< Zaburi 27 >

1 Yahwe ni nuru yangu na wokovu wangu; nimuogope nani? Yahwe ni salama ya maisha yangu; ni mhofu nani?
Zaburi ya Daudi. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani?
2 Wakati waovu waliponijia kunila mwili wangu, wapinzani wangu na adui zangu walijikwaa na wakaanguka.
Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wanile nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka.
3 Ingawa jeshi hujipanga kupigana na mimi, moyo wangu hautaogopa; japo vita vijapo inuka kupigana nami hata hapo nitabaki kuwa jasiri.
Hata jeshi linizunguke pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri.
4 Kitu kimoja nimekiomba kwa Yahwe, nami nitakitafuta hicho: kwamba niweze kukaa katika nyumba ya Yahwe siku zote za maisha yangu, kuutazama uzuri wa Yahwe na kutafakari hekaruni mwake.
Jambo moja ninamwomba Bwana, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Bwana na kumtafuta hekaluni mwake.
5 Kwa kuwa katika siku ya shida atanificha nyumbani mwake; atanificha katika mfuniko wa hema lake. Yeye ataniinua juu ya mwamba!
Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema yake na kuniweka juu kwenye mwamba.
6 Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya maadui wote wanizungukao, nami nitatoa sadaka ya furaha hemani mwake! Nitaimba na kutunga nyimbo kwa Yahwe!
Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia Bwana na kumsifu.
7 Sikia, sauti yangu nikuitapo, Yahwe! Unihurumie, na unijibu!
Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana, unihurumie na unijibu.
8 Moyo wangu huongea kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Nami nautafuta uso wako, Yahwe!
Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, Bwana “Nitautafuta.”
9 Usiufiche uso wako mbali na mimi; usinikasirikie mimi mtumishi wako! Wewe umekuwa msaada wangu; usiniache wala kunitelekeza, Mungu wa wokovu wangu!
Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu.
10 Hata kama baba yangu na mama yangu wakiniacha, Yahwe utanitunza kwako.
Hata kama baba yangu na mama wakiniacha, Bwana atanipokea.
11 Unifundishe njia yako, Yahwe! Kwa sababu ya adui zangu uniongoze katika njia salama.
Nifundishe njia yako, Ee Bwana, niongoze katika njia iliyonyooka kwa sababu ya watesi wangu.
12 Usiwaache adui zangu wanifanyie watamanivyo, kwa sababu mashahidi wa uongo wameinuka kinyume namimi, nao wanapumua vurugu!
Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri.
13 Kitu gani kingeweza kunitokea kama nisingeamini kuwa nitauona uzuri wa Yahwe katika nchi ya walio hai?
Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai.
14 Umngoje Yahwe; uwe imara, na moyo wako uwe jasiri! Umngoje Yahwe!
Mngojee Bwana, uwe hodari na mwenye moyo mkuu, nawe, umngojee Bwana.

< Zaburi 27 >