< Mithali 20 >

1 Divai ni dhihaka na kinywaji kikali ni mgomvi; anayepotea kwa kunywa hana busara.
Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.
2 Kumwogopa mfalme ni kama kumwogopa simba kijana aungurumaye, yeyote anayemkasirisha hutoa fidia ya maish yake.
Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.
3 Ni heshima kwa mtu yeyote kujiepusha na mafarakano, bali kila mpumbavu hurukia kwenye mabishano.
Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi, bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.
4 Mtu mvivu halimi majira ya kipupwe; hutafuta mazao wakati wa mavuno lakini hapati kitu.
Mvivu halimi kwa majira; kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama lakini hapati chochote.
5 Makusudi ndani ya moyo wa mtu ni kama maji yenye kina, bali mtu mwenye ufahamu huyateka.
Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina, lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.
6 Mara nyingi mtu husema yeye ni mwaminifu, lakini ni nani awezaye kumpata yule mwaminifu?
Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma, bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?
7 Mtu atendaye haki hutembea katika uaminifu wake na wana wake wanaofuata baada yake wanafuraha.
Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake.
8 Mfalme anayeketi kwenye kiti cha hukumu akifanya kazi za kuhukumu hupembua kwa macho yake mabaya yote yaliyoko mbele yake.
Wakati mfalme aketipo katika kiti chake cha enzi kuhukumu, hupepeta ubaya wote kwa macho yake.
9 Nani anayeweza kusema, “Nimeuweka safi moyo wangu; nipo huru na dhambi zangu”?
Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi; mimi ni safi na sina dhambi?”
10 Mizani tofauti na vipimo visivyosawa - Yehova huvichukia vyote.
Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, Bwana huchukia vyote viwili.
11 Hata kijana hujulikana kwa matendo yake, kwa mwenendo wake kama ni safi na uadilifu.
Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili.
12 Masikio yanayosikia na macho yanayoona- Yehova aliyafanya yote.
Masikio yasikiayo na macho yaonayo, Bwana ndiye alivifanya vyote viwili.
13 Usipende usingizi au utakuwa masikini; fumbua macho yako na utakuwa na vyakula tele.
Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.
14 “Mbaya! Mbaya!” anasema mnunuzi, lakini akiondoka anajisifu.
“Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.
15 Ipo dhahabu na mawe ya thamani, lakini midomo yenye maarifa ni kito cha thamani.
Dhahabu kunayo, na marijani kwa wingi, lakini midomo inenayo maarifa ni kito cha thamani kilicho adimu.
16 Chukua vazi kama mmiliki wake ataweka fedha kama dhamana kwa deni la mgeni, na lichukue kama anaweka dhamana kwa uzinifu.
Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo kwa ajili ya mwanamke mpotovu.
17 Mkate uliopatikana kwa ulaghai unaladha tamu, lakini baadaye kinywa chake kitajaa kokoto.
Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.
18 Mipango huimarishwa kwa ushauri na kwa mwongozo wa busara utapigana vita.
Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo.
19 Mmbea hufunua siri na kwa hiyo hupaswi kushirikiana na watu ambao huongea sana.
Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika, kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.
20 Kama mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itapulizwa katikati ya giza.
Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene.
21 Urithi uliopatikana mwanzoni kwa haraka utakuwa na mema kidogo mwishoni.
Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni.
22 Usiseme “Mimi nitakulipiza kwa kosa hili” Msubiri Yehova na yeye atakuokoa.
Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!” Mngojee Bwana, naye atakuokoa.
23 Yehova huchukia mizani isiyo sawa na vipimo vya udanganyifu si vizuri.
Bwana anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.
24 Hatua za mtu huongozwa na Yehova; namna gani basi ataifahamu njia yake?
Hatua za mtu huongozwa na Bwana. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?
25 Ni mtego kwa mtu kusema kwa pupa, “Kitu hiki ni kitakatifu” na kuanza kufikiri juu yake kwamba kina maana gani baada ya kufanya kiapo.
Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.
26 Mfalme mwenye busara huwapepeta waovu na huligeuza juu yao gurudumu la kupuria.
Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu, hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.
27 Roho ya mtu ni taa ya Yehova, hutafiti sehemu zake zote za ndani kabisa.
Taa ya Bwana huchunguza roho ya mwanadamu, huchunguza utu wake wa ndani.
28 Agano la uaminifu na udhamini humhifadhi mfalme; kiti chake cha enzi hufanywa thabiti kwa upendo.
Upendo na uaminifu humweka mfalme salama, kwa njia ya upendo, kiti chake cha enzi huwa salama.
29 Utukufu wa watu vijana ni nguvu zao na fahari ya watu wazee ni mvi zao.
Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee.
30 Mapigo yanayoleta kidonda huusafisha ubaya na vichapo hufanya sehemu za ndani kabisa kuwa safi.
Mapigo na majeraha huusafisha ubaya, nayo michapo hutakasa utu wa ndani.

< Mithali 20 >