, naye atatembea katika tufani za kusini,
15 Yahwe wa majeshi atawatetea, nao watawararua na kuyashinda mawe ya kombeo. Ndipo watakapo kunywa na kupiga kelele kama mtu aliyelewa kwa mvunyo, nao watajazwa na mvinyo kama mabakuri, kama pembe za madhabahu.
na Bwana Mwenye Nguvu Zote atawalinda. Wataangamiza na kushinda kwa mawe ya kutupa kwa kombeo. Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo; watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia kwenye pembe za madhabahu.
16 Hivyo Yahwe Mungu wao atawaokoa siku hiyo; watakuwa kama kundi la kondoo lililo na watu wake, kwani watakuwa mapambo ya taji, yaliyoinuliwa juu ya nchi yake.
Bwana Mungu wao atawaokoa siku hiyo kama kundi la watu wake. Watangʼara katika nchi yake kama vito vya thamani kwenye taji.
17 Jinsi gani watakavyokuwa wazuri na warembo! vijana watastawi juu ya nafaka na bikra juu ya divai tamu!
Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri! Nafaka itawastawisha vijana wanaume, nayo divai mpya vijana wanawake.

< Zekaria 9 >