< Mathayo 23 >
1 Baadaye aliongea na umati wa watu na wanafunzi wake. Akasema,
2 “Waandishi na Mafarisayo wanakalia kiti cha Musa.
3 Kwa hiyo chochote wanacho waamuru kufanya, fanyeni huku mkiwachunguza. Lakini msije mkaiga matendo yao, kwa sababu wao hutamka mambo wasiyoyafanya.
4 Kweli, wao hufunga mizigo mizito ambayo ni vigumu kuibeba, na kisha huwabebesha watu mabegani mwao. Lakini wao wenyewe hawasogezi hata kidole kuibeba.
5 Matendo yao yote, huyafanya ili watazamwe na watu. Kwa sababu wao hupanua masanduku yao na huongeza ukubwa wa mapindo ya mavazi yao.
6 Wao hupendelea kukaa maeneo ya kifahari katika sherehe na katika viti vya heshima ndani ya masinagogi,
7 na kusalimiwa kwa heshima maeneo ya sokoni, na kuitwa “Walimu” na watu.
8 Lakini ninyi hampaswi kuitwa “Walimu,” Kwa kuwa mnaye Mwalimu mmoja, na ninyi wote ni ndugu.
9 Msimuite mtu yeyote hapa duniani kuwa baba yenu, kwa kuwa mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni.
10 Wala msije kuitwa 'walimu,' kwa kuwa mnaye Mwalimu mmoja tu, yaani Kristo.
11 Bali aliye mkubwa miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.
12 Yeyote ajiinuae atashushwa. Na yeyote anaye jishusha atainuliwa.
13 Lakini ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Mnawafungia watu ufalme wa mbinguni. Nanyi hamwezi kuuingia, na hamwaruhusu wanaoingia kufanya hivyo.
14 (Zingatia: Msitari wa 14 hauonekani katika nakala bora za kale. Baadhi ya nakala huongeza msitari huu baada ya msitari wa 12. Msitari wa 14 “Ole wenu wandishi na Mafarisayo wanafiki! Kwa kuwa mnawameza wajane”).
15 Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Mnavuka ngambo ya bahari na kufika kumfanya mtu mmoja aamini yale mnayoyafundisha, na anapokuwa kama ninyi, mnamfanya mara mbili mwana wa jehanamu kama ninyi wenyewe mlivyo. (Geenna )
16 Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Yeyote aapaye kwa hekalu, si kitu. Lakini anayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amefungwa na kiapo chake.
17 Enyi vipofu wapumbavu, kipi ni kikubwa kuliko kingine, dhahabu au hekalu ambalo limeweka wakfu dhahabu kwa Mungu?
18 Na, yeyote aapaye kwa madhabahu, si kitu. Bali anayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amefungwa na kiapo chake.
19 Enyi watu vipofu, kipi ni kikubwa kuliko kingine, sadaka au madhabahu ambayo huweka wakfu sadaka zinazotolewa kwa Mungu?
20 Kwa hiyo, yeye aapaye kwa madhabahu huapa kwa hiyo na kwa vitu vyote vilivyo juu yake.
21 Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo na kwa yeye akaaye ndani yake.
22 Na yeye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketie juu yake.
23 Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka kwa bizali, mnaanaa na mchicha, lakini mnaacha mambo mazito ya sheria- haki, rehema, na imani. Lakini haya mnapaswa kuwa mmeyafanya, na siyo kuacha mengine bila kuyatekeleza.
24 Enyi viongozi vipofu, ninyi ambao mnachuja mdudu mdogo lakini mnameza ngamia!
25 Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya vikombe na nje ya sahani, lakini ndani pamejaa dhuluma na kutokuwa na kiasi.
26 Enyi Mafarisayo vipofu, safisheni kwanza ndani ya kikombe na ndani ya sahani, ili upande wa nje nao pia uwe safi.
27 Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo kwa nje huonekana mazuri, lakini kwa ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila kitu kilicho kichafu.
28 Vivyo hivyo, nanyi kwa nje mwaonekana wenye haki mbele ya watu, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na udhalimu.
29 Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mwajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki.
30 Ninyi mwasema, kama tungeishi siku za baba zetu, tusingekuwa tumeshiriki pamoja nao kumwaga damu za manabii.
31 Kwa hiyo mwajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni watoto wa hao waliowaua manabii.
32 Pia ninyi mnakamilisha kujaza sehemu inayostahili dhambi ya baba zenu.
33 Enyi nyoka, wana wa vipiribao, kwa namna gani mtaikwepa hukumu ya jehanamu? (Geenna )
34 Kwahiyo, tazama, nawatuma kwenu manabii, watu wenye hekima, na waandishi. Baadhi yao mtawaua na kuwasulibisha. Na baadhi yao mtawachapa ndani ya masinagogi yenu na kuwafukuza kutoka mji mmoja hadi mwingine.
35 Matokeo ni kwamba juu yenu patatokea damu zote za wenye haki zilizomwagwa duniani, kuanzia damu ya Habili mwenye haki hadi kwa damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliye muua kati ya patakatifu na madhabahu.
36 Kweli, nawaambieni, mambo haya yote yatakipata kizazi hiki.
37 Yerusalemu, Yerusalemu, wewe unayewaua manabii na kuwapiga mawe wale ambao wanatumwa kwako! mara ngapi nimewakusanya watoto wako pamoja kama vile kuku awakusanyavyo vifaranga wake chini ya mbawa zake, lakini haukukubali!
38 Tazama, nyumba yako imebaki ukiwa.
39 Nami nakuambia, Kuanzia sasa na kuendelea hautaniona, hadi utakaposema, 'Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.”'