< Zaburi 139 >

1 Ee Yahwe, wewe umenichunguza, na unanijua.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
2 Wewe unajua nikaapo na niinukapo; unayajua mawazo yangu tokea mbali sana.
Unajua ninapoketi na ninapoinuka; unatambua mawazo yangu tokea mbali.
3 Unachunguza wenendo wangu na kulala kwangu; unazijua njia zangu zote.
Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu; unaelewa njia zangu zote.
4 Kabla hakujawa na neno kwenye ulimi wangu, wewe unalijua kabisa, Yahwe.
Kabla neno halijafika katika ulimi wangu, wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana.
5 Nyuma yangu na mbele yangu unanizunguka na kuniwekea mkono wako.
Umenizunguka nyuma na mbele; umeweka mkono wako juu yangu.
6 Maarifa hayo ni mengi yananizidi mimi; yako juu sana, nami siwezi kuyafikia.
Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu, ni ya juu sana kwangu kuyafikia.
7 Niende wapi mbali na roho yako? Niende wapi niukimbie uwepo wako?
Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
8 Kama nikipaa mbinguni, uko huko; kama nikifanya kitanda changu Kuzimuni, tazama, uko huko. (Sheol h7585)
Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko. (Sheol h7585)
9 Kama nikipaa kwa mbawa za asubuhi na kwenda kuishi pande za mwisho wa bahari,
Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko, kama nikikaa pande za mbali za bahari,
10 hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika.
hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.
11 Kama nikisema, “Hakika giza litanifunika, na nuru inizungukayo itakuwa usiku,”
Kama nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,”
12 Hata giza lisingweza kuwa giza kwako. Usiku ungeng'aa kama mchana, maana giza na nuru kwako vinafanana.
hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utangʼaa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
13 Wewe uliumba sehemu zangu za ndani; uliniumba tumboni mwa mama yangu.
Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
14 Nitakusifu, kwa maana nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu. Nafsi yangu yalijua hili vizuri sana.
Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu.
15 Mifupa yangu haikusitirika kwako nilipoumbwa kwa siri, nilipoumbwa kwa ustadi pande za chini za nchi.
Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
16 Uliniona ndani ya tumbo; siku zote zilizo pangwa kwangu ziliandikwa kitabuni mwako hata kabla ya siku ya kwanza kutokea.
macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwepo hata moja.
17 Ni jinsi gani mawazo yako ni ya thamani kwangu, Mungu! Njinsi ilivyo kubwa jumla zake!
Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!
18 Kama nikijaribu kuyahesabu ni mengi kuliko mchanga. Niamkapo bado niko na wewe.
Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga. Niamkapo, bado niko pamoja nawe.
19 Ee Mungu, kama ungewaua waovu; ondokeni kwangu enyi watu wenye vurugu.
Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu! Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!
20 Wanakuasi wewe na kutenda udanganyifu; adui zako wananena uongo.
Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya, adui zako wanatumia vibaya jina lako.
21 Je, siwachukii hao, wale wakuchukiao Yahwe? Je, siwadharau wale wanao inuka dhidi yako?
Ee Bwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?
22 Nawachukia kabisa; wamekuwa adui zangu.
Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao, ninawahesabu ni adui zangu.
23 Ee Mungu, unichunguze na kuujua moyo wangu; unijaribu na uyajue mawazo yangu.
Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu.
24 Uone kama kuna njia ya uovu ndani yangu, na uniongoze katika njia ya milele.
Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele.

< Zaburi 139 >