< Mithali 24 >

1 Usiwe na husuda kwa wenye ubaya, wala usitamani kuambatana nao,
Usiwaonee wivu watu waovu, usitamani ushirika nao;
2 kwa sababu mioyo yao inapanga njama za vurugu na midomo ya huongea juu ya madhara.
kwa maana mioyo yao hupanga mambo ya jeuri, nayo midomo yao husema juu ya kuleta madhara.
3 Kwa hekima nyumba hujengwa na kwa ufahamu huimarishwa.
Kwa hekima nyumba hujengwa, nayo kwa njia ya ufahamu huimarishwa
4 Kwa maarifa vyumba hujazwa vitu vyote vya thamani na utajiri wa kupendeza.
kwa njia ya maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vya thamani na vya kupendeza.
5 Shujaa wa hekima ni imara, na mtu wa maarifa huongeza nguvu zake;
Mtu mwenye hekima ana uwezo mkubwa, naye mtu mwenye maarifa huongeza nguvu,
6 maana kwa uongozi wa busara unaweza kufanya vita na kwa washauri wengi kuna ushindi.
kwa kufanya vita unahitaji uongozi na kwa ushindi washauri wengi.
7 Hekima ipo juu sana kwa mpumbavu; hafumbui kinywa chake kwenye mlango.
Hekima i juu mno kwa mpumbavu, katika kusanyiko langoni hana lolote la kusema.
8 Kuna yule mwenye kupanga kufanya mabaya- watu wanamwita bwana wa njama.
Yeye apangaye mabaya atajulikana kama mtu wa hila.
9 Mipango ya mpumbavu ni dhambi na watu humchukia mwenye dhihaka.
Mipango ya upumbavu ni dhambi, watu huchukizwa na mwenye dhihaka.
10 Kama utakuwa dhaifu na mwenye kuogopa siku ya taabu, basi nguvu zako ni haba.
Ukikata tamaa wakati wa taabu, jinsi gani nguvu zako ni kidogo!
11 Waokoe wanaochukuliwa kwenda kwenye mauti na uwashikilie wale wanaopepesuka kwenda kwa mchinjaji.
Okoa wale wanaoongozwa kwenye kifo; wazuie wote wanaojikokota kuelekea machinjoni.
12 Kama utasema, “Tazama, hatujui chochote juu ya hili,” je yule anayepima mioyo hajui unachosema? Na yule anayelinda maisha yako, je hajui? Je Mungu hatampa kila mmoja kile anachostahili?
Kama mkisema, “Lakini hatukujua lolote kuhusu hili,” je, yule apimaye mioyo halitambui hili? Je, yule awalindaye maisha yenu halijui hili? Je, hatamlipa kila mtu kulingana na aliyotenda?
13 Mwanangu, kula asali kwa kuwa ni nzuri, kwa sababu matone ya sega la asali ni matamu unapoonja.
Ule asali mwanangu, kwa kuwa ni nzuri; asali kutoka kwenye sega ni tamu kwa kuonja.
14 Hekima ndiyo ilivyo katika nafsi yako - kama utaitafuta, tumaini lako halitabatilika na kutakuwa na tumaini.
Ujue pia kwamba hekima ni tamu kwa nafsi yako, kama ukiipata, kuna matumaini kwako ya siku zijazo, nalo tumaini lako halitakatiliwa mbali.
15 Usisubiri kwa kuvizia kama waovu ambao hushambulia nyumba ya mwenye haki. Usiiharibu nyumba yake!
Usivizie kama haramia afanyavyo ili kuyashambulia makao ya mwenye haki, wala usiyavamie makazi yake,
16 Maana mwenye haki huanguka mara saba na kuinuka tena, lakini waovu huangushwa kwa maafa.
Kwa maana ingawa mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena, lakini waovu huangushwa chini na maafa.
17 Usisherekee wakati adui yako anapoanguka na wala moyo wako usifurahi anapojikwaa,
Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo; wakati ajikwaapo, usiruhusu moyo wako ushangilie.
18 au Yehova ataona na kutoridhika na kuondoa ghadhabu juu yake.
Bwana asije akaona na kuchukia akaiondoa ghadhabu yake mbali naye.
19 Usifadhaike kwa sababu ya watenda mabaya, na wala usiwahusudu watu waovu,
Usikasirike kwa sababu ya watu wabaya wala usiwaonee wivu waovu,
20 maana mtu mbaya hana matumaini na taa ya watu waovu itazimika.
kwa maana mtu mbaya hana tumaini la siku zijazo, nayo taa ya waovu itazimwa.
21 Mwanangu; mche Yehova, na umwogope mfalme, usishirikiane na watu wenye kuasi dhidi yao,
Mwanangu, mche Bwana na mfalme, wala usijiunge na waasi,
22 maana kwa ghafula msiba wao utakuja na ni nani ajuaye ukubwa wa uharibifu utakao kuja kutoka kwa hao wote?
kwa maana hao wawili watatuma maangamizi ya ghafula juu yao, naye ni nani ajuaye maafa wawezayo kuleta?
23 Haya ni maneno ya wenye busara pia. Upendeleo katika kuhukumu kesi kwa sheria si vizuri.
Hii pia ni misemo ya wenye hekima: Kuonyesha upendeleo katika hukumu si vyema:
24 Anayemwambia mwenye hatia, “Wewe upo sawa,” atalaaniwa na watu na mataifa yatamchukia.
Yeyote amwambiaye mwenye hatia, “Wewe huna hatia,” Kabila zitamlaani na mataifa yatamkana.
25 Bali wenye kuwakemea waovu watakuwa na furaha na zawadi za wema zitakuja kwao.
Bali itakuwa vyema kwa wale watakaowatia hatiani wenye hatia, nazo baraka tele zitawajilia juu yao.
26 Anayetoa jibu la kweli hutoa busu kwenye midomo.
Jawabu la uaminifu ni kama busu la midomoni.
27 Andaa kazi yako ya nje, na tayarisha kila kitu kwa ajili yako mwenyewe shambani; baada ya hapo, jenga nyumba yako.
Maliza kazi zako za nje, nawe uweke mashamba yako tayari, baada ya hayo, jenga nyumba yako.
28 Usitoe ushahidi dhidi ya jirani yako bila sababu na usidanganye kwa midomo yako.
Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu, au kutumia midomo yako kudanganya.
29 Usiseme, “Mimi nitamtendea kile alichonitendea; nitalipiza kwa kile alichofanya.”
Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; nitamlipiza mtu yule kwa kile alichonitendea.”
30 Nilikwenda jirani na shamba la mtu mvivu, nikapita kwenye shamba la mzabibu la mtu asiye na akili.
Nilipita karibu na shamba la mvivu, karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,
31 Miiba imeota kila sehemu, ardhi ilikuwa imefunikwa kwa upupu, na ukuta wake wa mawe ulikuwa umebomoka.
miiba ilikuwa imeota kila mahali, ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.
32 Kisha nikaliona na kufikiria juu yake; nikatazama na kupokea mafundisho.
Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona, nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:
33 Kulala kidogo, kusinzia kidogo, kupumzika kwa kukunja mikono kidogo-
Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:
34 na umasikini huja kwa kutembea juu yako, na mahitaji yako kama askari mwenye silaha.
hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

< Mithali 24 >