< Mithali 21 >

1 Moyo wa mfalme ni mfereji wa maji katika mkono wa Yehova; anaugeuza popote anakopenda.
Moyo wa mfalme uko katika mkono wa Bwana; huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo.
2 Kila njia ya mtu ni sawa katika macho yake mwenyewe, lakini ni Yehova anayeipima mioyo.
Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake, bali Bwana huupima moyo.
3 Kutenda haki na adili hukubaliwa zaidi na Yehova kuliko sadaka.
Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika zaidi kwa Bwana kuliko dhabihu.
4 Macho ya kiburi na moyo wa majivuno- taa ya waovu- ni dhambi.
Macho ya kudharau na moyo wa kiburi, ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi!
5 Mipango ya mwenye juhudi huelekea kwenye mafanikio tu, bali kila mtu anayetenda kwa haraka huelekea umasikini.
Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.
6 Kujipatia utajiri kwa ulimi wa uongo ni mvuke unaopita upesi na mtego ambao unafisha.
Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.
7 Vurugu ya waovu itawaburuta mbali, maana wanakataa kutenda haki.
Jeuri ya waovu itawaburuta mbali, kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa.
8 Njia ya mwenye hatia ni ukatiri, bali mwenye usafi hutenda yaliyo ya haki.
Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu, bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu.
9 Bora kuishi kwenye kona ya juu darini kuliko katika nyumba pamoja na mke mgonvi.
Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
10 Hamu ya mwovu ni uchu wa mabaya; jirani yake haoni ukarimu katika macho yake.
Mtu mwovu hutamani sana ubaya, jirani yake hapati huruma kutoka kwake.
11 Mwenye dhihaka anapoadhibiwa mjinga hupata busara, na mtu mwenye busara anapofundishwa, anaongeza maarifa.
Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa, mjinga hupata hekima; wakati mtu mwenye hekima afundishwapo, hupata maarifa.
12 Atendaye haki huilinda nyumba ya mwovu; huwashusha waovu kwenye uharibifu.
Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu, naye atawaangamiza waovu.
13 Anayeziba masikio yake kwenye kilio cha masikini, pia atalia, lakini hatajibiwa.
Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini, yeye pia atalia, wala hatajibiwa.
14 Zawadi ya siri hutuliza hasira na zawadi ya kificho hutuliza ghadhabu kuu.
Zawadi itolewayo kwa siri hutuliza hasira na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali.
15 Haki ikitendeka, huleta furaha kwa mwenye kutenda wema, lakini huleta hofu kubwa kwa watenda mabaya.
Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki, bali kitisho kwa watenda mabaya.
16 Yule anayezurura kutoka kwenye njia ya ufahamu, atapumzika kwenye kusanyiko la wafu.
Mtu anayepotea kutoka mapito ya ufahamu, hupumzika katika kundi la waliokufa.
17 Anayependa raha atakuwa masikini; anayependa divai na mafuta hawezi kuwa tajiri.
Mtu apendaye anasa atakuwa maskini, yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.
18 Mtu mbaya ni fidia kwa yule atendaye haki, na mdanganyifu ni fidia kwa waaminifu.
Waovu huwa fidia kwa ajili ya wenye haki, nao wasio waaminifu kwa ajili ya wanyofu.
19 Bora kuishi jangwani kuliko kuishi pamoja na mwanamke ambaye huchochea sana ugomvi na malalamiko.
Ni afadhali kuishi jangwani kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi.
20 Hazina yenye thamani na mafuta vipo nyumbani kwa mwenye busara, bali mtu mpumbavu huviharibu.
Katika nyumba ya mwenye hekima kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta, lakini mtu mpumbavu hutafuna vyote alivyo navyo.
21 Mtu atendaye haki na mwema -huyu mtu hupata uzima, haki na heshima.
Yeye afuatiaye haki na upendo hupata uzima, mafanikio na heshima.
22 Mtu mwenye busara huupima mji wa mashujaa, na huiangusha ngome wanayoitumaini.
Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu, na kuangusha ngome wanazozitegemea.
23 Anayelinda kinywa chake na ulimi wake hujilinda mwenyewe na taabu.
Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake hujilinda na maafa.
24 Mtu mwenye kiburi na maringo- “Dhihaka” ndilo jina lake - hutenda kwa majivuno na kujidai.
Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake; hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi.
25 Shauku ya mtu mvivu itamuua, maana mikono yake hukataa kufanya kazi.
Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake, kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi.
26 Kwa siku nzima hupatwa na uchu na uchu zaidi, lakini atendaye haki hutoa na wala hazuii.
Mchana kutwa hutamani zaidi, lakini mnyofu hutoa pasipo kuzuia.
27 Sadaka ya mwovu ni chukizo; huwa ni chukizo zaidi anapoileta kwa nia mbaya.
Dhabihu ya mtu mwovu ni chukizo, si zaidi sana itolewapo kwa nia mbaya!
28 Shahidi wa uongo ataangamia, bali anayesikiliza ataongea kwa muda wote.
Shahidi wa uongo ataangamia, bali maneno ya mwenye kusikia yatadumu.
29 Mtu mwovu huufanya uso wake kuwa mgumu, bali mtu mwadilifu ni thabiti juu ya njia zake.
Mtu mwovu ana uso wa ushupavu, bali mtu mnyofu huzifikiria njia zake.
30 Hakuna hekima, hakuna ufahamu, na hakuna shauri linaloweza kusimama kinyume na Yehova.
Hakuna hekima, wala akili, wala mpango unaoweza kufaulu dhidi ya Bwana.
31 Farasi hutayarishwa kwa siku ya mapigano, lakini ushindi hupatikana kwa Yehova.
Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita, bali ushindi huwa kwa Bwana.

< Mithali 21 >