< Zaburi 26 >
1 Unihukumu mimi, Yahwe, kwa kuwa nimeenenda katika uadilifu; nimeamini katika Yahwe bila kusita.
Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, nithibitishe katika haki, maana nimeishi maisha yasiyo na lawama; nimemtumainia Bwana bila kusitasita.
2 Unichunguze, Yahwe, na unijaribu; uujaribu usafi wa sehemu zangu za ndani na moyoni mwangu!
Ee Bwana, unijaribu, unipime, uuchunguze moyo wangu na mawazo yangu;
3 Kwa maana uaminifu wa agano lako uko mbele ya macho yangu, na mwenendo wangu ni katika uaminifu wako.
kwa maana upendo wako uko mbele yangu daima, nami natembea siku zote katika kweli yako.
4 Mimi sichangamani na watu waovu, wala sichangamani na watu wanafiki.
Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki,
5 Ninachukia waovu, na siishi na waovu.
ninachukia kusanyiko la watenda mabaya na ninakataa kuketi pamoja na waovu.
6 Ninaosha mikono yangu kounesha sina hatia, na kuikaribia madhabahu yako, Yahwe,
Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia, naikaribia madhabahu yako, Ee Bwana,
7 kuimba wimbo wa sauti ya sifa na kutoa taarifa ya matendo yako yote ya ajabu.
nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa, huku nikisimulia matendo yako ya ajabu.
8 Yahwe, ninaipenda nyumba ninayoishi, mahali ambapo utukufu wako unaishi!
Ee Bwana, naipenda nyumba yako mahali unakoishi, mahali ambapo utukufu wako hukaa.
9 Usiniangamize pamoja na wenye dhambi, au maisha yangu na watu wenye kiu ya kumwaga damu,
Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wamwagao damu,
10 ambao katika mikono yao kuna njama, na ambao mkono wa kuume umejaa rushwa.
ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa.
11 Lakini kwangu mimi, nitaenenda katika uadilifu; uniokoe na unihurumie.
Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama; nikomboe na unihurumie.
12 Miguu yangu husimama sehemu salama; katika kusanyiko la watu nitambariki Yahwe!
Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare; katika kusanyiko kuu nitamsifu Bwana.