< Hesabu 6 >

1 BWANA alinena na Musa. Akamwabia,
Bwana akamwambia Mose,
2 'Nena na wana wa Israeli, uwaambie, 'Kama mume au mke ataweka nadhiri kwa BWANA kwa kiapo maalumu cha mnadhiri, ndipo atajiepusha na divai na vileo. hatakunywa siki itokanayo na divai.
“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili ya Bwana kama Mnadhiri,
3 Asinywe kileo kitokanacho na siki au kilevi. Asinywe maji ya divai yeyote au kula zabibu mbichi wala zilizokauka.
ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine chochote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu.
4 Katika siku zote ambazo amejitenga kwa ajili yangu, asile chochote kinachotokana na zabibu, wala kitu chochote kitokanacho na makokwa hadi maganda.
Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula chochote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.
5 Wakati wote wa nadhiri yake, wembe usiipite kichwani mwake mpaka siku zake za nadhiri kwa BWANA zitimilike. Lazima ajitenge kwa BWANA. Ataziacha nywele zake zikue kichwani mwake.
“‘Kwa muda wote wa nadhiri yake ya kujitenga kwa ajili ya Bwana, wembe hautapita kichwani mwake. Ni lazima awe mtakatifu mpaka kipindi cha kujitenga kwake kwa ajili ya Bwana kiishe; ni lazima aache nywele za kichwa chake zirefuke.
6 Wakati wote wa kujidhiri kwake kwa BWANA, asiikaribie maiti.
Kwa kipindi chochote cha kujitenga kwa ajili ya Bwana hatakaribia maiti.
7 Asijinajisi kwa namna yeyote hata kama atakufa baba yake, mama, dada, au ndugu yake. Hii ni kwa sababu amejitenga kwa ajili ya Mungu, kama ambavyo kila mmoja anavyoweza kumuona kwa uerfu wa nywele zake.
Hata kama baba yake mwenyewe au mama au kaka au dada akifa, hatajinajisi mwenyewe kwa taratibu za ibada kwa ajili yao, kwa sababu ishara ya kujiweka wakfu kwake kwa Mungu ipo katika kichwa chake.
8 Wakati wote wa kujidhiri kwake atakuwa mtakatifu, alijitunza kwa ajili ya BWANA.
Kwa kipindi chote cha kujitenga kwake yeye ni wakfu kwa Bwana.
9 Ikitokea mtu amekufa ghafla pembeni yake na kukitia unajisi kichwa chake kitakatifu, ndipo atakaponyoa kichwa chake katika siku ya kujitakasa —Siku ya saba atanyoa kichwa chake.
“‘Kama mtu yeyote akifa ghafula karibu naye, atakuwa ametiwa unajisi nywele zake alizoziweka wakfu, hivyo ni lazima anyoe nywele zake siku ya utakaso wake, yaani siku ya saba.
10 Siku ya nane atamletea kuhani njiwa wawili au makinda mawili ya njiwa kwenye lango la hema ya kukutania.
Kisha siku ya nane ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani katika mlango wa Hema la Kukutania.
11 Naye kuhani atamtoa ndege mmoja kama sadaka ya dhambi na mwingine kama sadaka ya kuteketezwa. Hawa watafanyika sadaka ya upatanisho kwake kwa sababu atakuwa ametenda dhambi ya kuwa karibu na mfu. Atatakasika kichwa chake siku hiyo.
Kuhani atatoa mmoja kama sadaka ya dhambi, na mwingine kama sadaka ya kuteketezwa ili kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa sababu ametenda dhambi kwa kuwepo mbele ya maiti. Siku iyo hiyo atakiweka wakfu kichwa chake.
12 Atajitenga kwa BWANA tena katika siku hizo za utakaso. Ataleta kondoo mume mwenye umri wa mwaka mmoja kama sadaka ya hatia. Zile siku zake kabla ya kunajisika hazitahesabiwa, kwa sababu kujiweka wakfu kwake kulinajisika.
Ni lazima ajitoe kabisa kwa Bwana kwa kipindi cha kujitenga kwake, na ni lazima atoe mwana-kondoo wa mwaka mmoja kama sadaka ya hatia. Siku zilizopita hazitahesabiwa kwa sababu alijitia unajisi katika siku zake za kujitenga.
13 Hii ndiyo sheria ya mnadhiri wakati wa muda wa kujidhiri unapokuwa umetimia. Ataletwa kwenye mlango wa hema ya kukutania.
“‘Basi hii ndiyo sheria kwa ajili ya Mnadhiri baada ya kipindi chake cha kujitenga kupita. Ataletwa kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
14 Ataleta sadaka yake kwa BWANA. Atatoa mwanakondoo mume wa mwaka mmoja asiye na hila kama sadaka ya kuteketezwa. Ataleta kondoo mke wa mwaka mmoja asiye na hila kama sadaka ya dhambi. Ataleta kondoo mume asiye na hila kama sadaka ya amani.
Hapo atatoa sadaka zake kwa Bwana: yaani, mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kondoo mke wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya amani,
15 Ataleta kikapu cha mikate iliyotengenezwa bila amira, mikate ya unga mwembamba iliyokandwa kwa mafuta, mikate ya kaki isiyo na amira iliyopakwa mafuta, pamoja na sadaka za unga na sadaka za vinywaji.
pamoja na sadaka zake za nafaka na za vinywaji, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, yaani maandazi yaliyotengenezwa kwa unga laini uliochanganywa na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta.
16 Kuhani atawaleta mbele za BWANA. Atazitoa hizo sadaka zake za dhambi na kuteketezwa.
“‘Kuhani atavileta vitu hivyo mbele za Bwana na kufanya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa.
17 Na kikapu cha mikate isiyowekwa amira, atamtoa yule kondoo mume kama sadaka ya amani kwa BWANA. Pia kuhani atatoa hiyo sadaka ya unga na sadaka ya vinywaji.
Ataleta pia kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, na atatoa dhabihu kondoo dume kama sadaka ya amani kwa Bwana, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka ya kinywaji.
18 Mnadhiri atanyoa nywele zake kama ishara ya kujitenga kwa ajili ya Mungu kwenye mlango wa hema ya kukutania. Atazitoa nywele zake kichwani kwake na kuzichoma kwa moto ulio chini ya sadaka ya amani.
“‘Kisha kwenye ingilio la Hema la Kukutania, Mnadhiri ni lazima anyoe nywele zake ambazo alikuwa ameziweka wakfu. Atazichukua hizo nywele na kuziweka ndani ya moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka ya amani.
19 Kuhani atachukua bega la kondoo mume lililotokoswa, na mkate usiotiwa amira toka kikapuni, na mkate mmoja wa kaki usiotiwa amira. Atauweka kwenye mikono ya Mnadhiri baada ya kuwa amenyoa nywele kwa ishara ya kujidhiri.
“‘Baada ya Mnadhiri kunyoa hizo nywele zake za kujitenga kwake, kuhani atampa mikononi mwake bega la kondoo dume lililochemshwa, na pia andazi na mkate mwembamba kutoka kwenye kikapu, vyote vikiwa vimetengenezwa bila kuwekwa chachu.
20 Kisha kuhani atavitikisa kuwa sadaka kwa BWANA, sehemu takatifu kwa kuhani, pamoja na kidari cha kutikiswa na paja lililotolewa kwa kwa kuhani. Baadaye, Mnadhiri anaweza kunywa divai.
Kisha kuhani ataviinua mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua; ni vitakatifu na ni mali ya kuhani, pamoja na kile kidari kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. Baada ya hayo, Mnadhiri anaweza kunywa divai.
21 Hii ndiyo sheri ya Mnadhiri anayeapia sadaka yake kwa BWANA kwa ajili ya kujidhiri kwake. Chochote atakachotoa, lazima afanye kama alivyoapa, kuilinda ahadi yake kama ilivyoaniswa katika sheria ya Mnadhiri.
“‘Hii ndiyo sheria ya Mnadhiri ambaye anaweka nadhiri kwa matoleo yake kwa Bwana kufuatana na kujitenga kwake, zaidi ya chochote kile anachoweza kupata. Ni lazima atimize nadhiri aliyoiweka kufuatana na sheria ya Mnadhiri.’”
22 Tena BWANA akanena na Musa, akasema,
Bwana akamwambia Mose,
23 “nena na Harunu na wanawe. Uwaambie, 'mtawabariki wana wa Israeli kwa njia hii. Mtawaambia,
“Mwambie Aroni na wanawe, ‘Hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli. Waambieni:
24 BWANA na awabariki na kuwatunza.
“‘“Bwana akubariki na kukulinda;
25 BWANA na awaangazie nuru ya uso wake na awe mwenye neema kwenu.
Bwana akuangazie nuru ya uso wake na kukufadhili;
26 BWANA na awatazame kwa neema na awape amani.'”
Bwana akugeuzie uso wake na kukupa amani.”’
27 Ni kwa jinsi hii kwamba wanaweza kuwapa jina langu wana wa Israeli.”
“Hivyo wataliweka Jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.”

< Hesabu 6 >